Saturday , 2 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Vigogo 600 wamtembelea Lissu hospitali
Habari za Siasa

Vigogo 600 wamtembelea Lissu hospitali

Samia Suluhu, Makamu wa Rais akimsalimia Tundu Lissu alipokuwa hospitali Nairobi
Spread the love

JUMLA ya wageni 617 walimtembelea kumjulia hali Tundu Lissu akiwa kitandani ndani ya Hospitali ya Nairobi, Kenya alimokuwa akipatiwa matibabu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Lissu alilazwa kwa miezi minne- kuanzia Septemba 7, mwaka jana hadi Januari 6, mwaka huu.

Idadi hiyo ni baada ya watu kuruhusiwa kumuona na kumsalimia Lissu akiwa kitandani kuanzia Novemba, mwaka jana hadi – Januari 5, siku moja kabla ya kuondoka kuelekea Brussels, Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

Tundu Lissu alishambuliwa Septemba 7, mwaka jana akiwa nje ya nyumba yake, mjini Dodoma, akiwa anatoka kwenye vikao vya bunge.

Miongoni mwa watu mashuhuri – kutoka Tanzania waliomtembelea Lissu ni Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Rais (mstaafu) wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Jaji Mkuu (mstaafu) Othman Chande na baadhi ya wabunge.

Wamo pia baadhi ya viongozi wa serikali ambao walifika kumusabahi, ingawa hawakutaka kujulikana. Haijawekwa wazi walikuwa wakihofia nini na endapo ulitolewa waraka wa kuwazuia au la?

Viongozi waandamizi wa Kenya waliomtembelea Lissu ni pamoja na Makamu wa Rais (mstaafu) Kalonzo Musyoka, Jaji Mkuu wa Kenya (mstaafu), Willy Mutunga, wanasiasa waandamizi na viongozi wengine wa serikali.

Je, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta au makamu wake, William Ruto walifika au kutuma salamu kwa Lissu?

“Siwezi kusema hapa kama walifika au kutuma salamu, maana hili litaingilia sana masuala ya diplomasia ya Tanzania na Kenya, hivyo siwezi kulijibu,” anasema Ally Hemed, Mkuu wa Kitengo Uenezi (Chadema).

Hemed anasema viongozi wengi wa serikali ya Kenya, wanasheria, wanasiasa, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida, walikuwa wakifika hospitali kumsalimia Lissu.

“Tumekuwa na faraja sana kuona hata wananchi wa kawada wa Kenya, siyo kutoka hapa Nairobi tu, hata maeneo ya pembezoni, walifika kwa wingi kumsalimia na kumpa pole mheshimiwa Lissu,” alisema Hemed ambaye amekuwa Nairobi akisaidia kumuuguza mbunge huyo wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Nairobi, Lissu alisema amefarijika sana kuona watu wa rika, vyeo na hali tofauti wakija kumsalimia na kumpa pole.

“Wako watu sijawahi kuwaona wala kuwasikia, lakini wamekuja kuniona, wengine wametoka nje ya Afrika, hakika Mungu ni mwema na hakupanga kuwaacha wauaji wangu wanimalize.

“Wako watu walisafiri kutoka vijijini, mbali kabisa ya Kenya, kutoka Tanzania, walikuja kuniona, nilifarijika sana.

“Yuko mzee mmoja alitoka moja ya vijiji vya mbali kabisa na Dar es Salaam, huyu alisema amechanga senti zake hata akapata nauli ya kumfikisha Nairobi, Kenya kuja kunisalimia, nilifurahi sana,” alisema Lissu, akionesha tabasamu.

Lissu alisema ujio wa mzee huyo na wengine asiowafahamu wala kuwa na ukaribu nao, kulimfanya kuona ana deni la kuendelea kuwatumikia Watanzania kabla hajafa.

“Kabla sijafa, napenda kuwekeza kwenye utetezi wa haki, kuwatumikia wananchi na kuhakikisha Tanzania yenye neema kwa kila mmoja ainapatikana,” aliongeza Lissu.

Dereva taksi – namba za usajili KCH 327K, Kamau Ndung’u anayefanya shughuli zake Jiji la Nairobi, akizungumza na Mwanahalisionline alisema Wakenya wanamzunguza sala Lissu na aliporuhusiwa kumusalimia hospitali, wengi tulienda kumuona.

Je, wengi mlimfahamu kabla ya jaribio la kuuawa kwa Lissu? Kamau alisema, waliokuwa wakifuatilia siasa za Tanzania walimjua, lakini wengi tumemuona baada ya kushambuliwa.

Lissu ambaye kwa sasa anaendelea na matibabu Brussels, Ubelgiji, alishambuliwa na wale wanaoitwa – “watu wasiojuliakana,” akiwa nje ya nyumba anamoishi, Area D- estate 3, eneo pia wanaloishi mawaziri, Desemba 7, mwaka jana.

Hadi sasa hakuna taarifa ya kukamatwa kwa watu waliofanya shambulizi hilo mchana – saa saba ndani ya eneo lenye ulinzi wa saa 24 unaofanywa na vyombo vya usalama.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia kuzindua programu ya nishati safi ya kupikia kwa wanawake Afrika

Spread the loveRais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua programu ya...

Habari za Siasa

AG aiagiza kamati ya maadili kuwashughulikia mawakili wanaokiuka maadili

Spread the loveMWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Eliezer Feleshi, ameagiza Kamati...

Habari za Siasa

Jaji avunja ukimya sakata la Mpoki kusimamishwa uwakili

Spread the loveJAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, amekitaka Chama cha...

Habari za Siasa

Sheikh Ponda ataka mwarobaini changamoto uchaguzi 2020

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa...

error: Content is protected !!