December 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania yang’ang’aniwa kutoa takwimu za Corona

Spread the love

 

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO), limeitaka serikali ya Tanzania kutoa takwimu za maambukizi ya virusi vya Covid 19, ili kuwezesha kujulikana idadi halisi ya maambukizi na vifo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

WHO imechukua hatua hiyo, kufuatia idadi kubwa ya wasafiri wa Tanzania waliopatikana na kuwa na virusi vya Corona kwenye mataifa ya nje.

Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 21 Februari 2021, imeeleza kuwa utoaji wa taarifa hiyo utasaidia kuonesha mwendo wa maambukizi nchini.

Wakati WHO ikitoa wito huo, leo Rais John Magufuli amewataka rais wa Tanzania kujikinga sambamba na kutumia njia za asili kukabiliana na virusi vya Corona.

Dk. Magufuli ametoa wito huo wakati akizungumza katika Ibada ya Misa Takatifu ya Dominika ya Kwanza ya Kwaresma, kwenye Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Kwa mara ya mwisho Tanzania kutoa takwimu za maambukizi na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo, ilikuwa Aprili mwaka jana.

WHO imekuwa ikisisitiza serikali ya Tanzania mara kwa mara, kutoa takwimu mpya za maambukizi na vifo, kwa kuwa hatua hiyo, “itarahisisha kuzuia maambukizi mapya.”

”Moja ya makubaliano ya nchi wanachama ni kutoa takwimu za mwenendo wa maambukizi, nimewakumbusha serikali ya Tanzania na ninazo kumbukumbu kwa maandishi kuwa wao ni sehemu ya wanachama wa WHO, hivyo wanatakiwa kuitikia wito huu,” imeeleza taarifa ya shirika hilo.

Katibu mkuu wa WHO, Tedros Ghebreyesus anasema, hatua dhabiti za kiafya zinapaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na Corona.

Amesisitiza, “takwimu ni suala la muhimu pia kwa Tanzania kuzitoa , tena baada ya kesi za miongoni mwa wasafiri na wageni katika miezi ya hivi karibuni.”

Tangu kuripotiwa madai ya kuwapo kwa mlipuko mpya wa maambukizi ya virusi vya Corona nchini, kumekuwa na kauli kinzani zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa serikali, zikilenga hasa kuonyesha kuwa Tanzania hakuna maambukizi hayo.

Kwa mfano, serikali kupitia kwa waziri wake wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dorothy Gwajima, amekuwa akieleza kuwa Tanzania haina maambukizi ya Covid19, bali ametaka wananchi kuchukua tahadhari ikiwemo kutumia dawa za asili.

Alisema, wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari kutokana na kuenea kwa ugonjwa huo katika mataifa jirani.

Akiongea kwa kujiamini, waziri Gwajima alisema, “…ninachotaka kusema hapa ni kwamba, nchi yetu ipo salama. Tunasikia kwa jirani huko kuna shida, usisubiri vitoke kwa jirani vije kwasababu tunaingiliana maisha, sisi tunajiandaa kwa maisha.”

Waziri huyo alifika mbali zaidi, baada ya kupiga marufuku matangazo ya wagonjwa wa Corona wala vifo vinavyodaiwa kutokana na ugonjwa huo, kutolewa hadharani na kile alichoita, “mamlaka zisizohusika.”

error: Content is protected !!