WIZARA Ofisi ya Rais-TAMISEMI, imetenga fedha kiasi cha Sh. 17.79 bilioni, kwa ajili ya uratibu na kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 16 Aprili 2024 na Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, akiwasilisha bungeni jijini Dodoma, makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha ujao wa 2024/25.
“Katika mwaka wa 2024/25 TAMISEMI imetenga Sh. 17.79 bilioni kwa ajili ya kuratibu na kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024. Kati ya fedha hizo Sh. 8.00 bilioni ni fedha kutoka serikali kuu kwa ajili ya uratibu Ofisi ya Rais – TAMISEMI (Makao Makuu) na Sh. 9.79 bilioni ni mchango wa halmashauri kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia uchaguzi huo,” amesema Mchengerwa.
Amesema mbali kiasi hicho cha fedha kilichotengwa na TAMISEMI kwa ajili ya uchaguzi huo, katika mwaka wa fedha wa 2023/24, ilitenga Sh. 12.00 bilioni kwa ajili ya maandalizi yake, ambapo hadi Machi 2024, ilipokea Sh. 5.6 bilioni huku zilizosalia zikihusisha shughuli za ununuzi ambazo taratibu zake zinaendelea.
Katika hatua nyingine, Mchengerwa aliliomba Bunge liidhinishe bajeti nzima ya TAMISEMI kwa 2024/25 kiasi cha Sh. 10.12 trilioni, ambapo Sh. 6.70 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwemo mishahara ya watumishi na Sh. 3.41 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Leave a comment