Wednesday , 1 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Uongozi wa Samia kuendelea hadi 2030
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Uongozi wa Samia kuendelea hadi 2030

Spread the love

KWETU sisi tuliowahi kusoma sekondari, iwe O levo au A levo, nani aliwahi kusikia tangazo la wavuta bangi kujumuika pamoja au tangazo la wazinzi wanaitana kujumuika pamoja au mabookwemu kuitana wakutane kwenye kikao cha dharura kuzungumzia masomo yao? Anaandika Nyaronyo Kicheere…(endelea).

Namaanisha hivi, wanafunzi wapya mmefika shule ya sekondari, ni mara ya kwanza kukutana na hamfahamiani. Lakini baada ya saa chache tu, unakuta wazinzi wako pamoja, walevi wako pamoja na wavuta bangi wako kikundi kimoja, sasa nauliza, nani huwakusanya na huwatambuaje? Kama ni wao wenyewe, je hutambuana vipi?

Hata vijijini mwetu, kwa wale tuliozaliwa na kukulia vijijini, kuna watu wanaitwa wachawi wanaochawia wenzao, wengine waturutumbi wanaoturutumba kwenye mazizi ya ng’ombe za majirani zao, warogi wanaoroga wenzao, wezi wanaowaibia wenzao na wagoni au wazinzi wanaotembea na wake wa majirani zao, wote hao utawakuta ni marafiki na hutembeleana.

Utasikia fulani na fulani ni marafiki na wanaturutumba pamoja yaani wakija kucheza usiku kwenye mlango wa zizi la ngombe wako, hao ng’ombe wanapata magonjwa na kufa mmoja baada ya mwingine.

Pia utasikia fulani na fulani ni marafiki na wanaroga pamoja; au fulani na fulani ni marafiki na wanaiba pamoja, sasa hawa watu waturutumbi, warogi na wezi wanachaguanaje?

Hata kwenye mikutano, semina na makongamano mambo ni hayohayo. Baada ya utambulisho na kuanza shughuli, wanasemina wakitoka kwenye kustafutahi utawakuta wameanza kugawanyika kwenye vikundi vidogovidogo.

Wazinzi wameanza kujikusanya na mazungumzo yao yanahusu wanawake waliojaaliwa mashalaa na wenye usafiri mzuri au wanazungumzia wanawake wapi wana resepusheni murua.

Ndipo wazungu Waingereza wakaja na msemo kwamba “nionyeshe marafiki zako nami nitakuambia wewe ni nani.”

Hii ni kwa sababu Waingereza wanaamini kwamba kwa kuwajua marafiki wa mtu, basi pale pale utamjua mtu huyo ni mtu wa namna gani.

Kwa msemo huu basi ukikuta mkutanoni au msibani watu wamekaa vikundi vikundi utaweza kuwajua tabia zao kwa kuwauliza majina yao.

Kikundi cha akina Mwita, Chacha na Marwa kutoka kanda maalumu hutauliza chochote kwani utafahamu hawa ni wagomvi na kikundi cha akina Kimaro, Shayo na Mmari utafahamu kuwa ni kundi la wezi.

Kadhalika ukikuta kikundi cha akina Malimi, Masanja na Shija utafahamu mara moja kuwA ni kundi la washirikina na hata kundi la akina Rugaimukamu, Rutashobororwa na Rutakomozibwa utafahamu ni kundi la wachoyo wa chakula, lakini wakarimu wa jambo fulani.

Pia Waingereza haohao wana msemo kuwa ndege wafananao, huruka pamoja na kweli kanga wana manyoya yanayofanana na wanaruka pamoja, kware wana manyoya yanayofanana na wanaruka pamoja.

Hata kerengende (ibhinyagenke kwa Kikurya) wanafanana sana na kuku, lakini ni wadogo kuliko kanga na kuku, nao manyoya yanayofanana na wanaruka pamoja.

Na tabia hizi za wachawi kukaa pamoja, wazinzi kuwa marafiki na waturutumbi kuturutumba pamoja, ndizo zinazotufikirisha sana siku hizi kwa sababu zimetufanya kujua chama chetu, Chama Cha Mapinduzi, ni chama cha watu wa namna gani kwani wamekusanyika pamoja kwa sababu tabia zao zinafanana.

