Monday , 4 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Bado askari wastaafu wanaonewa
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Bado askari wastaafu wanaonewa

Spread the love

RAIS wangu Samia Suluhu Hassan tunaendelea kumshukuru Mungu kwamba wote hatujambo na kwamba Yeye anazidi kutujalia afya ya roho na mwili mpaka dakika hii. Anaandika Leonard Manyama…(endelea).

Bila Mungu hatuna chochote tunachoweza kujivunia. Tunaweza kuteswa na kiburi cha uzima kudhani kwamba tunaweza kuishi kwa muda tunaotaka, lakini hakika uhai na uzima wetu uko mikononi mwa Mungu wetu kwa neema zake. Basi, ndivyo inavyompendeza Mungu sisi kuishi ili kutendeana mema.

Rais wangu mama Samia, naomba leo tena niendelee kukusihi sana ulitazame vizuri sana  jeshi letu la polisi. Kuna shida kubwa sana. Unaweza usijue lakini kwa jinsi ya taarifa zinavyotufikia, inaonekana kabisa kwamba hali si salama.

Wana wema wa nchi hii wanaweza kujiuliza kwamba kwani kuna shida gani kwenye malipo ya wastaafu wa jeshi la polisi? Ni nani anayekwamisha malipo ya maaskari hawa? Je, mtu huyo haguswi au anakingiwa kifua na wakubwa gani ambao wako juu ya sheria au ambaye ameamua kukukwamisha na kukugombanisha na maaskari hawa wastaafu?

Rais wangu mama Samia, leo naomba nikuambie kwamba walioko juu ya uonevu unaofanyika ndani ya jeshi la polisi kwenye malipo ya maaskari wastaafu, ni watu ambao hawakutakii mema. Wameamua kukuchonganisha na wastaafu na zaidi na maaskari wetu.

Kutowalipa maaskari wastaafu leo maana yake ni kuwaambia walioko kazini kwamba na wao kiama chao kinakuja siku wakistaafu. Na wao wanayaona wanayopitia wenzao, na hakika mioyo yao pia hujaa simanzi na sononeko hata kabla hawajastaafu.

Kwani kuna ugumu gani kulipa madeni ya watumishi? Rais wangu kustaafu sio kufa. Sio jambo la dharura. Kustaafu ni jambo linalojulikana ndiyo maana mhusika huandaliwa. Tena kwa jeshi la polisi, askari anayekaribia kustaafu hupewa likizo na akiimaliza, anatakiwa kurudi kazini na kukabidhi vitendea kazi vyote vya jeshi zikiwemo sare za kazi kwa ajili ya kuanza maisha mapya uraiani.

Kwa muda wote huo wa karibia miezi mitatu ya likizo, kwanini malipo ya askari yasiandaliwe ili mhusika alipwe? Lakini cha ajabu askari anastaafu bila kulipwa fedha za usafiri na mizigo kana kwamba ni malipo ya hisani. Shida iko wapi?

Rais wangu mama Samia, wasaidizi wako wanajua mchezo huu wa dhuluma inayofanywa ndani ya jeshi la polisi. Kama hawajui kwanini kila mwaka malipo ya wastaafu yanaibuka tena ikiwa ni kwa baadhi tu ya maaskari?

Kwa mfano maaskari wetu waliostaafu mwaka 2020 kwenye kundi hilo kuna waliolipwa fedha zao za usafiri na mizigo, lakini wengine wanasota mpaka leo. Na hili tangu tumeanza kulipigia kelele hakuna anayetaka kuchukua hatua.

Ukiwa na watendaji wenye vichwa ngumu namna hii, wanaoweza kupuuza mambo muhimu kama malipo halali ya watu, inatia hasira na inakuharibia wewe. Rais wangu unashindwa nini kuamuru maaskari hawa walipwe?

Wamefanya dhambi gani mpaka wasilipwe haki yao ya usafiri na mizigo? Kwani ni mkubwa gani ndani ya jeshi la polisi yuko nyuma ya uonevu huu? Au ni mkubwa gani hapo jeshini atakayestaafu halafu asilipwe fedha za mizigo na usafiri akafurahia? Kama wakubwa wanalipwa, kwanini maaskari wa chini hawa wanadhulumiwa haki yao? Kwanini kulipwa iwe hisani?

