Tuesday , 7 May 2024
Home Habari Mchanganyiko TRA yatoa taarifa ya makusanyo ya kodi katika robo tatu ya mwaka
Habari Mchanganyiko

TRA yatoa taarifa ya makusanyo ya kodi katika robo tatu ya mwaka

Alphayo Kidata, Kamishna Mkuu wa TRA
Spread the love

 

KATIKA kipindi cha robo ya tatu ya Mwaka wa fedha 2023/24, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. 6.63 trilioni, sawa na ufanisi wa asilimia 95.17 ya lengo la kukusanya Sh. 6.97 trilioni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mamlaka hiyo imesema, makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 11.68 ikilinganishwa na makusanyo ya Sh. 5.94 trilioni ya kipindi kama hicho katika Mwaka wa fedha 2022/23.

Katika taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata amesema katika mwezi Machi 2024, TRA imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh trilioni 2.49, sawa na ufanisi wa asilimia 97.05 katika lengo la kukusanya kiasi cha Sh. 2.56 trilioni.

Amesema kuwa makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 6.91 ukilinganisha na kiasi cha Sh. 2.32 trilioni kilichokusanywa mwezi kama huo katika mwaka wa fedha 2022/23.

“Makusanyo ya kodi katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha Mwaka wa Fedha 2022/23 Januari tulikusanya Sh 2,011,169.93 wakati lengo lilikuwa Sh 2.248,412 lakini kwa mwaka huu makusanyo ya Januari ni Sh 2,123,332.51 sawa na 94.44%,” amesema.

Ameongeza kuwa”Februari mwaka huu tulikusanya 2,021,106.00 sawa na 93.70 % wakati lengo lilikuwa ni 2,157,069 hata hivyo, mwaka 2022/23 tulikusanya Sh 1,600,841.93,”

Kamishna huyo amesema mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka ni kuongezeka kwa uhiari wa ulipaji kodi kufuatia maboresho yanayoendelea kufanywa ikiwemo kusogeza huduma jirani na walipakodi.

Ameeleza kuwa kuanzishwa Divisheni za Walipakodi Wadogo na Walipakodi wa Kati, pamoja na kuendelea kusuluhisha pingamizi za kodi nje ya mahakama zimechangia ukusanyaji huo wa kodi.

Pia, amesema mafanikio hayo yamechagizwa na muitikio mzuri wa walipakodi kuwasilisha kwa wakati ritani za kodi kwa mwaka 2024 kupitia mifumo ya Tehama ya Uwasilishaji wa Ritani.

“Kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji na ukuaji wa shughuli za kiuchumi hapa nchini zinazochangia mapato kama vile sekta za madini, taasisi za kifedha ikiwemo mabenki, sekta ya utalii,” amesisitiza.

Vilevile amesema kuongezeka kwa ufanisi kwenye huduma za forodha hususani katika kusimamia kodi zinazohusiana na uingizaji wa mizigo toka nje ya nchi.

Akielezea mikakati yao kufikia lengo la ukusanyaji kodi, Kidata amesema wananchi wanapaswa kuendelea kutoa taarifa juu ya vitendo vinayoashiria ukwepaji wa kodi nchini ikiwemo biashara za magendo na uuzwaji wa bidhaa ambazo hazijabandikwa stempu za kielektroniki (ETS).

“Ikumbukwe kuwa kukithiri kwa vitendo hivi haviathiri makusanyo ya mapato ya serikali pekee, bali vinahatarisha afya na usalama wa wananchi kwa bidhaa hizi kuuzwa sokoni wakati
hazina viwango vya ubora kwa matumizi ya binadamu,” ameeleza.

Aidha, amewataka wafanyabiashara wote wanashauriwa kuendelea kutoa risiti za kielektroniki (EFD) zenye viwango sahihi kila wanapouza bidhaa au kutoa huduma.

“TRA inawashukuru na kuwataka
wananchi wote kuendelea kushiriki katika kampeni ya TUWAJIBIKE kwa kudai risiti stahiki za kielektroniki (EFD) zinazobainisha bidhaa na kiasi sahihi kilicholipiwa,” amefafanua Kidata.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Samia aagiza huduma za dharura maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga Hidaya

Spread the love   RAIS wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Samia...

Habari Mchanganyiko

Mahakama yatoa uamuzi zuio dhidi ya Club House

Spread the loveMAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu jijini Dar es Salaam,...

Habari Mchanganyiko

GGML, OSHA yawanoa bodaboda 200 Arusha

Spread the loveZAIDI ya madereva bodaboda 200 wa jiji la Arusha wamepatiwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Serikali kuwakopesha wajasiriamali 18.5bn/- kupitia NMB

Spread the loveSerikali imetenga kiasi cha Sh 18.5 bilioni kwa ajili ya...

error: Content is protected !!