July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ukatili: Mke adaiwa kuuawa na mumewe, kiwiliwili chatenganishwa, viungo vyatawanywa

Spread the love

 

KATIKA hali ya kushangaza na kusikitisha, mkazi wa kitongoji cha Lubela, mtaa wa Nyashimbi kata ya Mhongolo wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga, Bundala Mathew anashikiliwa na Polisi, kwa tuhuma ya kumuua mkewe, Rehema Nyamgila kwa kumcharanga mapanga. Anaripoti Mwandishi Wetu, Shinyanga … (endelea).

Imedaiwa mwanamume huyo baada ya kutekeleza mauaji hayo, alitenganisha viungo vya mwili wa mkewe na kuchukua baiskeli na kuvisafirisha mpaka mbugani usiku wa manane na kuvitawanya ili kupoteza ushahidi.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo, Magdalena Katambi ambaye ni mtu wa karibu na familia hiyo, alidai kuwa tukio hilo liligunduliwa na mtoto wa marehemu, Ezekiel Bundala tarehe 27 Mei 2022.

Bundala alitoa taarifa kwake na akazifanyia kazi hata kukamatwa kwa mhalifu huyo, kutokana na ukatili aliomfanyia mkewe.

“Kwa kweli hili tukio lilitutia simanzi kubwa kijijini kwetu, na ni la aina yake ambalo halijawahi kutokea, kwa kweli sikuwa na hili wala lile, siku hiyo nilikwenda nyumbani kumjulia hali mtoto aliyekuwa anaumwa, ndipo Ezekia akanishirikisha jambo hilo,” alisema Shuhuda huyo na kuongeza:

“Ilikuwa kati ya saa moja na saa mbili usiku, wakati wanapika ndipo mtoto akaniambia mama hatunaye duniani, tangu Jumatano mama hapatikani hata kwenye simu, na uthibitisho kamili niliona simu kwenye viatu vya baba, nikakaa kimya, lakini baadaye nikaona beseni na baiskeli vina damu,” alisema shuhuda.

Kwa mujibu wa shuhuda huyo alidai mtoto alipombana baba yake kuhusu beseni kuwa na damu nyingi, baba alichomjibu mwanawe, ni kwamba hiyo ni rangi tu na si damu, kijana hakuridhika baba ake alipotoka ndani aligusa beseni kwa mkono na kunusa akagundua ni damu tena mbichi.

Shuhuda huyo anaendelea kusimulia kuwa hatua aliyoichukua kijana ni kuwasiliana na kaka yake aliye Masumbwe wilaya ya Mbogwe, Geita ili washirikiane juu ya tukio hilo na kwamba hata baadhi ya viungo baba yake alivileta nyumbani.

Alidai walitoa taarifa kwa viongozi waliopuliza king’ora cha mwano, baada ya polisi kufika kwenye kijiji hicho na umati wa watu kukusanyika kusaka mwili mpaka saa sita usiku, mwili ulipatikana mbugani na viungo vingine ikiwamo miguu.

“Mtu amenyofolewa shingo na mikono, amekatwa kuanzia kwenye mabega, matiti yamekatwa na kunyofolewa kabisa, na sehemu za siri zimenyofolewa, magoti yamekatwa mpaka vidole vya miguu.

“Kwa kweli mtu amebaki kipande, kwa jinsi alivyotawanywa viungo, lakini tulimtambua licha ya kwamba alishaanza kuharibika,” alisema Magdalena.

Alidai Ijumaa mwili ulipelekwa kuhifadhiwa mochari ya Hospitali ya Manispaa ya Kahama na 28 Mei 2022 polisi walirudi na mtuhumiwa kuonesha mahali alipohifadhi viungo vingine vya mwili huo, ndipo kichwa kikapatikana kimezikwa juu ya kaburi la marehemu babu yake kwa mama yake, lililopo nyumbani kwake.

Magdalena alidai viungo vingine vya sehemu za siri na matiti vilipatikana karibu na mlango, kwenye mafiga ya jiko, ndipo alipozika, huku akitaka watoto wake wapikie hapo mara kwa mara, kwani ameweka mbayuwayu wake akauke kwa ajili ya kutengenezea dawa.

