Tuesday , 16 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kigwangalla ni ‘juha’ – Sumaye              
Habari za SiasaTangulizi

Kigwangalla ni ‘juha’ – Sumaye              

Spread the love

WAZIRI mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameshangazwa na hatua ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, kumtuhumu kupitia vyombo vya habari, kuwa ni mmoja wa viongozi serikalini, waliojimilikisha viwanja vya umma, jijini Arusha. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

“Yule Kigwangalla, ni juha. Ni mtu anayependa sifa na kukurupuka. Binafsi, achilia mbali kuwa na nyumba, sina hata kiwanja jijini Arusha,” anaeleza Sumaye.

Amesema, “huyu bwana (Kigwangalla), amezoea kuchafua viongozi wenzake kwenye magazeti. Amezoea kusingizia watu kwa maslahi binafsi na ambayo yeye ndio anayejua faida zake.”

Sumaye alikuwa akujibu swali la mwandishi wa habari hizi juu ya madai kuwa kiongozi huyo, ni miongoni mwa watumishi wa umma, waliojimilikisha maeneo ya serikali.

Kuibuka kwa Sumaye kumefuatia madai yaliyoporomoshwa na Dk. Kigwangalla, Jumatatu iliyopita, kuwa watu 83, wamejimilisha viwanja katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), jijini Arusha.

Kigwangalla alitoa tuhuma hizo nzito wakati akizungumza na wajumbe wa bodi mpya ya shirika la hilo.

Mwingine aliyetajwa na Kigwangalla, ni aliyekuwa waziri mkuu wa kwanza katika serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na ambaye katika uchaguzi mkuu uliopita, alijitosa katika mbio za urais, kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa.

Kwa sasa, Lowassa na Sumaye, ni wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katika mahojiano yake na gazeti hili, Sumaye anasema, “kwa mtu mwenye akili timamu, hawezi kuibuka na kutuhumu wenzake bila kuwauliza. Ukimuona mtu anafanya hivyo, basi jua kuwa ndani ya kichwa chake, kuna matatizo.”

Anasema, “mimi nilikuwa kiongozi serikalini, nafahamu miiko ya uongozi. Nafahamu miiko ya kazi. Kiongozi wa umma, hawezi kuamka na kuanza kutuhumu watu, bila kuwasikiliza.”

Sumaye ambaye alikuwa waziri mkuu kwa miaka 10 ya utawala wa Benjamin Mkapa – 1995 hadi 2005 – anasema, ni makosa makubwa kwa kiongozi wa serikali kutenda kazi kwa maneno ya kuambiwa au hisia zake binafsi.

“Kigwangalla anafahamu ninapoishi. Anafahamu simu yangu. Uongozi bora, unamuelekeza kabla ya kunituhumu, angenitafuta ili kupata ukweli wa madai yake. Lakini kwa kuwa ni mtu wa kukurupuka, hakufanya hivyo,” ameeleza Sumaye.

Anaongeza, “mtu juha, ndiye ambaye hawezi kuuliza. Huyo akisikia jambo analirukia. Napenda kuuhakikishia umma, kuwa mimi Frederick Tluway Sumaye, sina nyumba wala kiwanja, jijini Arusha.

“Hivyo basi, madai yote ya Kigwangalla dhidi yangu, naomba yapuuzwe. Sina nyumba yoyote Arusha sasa kama anadhani yeye kazi yake ni kuwachafua watu acha aendelee, nitampeleka mahakamani.”

Kigwangalla aliwataja viongozi wengine aliodai wanamiliki nyumba katika kiwanja cha shirika la hifadhi ya Ngorongoro, kuwa ni pamoja na Daniel ole Njoolay.

Hata hivyo, katika hali inayothibitisha madai ya Sumaye kuwa waziri huyo amekurupuka, Kigwangalla anasema, “…tusubiri tupate majibu toka kwa mamlaka inayohusika na kutoa hati za umiliki wa ardhi.”

Waziri Kigwangalla alitoa kauli hiyo kujibu andishi la mtoto wa Lowassa – Fredrick Lowassa (Fred) – kuwa baba yake, hahusiki na tuhuma hizo.

“Mdogo wangu Fredrick Lowassa, tulia usiwe na hofu. Sikukurupuka kuhusu issue ya mzee wako, Ndg. Edward Lowassa, kama ana kiwanja ama la, kwenye eneo la Plot. No. 4091 Njiro Arusha.”

Anasema, “kuna majina mengi makubwa yanasemwa, yakiwemo ya mawaziri wakuu wastaafu, Ndg. Frederick Sumaye na Ndg. Edward Lowassa, watumishi wa zamani wa mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro na Bodi ya Utalii, kuna mkuu wa mkoa wa zamani Ndg. Ole Njoolay anatajwa.

“Kuna waziri wa zamani, Ndg. Batilda Buriani, Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro, Ndg. Mshana Joseph na wengine wengi, lakini hatuwezi kuwahukumu ama kuwataja waziwazi kwa sasa mpaka tupate nyaraka maana inawezekana wanasingiziwa ama vipi.”

Katika ujumbe wake, Fred anasema, “nikiwa kama msemaji wa familia ninazo katika kiganja cha mikono yangu taarifa zote za umiliki wowote unaomgusa Lowassa.”

Amesema, “ninaweza kuuhakikishia umma kwamba yote aliyosema Kigwangalla hayapo; kama anayo basi sisi tuko tayari afanye lolote lililo chini ya mamlaka yake. Tumechoka kurejea kule tulikopita ambako yeye na wenzake kadhaa walifanya bila mafanikio kuchafua heshima za wote anaowataja bila sababu.”

Naye Njoolay, ambaye amewahi kuwa mkuu wa mikoa ya Mwanza, Arusha na Rukwa pamoja na kukiri kuwa anamiliki kiwanja jijini Arusha anasema, “niliwahi kuwa kiongozi serikalini, siwezi kuwa mvamizi. Jiji lilitangaza viwanja na sisi tukaomba na kupatiwa kama wananchi wengine.”

Anasema, “kama Kigwangalla alitaka kupata ukweli angekutana na sisi kwanza. Angesikiliza kabla ya kutuhumu. Huo ndio utawala bora. Serikali haifanyi kazi kwa matamko, kama suala hili lipo tunasubiri barua, tutajibu kila kitakachoulizwa.”

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Samia arejesha mikopo ya 10%, bilioni 227.96 zatengwa

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amerejesha utaratibu wa utoaji mikopo...

Habari za Siasa

Rais Samia amfariji mjane wa Musa Abdulrahman

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan leo Jumanne amempa pole Mwanakheri Mussa...

Habari za Siasa

Nape: Wanasiasa, wanahabari, wafanyabiashara mteteeni Samia

Spread the loveWaziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,...

Habari za Siasa

CAG: TAWA imegawa vibali vya uwindaji bila idhini ya waziri

Spread the loveRIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali...

error: Content is protected !!