Rais wangu juzi tulipokea malalamiko ya maaskari wengine waliostaafu mwaka 2021. Baadhi ya maaskari hawa walikuwa wanalalamika kutokulipwa fedha za usafiri pamoja na mizigo. Na kwamba maaskari hawa badala ya kulipwa fedha zao hizo, wakubwa walioko kazini ambao bado wanakula kuku kwa mrija, walifanya kikao huko Kilwa Road na kuwaamuru mameja wa kambi wawatangazie maaskari katika kambi zao kuwa askari ambao hawajalipwa, fedha za nauli na mizigo, magari yameshaandaliwa kupakia mizigo yao kuwarudisha kwenye mikoa waliko tokea. Kwa maana hiyo walitakiwa kuondolewa kwenye nyumba za jeshi la polisi.

Rais wangu inasemekana kuna sehemu ambako tayari operesheni hiyo ya kuwaondoa maaskari hao kambini imeshaanza kutekelezwa. Wana wema wa nchi hii tunauliza, kwani haya yanafanyika kwa faida ya nani?

Rais wangu mama Samia, kuwaamuru maaskari wanaostaafu utumishi jeshini wafunge mizigo yao ili warudishwe mikoa waliyotoka kwa magari ya mizigo, ni utaratibu uliowekwa na nani? Je, ni kwa mujibu wa sheria? Au ndivyo utaratibu wa jeshi la polisi ulivyo?

Kama huo sio utaratibu, kwa nini watu wachache wajiundie utaratibu wao kinyume cha sheria? Rais wangu maaskari wale wanalalamika kwamba jeshi la polisi limesema wao watalipwa wakifika majumbani kwao huko mikoani.  Sisi wana wema wa nchi hii tunauliza kwa nini hawa wapiganaji wetu wakalipiwe mikoani na wasilipiwe kwenye vituo vyao vya kazi?

Tunajiuliza tena, huu utaratibu wa malipo ni kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi? Rais wangu maaskari wanalalamika kwamba kila wanapoulizia madai yao wanaambiwa  na jeshi la polisi kwamba madai yao yameingizwa kwenye madeni. Na hii ni tangu ya baadhi ya waliostaafu mwaka 2020 na wengine waliostaafu mwaka 2021.

Ikiwa hivi ndivyo, hivi ni kweli kwamba madai ya maaskari yanaweza kuingizwa kwenye madeni ya serikali? Kwamba mtumishi anaweza kuikopesha serikali? Na ilikuwaje madai ya maaskari wanaostaafu yasichakatwe sambamba na mchakato wao wa kustaafu?

Rais wangu, hawa watendaji wako wanakugombanisha na wastaafu. Tafadhali mulika ndani ya jeshi la polisi kuna sehemu tatizo lipo tena kubwa. Jitihada zetu za kutafuta ukweli wa madai haya ndani ya jeshi la polisi ziligonga mwamba baada ya msemaji wa jeshi la polisi kutojibu maswali tuliyomtumia kwa njia ya whatsap kama alivyoelekeza baada ya kumpigia simu kuomba ufafanuzi wa jambo hilo. Pamoja na kumkumbusha mara kadhaa lakini hakuonyesha ushirikiano. Kuna nini kinachofichwa?

Rais wangu nilikusikia ukisema utamtafutia mkuu wa jeshi la polisi (IJP) kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi. Naomba kama hilo linawezekana, basi umtafutie na hivyo vijisenti kiduchu wanavyodai maaskari wetu hawa wastaafu ili mkuu huyo wa jeshi la polisi pia amalizane na hawa maaskari wake waliokwisha kukoma utumishi ndani ya jeshi hilo kwa kuwalipa madai yao ya msingi. Haina maana yoyote kuwatimua kutoka kambini kwa kuwapandisba magari ya mizigo bila kuwalipa fedha zao.

Rais wangu tusiweke sumu kwenye mioyo ya watumishi. Haya wanayotendewa maaskari wastaafu na wastaafu wengine yanaweza yakaonekana ya kawaida kwa sababu wakubwa kwenye mamlaka wanayashughulikia watakavyo. Wanaweza kuendelea kuyapuuza na wanaweza hata kutunyamazisha sisi tunaoyapigia kelele.

0756888896

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Mwinyi aungana na Samia kuuaga mwili wa baba yake

Spread the loveRais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk....

Habari za SiasaTangulizi

Mtoto wa Mzee Mwinyi amwaga machozi

Spread the loveMtoto wa Hayati mzee Mwinyi, Abdullah Ali Hassan Mwinyi ameshindwa...

Habari za SiasaTangulizi

Mzee mwinyi alikuwa mwanademokrasia wa kweli

Spread the loveMtoto wa Hayati Ali Hassan Mwinyi, Abdullah Ali Hassan Mwinyi...

Habari za SiasaTangulizi

Samia: Mwinyi alikuwa maktaba inayotembea

Spread the loveRais Samia Suluhu hassan amesema Hayati rais mstaafu, Ali Hassan...

error: Content is protected !!