“Baada ya askari kumhoji tena wapi vilipo viungo vingine, aliwapeleka mbugani ulikookotwa mwili katikati ya majaruba ya mpunga ilipatikana mikono na magoti, lakini wakati huo vidole vya mikono na miguu havikuonekana, kwa kweli tukio hili limetusikitisha na kutuachia simanzi kubwa,” alisema Magdalena.

Hata hivyo, mama mzazi wa mtuhumiwa, Mhoja Bundala alidai kupata taarifa kwa watu kuwa mwanawe ameachana na mkamwana wake, hivyo akawa anasubiri taarifa rasmi kutoka kwake, lakini ajabu aliletewa taarifa za tukio hilo la kushitua.

“Kwa kweli tukio hili linanishangaza, ni majuzi tu nilisikia kwa watu kuwa mwanangu ameachana na mkewe, chanzo cha ugomvi wao sikijui, hivi ndiyo nilikuwa nasubiri aje kuniambia, maana sina uwezo wa kutembea, umri wangu ni mkubwa sana.

“Lakini nashangaa kuletewa tukio la mauaji na nimekuja nimethibisha, kweli mkamwana wangu amefariki dunia,” alisema Mhoja.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyashimbi, Peter Nzingula alisema tukio hilo lilitokea usiku wa Mei 27 mwaka huu kwa mama Rehema Nyamgila kukatwa mapanga na mumewe, Bundala Mathew.

Mwenyekiti huyo alisimulia, kuwa kichwa kilitenganishwa na kiwiliwili, mikono na miguu halikadhalika, huku matiti na sehemu za siri vikinyofolewa na akathubutu kwenda kuzika mwenyewe na viungo akivitapanya majarubani ambako wananchi wanalima mpunga.

“Baada ya kupata taarifa kwa majirani waliofikishiwa na mtoto wa marehemu, tulitoa taarifa kwa vyombo vya Dola na cha kumshukuru Mungu, polisi walitusaidia kubaini tukio hilo, na mtuhumiwa alihojiwa akakiri kutenda unyama huo kwa kinywa chake,” alisema Mwenyekiti na kuongeza:

“Alipohojiwa chanzo cha kufanya unyama huo, alidai alikuwa na wivu wa mapenzi.

“Watu waliokwenda kuvuna mpunga walitwambia waliona kiwiliwili ikaturahisishia, kwa kuwa taarifa kwa mujibu wa maelezo yake ni kwamba mtuhumiwa alikuwa akisomba viungo kwa baiskeli vikiwa kwenye mifuko ya sandarusi, kwa lengo la kupoteza ushahidi,” alisema Nzingula.

Mwenyekiti aliendelea, kuwa hilo ni tukio kubwa na limeacha gumzo kwa wakazi wa mtaa wake na kata nzima ya Mhongolo na aliomba wananchi wasikae na kinyongo wala kuona aibu kufichua migogoro ya kifamilia kwenye ofisi za serikali na taasisi za kidini badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mhongolo, Boniphace Maziku alidai kuwa tukio hilo lilitokea kwenye kata yake Mtaa wa Nyashimbi, na alishirikiana na viongozi wa ngazi ya mtaa, kutoa taarifa sehemu husika, na sasa uchunguzi wa tukio unaendelea Polisi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, George Kyando akizungumza na MwanaHALISI Online kwa njia ya simu, alithibitisha uwepo wa tukio hilo na kuongeza kuwa uchunguzi wake unaendelea, na sheria itachukua mkondo wake. Marehemu Rehema ameacha mume na watoto wanne.

Tukio hilo linatokea wakati hivi karibuni, mfanyabiashara mkazi wa Mwanza, Said Oswayo (37) alimwua mkewe, Swalha Salum (28) na kisha kudaiwa kujiua kutokana na ugomvi wa kimapenzi, ambapo mkewe alizikwa Mwanza na yeye kuzikwa Musoma.

error: Content is protected !!