Na hivyo hivyo hata kuteuliwa Paul Christian Bashte Makonda, kunatufundisha kwamba yeye Makonda, Jakaya Kikwete, Abdulrahman Kinana, Nnape Nnauye, Albert Chalamila, “Mzee wa hatukubali hata kidogo,” Bwana Mohamed Mchengerwa, Ole Sabaya, Ali Hapi, Katibu Mkuu wao Chongolo na hata Chifu Hangaya mwenyewe, wote wanakaa pamoja, wanafanya siasa pamoja, kwa hiyo ni wapenzi wa tabia za Makonda.

Kwa kanuni ile ile ya ndege wenye manyoya yanayofanana kuruka pamoja, na kanuni ileile ya watu wenye mapenzi yanayofanana na tabia zinazofanana kukusanyika pamoja au kujikuta wameunda kikundi kimoja cha watu wenye tabia zinazofanana, basi na hawa viongozi wa CCM, wana-CCM na wafuasi wa CCM hawawezi hata kidogo kujitenga na mambo ya Makonda.

Kwa sababu ya kanuni hii, wakuu wa Chama Cha Mapinduzi, wanachama na wafuasi wao, hawawezi hata kidogo, nikitumia lugha ya rafiki yangu Mchengerwa, kusema hawakubaliani na tabia na vitendo vya aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na hawawezi hata kidogo, kusema hawapendi tabia na vitendo vya aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya.

Mtu hawezi kuambatana na wezi kama yeye siyo mwizi. Hawezi kuambatana na wazinzi kama yeye siyo mzinzi. Hawezi kuambatana na walevi kama yeye siyo mlevi na hawezi kuambatana na wanasiasa kama yeye siyo mwanasiasa au hapendi siasa hata kama hajawahi kuchagua au kuchaguliwa katika nafasi fulani ya kisiasa.

Kinachotushangaza sisi, ni watu tunawaowaheshimu sana, tunaotambua busara na hekima zao na tunaotambua historia yao iliyotukuka, kukubali kukaa pamoja na watu kama Makonda, wanaambatana nao, maana yake wanapenda mambo yao au wanapendana na kupendezwa na matamshi yao na vitendo vyao.

Zipo kumbukumbu nyingi mitandaoni za tuhuma dhidi ya Makonda za kuunda kundi la watesaji, watekaji, wauaji na wadhulumaji wa mali za raia wema.

Hata kama Makonda hajawahi kushitakiwa kama mwenzake Sabaya alivyoshitakiwa, ukweli unabaki ule ule kwamba anatuhumiwa kwa hili au lile, yote mabaya tupu.

Kwa sasa Makonda ni namba nne kwenye ngazi yauongozi wa CCM. Kwa nafasi yake ya ukatibu wa Itikadi na Uenezi, yeye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama chetu, inayokaa na kutafakari nani agombee Zanzibar, nani agombee Muhambwe, nani agombee Buhigwe, nani agombee Ruangwa na nani agombee Kongwa.

Kwa maana hiyo, wakubwa wengi kama si wote, lazima sasa watalazimika kumlamba miguu kwa kujua kwamba yeye atakuwa Katibu wa mwenyekiti Samia Suluhu Hassan wakati wa kuteua wagombea.

Hivyo ndivyo Makonda alivyokwea ngazi ya kisiasa na kuwa mmoja wa vigogo wa siasa za Tanzania.

Uongozi huu wa NEC, mwenyekiti Rais Samia na Katibu wake Paul Christian Bashite Makonda, ndio utakaojadili, kuamua, kupitisha na kukubali matamshi ya Bibi Sophia Mjema, aliyekuwa msemaji wa CCM kabla ya Makonda, kwamba Rais wa sasa, Samia Suluhu Hassan, aendelee hadi 2030 yatekelezwe.

Maamuzi ya namna hii hayatapingwa na mtu, kwa sababu wote watakaokuwa wamekaa katika kikao kitakachoamua hivyo ni watu wenye tabia zinazofanana, matamanio yanayofanana, vitendo vyao vinafurahiwa na wote kama kanuni inavyosema: Ndege wenye manyoya yanayofanana huruka pamoja au kwa Kibritish kwamba birds of the same feathers flock together. Kidumu Chama Cha Mapinduzi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

error: Content is protected !!