RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amezindua Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, yenye jukumu la kudhibiti uvujaji wa taarifa za faragha za watu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Uzinduzi wa tume hiyo pamoja na mifumo ya usajili wa malalamiko ya ukiukwaji wa misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi, umefanywa na Rais Samia leo tarehe 3 Aprili 2024, jijini Dar es Salaam.
Mkuu huyo wa nchi amesema tume hiyo itasaidia kulinda taarifa za watanzania katika sekta ya kiuchumi, kijamii na kisiasa huku akidai itasaidia kuwadhibiti wanasiana wanaozitumia taarifa za watu vibaya mitandaoni kwa lengo la kujipatia mamlaka.
“Sheria ya ulinzi binafsi na tume ya kulinda taarifa binafsi ni nyenzo muhimu katika kujenga uchumi na mifumo ya kidigitali. Niseme tunapoizindua tume hii itambue kwamba ina kazi nzito sana na ni muhimu kwa maisha yetu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi,”
“Mifumo yake mnayokwenda kusimamia inaweza kutumika kukuza uchumi wa kidigitali na kisiasa kwa wanaotaka mamlaka wakaitumia hiyo mifumo ya kisiasa wakawasema wengine wakapenya,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema tume hiyo itasaidia kudhibiti watu au vikundi vinavyodukua taarifa za watu binafsi, kwa kuwa itakuwa na jukumu la kukusanya na kutunza taarifa hizo.
“Kila mwanadamu ana utashi na anastahili staha, hivyo zipo baadhi ya taarifa asingependa kujulikana kwa kila mtu, kwa kweli ingekuwa taarifa zetu zote ziko wazi na watu wanazijua tusingetazamana usoni au hii dunia ingekuwa ya aina nyingine. Hakuna faragha hakuna staha lakini kwa sababu mwanadamu anahitaji staha ndio maana tumekuja na tume hii,” amesema Rais Samia.
Rais Samia ameagiza taasisi za umma na vinafsi zinasajiliwa katika mfumo wa tume hiyo kabla ya Disemba 2024.
Miongoni mwa majukumu ya tume hiyo, ni kufanyia kazi malalamiko ya haki ya faragha kisha kuwachukulia hatua wahusika watakaobainika kutenda kosa hilo.
Lengo lingine ni kudhibiti taasisi zinazohusika na utunzaji wa taarifa binafsi, kutotoa siri za wateja wao hadharani kinyume cha sheria, kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
Leave a comment