Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu: Kiburi cha Mbowe kimeniokoa
Habari za SiasaTangulizi

Lissu: Kiburi cha Mbowe kimeniokoa

Tundu Lissu, Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki akiwa hospitali ya Nairobi nchini Kenya
Spread the love

UAMUZI wa kumsafirisha haraka Tundu Lissu, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kwenda Nairobi, Kenya kwa matibabu, kuliokoa maisha yake. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Aliyesimama kidete kuhakikisha Lissu anasafirishwa kwenye Nairobi kwa matibabu zaidi ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe. 

“Pamoja na jitihada zote za madaktari wa Hospitali ya Dodoma, ambako nilipewa huduma za awali kuokoa maisha yangu, uamuzi wa Mbowe na wengine wachache, hakika ni kipimo kikubwa cha uhai wangu hata leo,” alisema Lissu wakati akihojiwa na mwandishi wetu kitandani kwake, ndani ya Hospitali ya Nairobi, Januari 5, siku moja kabla ya kusafirishwa kwenda Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

“Wengi nimewashukuru, hasa madaktari wa Dodoma na Nairobi, lakini kwa namna ya pekee, niweke wazi hili, kwamba kiburi cha chairman (mwenyekiti) Mbowe, kiliokoa uhai wangu na hata sasa naendelea kupumua…

“Nimeelezwa kuwa kulikuwepo mvutano wa hospitali gani nipelekwe baada ya kutibiwa Dodoma, kwamba iwe Dar es Salaam au eneo jingine ndani ya Tanzania, lakini Mbowe alikataa kupelekwa eneo jingine lolote, isipokuwa Nairobi…

“Mbowe naambiwa alisimama imara na kueleza waziwazi kuwa Lissu atatibiwa Nairobi, huku wengine wakianza kususa…

“Hakika isingekuwa kiburi cha kupingana na wengine, wakiwamo baadhi ya vigogo wa serikali, waliopendekeza nipelekwe Dar es Salaam, msingekuwa na Lissu ambaye, angalau sasa anaishi, licha ya kuwepo juu ya kitanda cha hospitali kwa miezi minne leo,” aliongeza.

Taarifa zinaeleza kuwa “kiburi” cha Mbowe kilishinda uamuzi wa awali na mapendekezo ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai na viongozi wengine wa serikali waliotaka Lissu apelekwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Kudhihirisha shukrani kwa Mbowe, katika mahojiano maalum na Mwanahalisionline, siku moja kabla ya kuruhusiwa kutoka Hospitali ya Nairobi, Lissu alimtaja Mbowe mara 16, ndani ya dakika 42 za mahojiano hayo.

“Nakushukuru sana mwenyekiti Mbowe” ndiyo maneno yaliyotamkwa na Lissu mara kwa mara.

Lissu ambaye alisafirishwa usiku kwa ndege ya kukodi kutokea Dodoma Septemba 7, mwaka jana alishambuliwa kwa risasi siku hiyohiyo mchana, akiwa nje ya nyumba anamoishi, Area D – Site 3, wanakoishi mawaziri na viongozi wengine waandamizi wa serikali.

Lissu alishambuliwa akiwa ametoka kwenye kikao cha bunge na alikuwa akielekea nyumbani kwa mapumziko na kupata chakula cha mchana.

Waliomshambulia mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema) hadi sasa hawajakamatwa. Jeshi la Polisi limeeleza kuwa Lissu alishambuliwa na “watu wasiojulikana.”

Mbowe aliyekuwa Nairobi wiki iliyopita aliiambia Mwanahalisionline kuwa uamuzi wa kumsafirisha Lissu kwenda Nairobi, haukuwa rahisi, ilibidi kung’ang’ania baada ya kushindwa kukubaliana na baadhi ya viongozi waliokuwepo Dodoma.

“Nashukuru sana kwamba sasa afya ya mheshimiwa Lissu inaendelea kuimarika, hii ni faraja kubwa kwetu na hasa wapenda amani na ukomavu wa demokrasia…

“Uamuzi ule ulikuwa na nguvu ya kipekee, kwani ndiyo uliosababisha Lissu kuwa hai hata sasa, vinginevyo siku ile kungekuwa na taarifa zenye huzuni zaidi, tunamshuuru sana Mungu kwa hatua ile na hata muda huu anaendelea kumpigania,” alisema Mbowe.

Mbowe kama ulivyo msimamo wa Lissu na viongozi wengine wa vyama siasa wanavyoamini, shambulio kwa Lissu lilikuwa na dhamira kuu ya kisiasa; “kummaliza Lissu” kwa kuwa amekuwa mkosoaji mkubwa wa utendaji wa Rais John Magufuli.

Pamoja na msimamo huo, serikali imeshindwa kutoa maelezo ya kukanusha au kukubali na kubaki kueleza kuwa “Lissu ni mgonjwa, aachwe apone, serikali haiwezi kujibishana na mgonjwa.”

Msimamo huo wa serikali umekuwa ukitolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dk. Hassan Abbasi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

DA, ANC waridhia kuunda serikali ya mseto Afrika Kusini

Spread the loveChama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC,...

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

Mataifa Afrika Mashariki yawasilisha bajeti 2024/2025 inayolenga kukuza uchumi

Spread the loveMataifa manne ya Afrika Mashariki jana Alhamisi yamewasilisha bungeni bajeti...

Habari za SiasaTangulizi

Gesi asilia, petroli kodi juu

Spread the loveWaziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amependekeza kufanya marekebisho kwenye...

Habari za SiasaTangulizi

Bilioni 155.4 kugharamia kicheko cha wastaafu 2022-2030

Spread the loveWaziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema jumla ya Sh...

error: Content is protected !!