Monday , 4 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Tunastawisha ufisadi na kuchukia matunda yake
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Tunastawisha ufisadi na kuchukia matunda yake

Wapiga kura
Spread the love

BUNGE la Jamhuri linaloendelea mjini Dodoma, kwa wiki nzima limetawaliwa na mjadala juu ya ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Ripoti ya CAG imejaa ubadhirifu, wizi na ukwapuaji wa fedha za umma. Neno moja linalojumuisha hayo yote ni ufisadi. Anaandika Kondo Tutindaga…(endelea).

Pamoja na hasira zinazoonyeshwa na baadhi ya wabunge katika kujadili ripoti, inaonekana wazi kuwa wabunge wanawachukia mawaziri kuliko wanavyochukia ufisadi.

Ni ama wabunge hao wanatamani wangekuwa wao katika nafasi za kujichotea fedha hizo au wanachukia kwa sababu mawaziri wamewanyima mgawo na kuwasahau.

Lakini ukipitia ripoti mbalimbali, haraka utaona kuwa Bunge letu ndilo linaongoza kwa kustawisha ufisafi nchini.

Ni kwa sababu, Bunge lina jukumu la kutunga sheria na kuisimamia serikali, lakini Bunge hili hili na wabunge wake hao hao, ndilo linapalilia ufisadi huo.

Ukikutana na wabunge binafsi utawasikia wakieleza jinsi mawaziri wanavyowaomba na kuwapa hela ili waseme au wasiseme kuhusu wizara zao.

Matokeo yake, wabunge wengi wamegeuka omba omba, wakizurura toka wizara moja kwenda nyingine kuomba fadhila kutoka kwa mawaziri.

Wapo wanaoomba mafuta, wanaoomba tenda, wanaoomba ajira za watoto wao, wanaoomba upendeleo wa miradi mbalimbali na wanaoomba mawaziri wafike majimboni mwao, kuwapigia debe na kuwadanganya wapigakura wao.

Wakati huo huo, wabunge nao wana mizigo mingi ya kuombwa fedha na wapigakura.

Wanaombwa ada, michango ya harusi, matibabu, ajira, kusafirisha makundi ya wapigakura kwenda kutembelea Bunge, harambee nyingi majimboni na bado wanatakiwa kuendesha ofisi za chama wilayani, katani na matawini.

Pamoja na ukubwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), unaochanganywa na vitega uchumi vyake na ruzuku inayopokea kutoka serikalini, bado wabunge wake, ndio wanunuzi wa sare za chama chao.

Ni wao wanaosafirisha makundi mbalimbali na ndio hutoa mafuta ya mikutano ya hadhara. Wabunge wa aina hii, hawawezi kutumia hela ya mshahara kwa shughuli hizi.

Lazima wazipate kutoka kwa mawaziri, wakandarasi na kwa wakurugenzi wa halmashauri za miji, manispaa na majiji. Wakishazitoa kwa wapigakura, ni sharti nao watafute namna ya kulipwa kwa njia moja ama nyingine.

Huu ndio mchakato wa kustawisha ufisadi nchini hata kama wabunge hao hao hawapendi matokeo yake.

Kutokuwapo kwa upinzani ndani ya Bunge na kwenye mabaraza ya madiwani, kumechochea kwa kiwango kikubwa ufisadi huu. Hii ni kwa sababu, kutokuwapo madiwani na wabunge wa upinzani, ni sawa na kuacha banda la kuku likiwa wazi katikati ya pori lenye vicheche.

Upinzani bungeni na kwenye halmashauri ndio msingi wa kudhibiti ufisadi. Tulishangilia pale Rais John Magufuli, alipojiapiza kuua upinzani. Haya ndio matokeo yake.

Tumeupa mhimili wa serikali nguvu kubwa dhidi ya mingine kwa hiyo rais na wateule wake wana mamlaka juu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru).

Wabunge wetu wengi ni makuwadi wa mawaziri katika kuwezesha uchotaji wa fedha za serikali. Wako tayari kusimama bungeni kuwatetea mawaziri wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu wa mali ya umma.

Kundi la pili ni la wabunge wanaomsifia sana Rais hata kwa mambo ambayo hakutenda. Wanaweza kumsifia hata kwa kuleta mvua na kuzuia mafuriko!

Wakiishamaliza kazi hiyo hadharani, huanza kazi ya kuwafitini mawaziri ili waondolewe katika nafasi ili kupisha uteuzi wao.

Kundi la tatu ni wabunge omba omba kwa wafanyabiashara wakubwa nchini. Wabunge hawa tayari wanawajua wafanyabiashara walio karibu na Rais na familia yake.

Ili uteuzi uwezekane inabidi wabunge wawe karibu na wafanyabiashara hao, kuweza kuwatetea mbele ya Rais.

Baadhi ya wabunge hao na wateule wengine, wanadaiwa kuwa wanaonekana wakijitolea kuosha vyombo kwenye nyumba za baadhi ya wafanyabiashara hao! Wanatajwa hata kwa majina.

Teuzi nyingi, maamuzi ya kandarasi za kitaifa na kimataifa, vinafanyika kwanza huko kwa wafanyabiashara hao kabla ya kupelekwa serekalini kurasimishwa.

Hali ya ufisadi katika nchi yetu ni ngumu mno kushughulikiwa na Bunge hili lisilo na uhalali na pia lililozama katika tope hilo hilo la ufisadi.

Rais Samia Suluhu Hassan hawezi tena kupambana na ufisadi uliojaa katika mihimili yote wakati chombo cha kuzuia na kupambana na ufisadi, tayari kikiwa kimeng’olewa meno na kufungwa minyororo mizito.

Inahitajika katiba mpya inayopunguza madaraka na kunahitajika jitihada za kuunda vyombo huru katika kupambana na ufisadi: Takukuru, Tume Huru ya Uchaguzi, mahakama huru na bunge huru.

Bila kuchukua majukumu hayo, hatutafika kokote. Tutakuwa tunaimba wimbo huo huo na kucheza ngoma ileile kila mwaka.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Mwinyi aungana na Samia kuuaga mwili wa baba yake

Spread the loveRais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk....

Habari za SiasaTangulizi

Mtoto wa Mzee Mwinyi amwaga machozi

Spread the loveMtoto wa Hayati mzee Mwinyi, Abdullah Ali Hassan Mwinyi ameshindwa...

Habari za SiasaTangulizi

Mzee mwinyi alikuwa mwanademokrasia wa kweli

Spread the loveMtoto wa Hayati Ali Hassan Mwinyi, Abdullah Ali Hassan Mwinyi...

Habari za SiasaTangulizi

Samia: Mwinyi alikuwa maktaba inayotembea

Spread the loveRais Samia Suluhu hassan amesema Hayati rais mstaafu, Ali Hassan...

error: Content is protected !!