MBUNGE wa Ukonga, Jerry Silaa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), amesema mkataba wa uwekezaji katika bandari nchini baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai umetaja maeneo machache mahususi ya ushirikiano na sio nchi nzima. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Akizungumza katika Kituo cha runinga cha Clouds leo Ijumaa amesema; “Tumesema IGA hii ni mkataba baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya Tanzania na Falme ya Dubai na ibara ya 2 (1) inaeleza kuwa nia hasa ni kutengeneza msingi wa kisheria wa ushirikiano.
“Sasa huo ushirikiano unatajwa ibara ya 4 (1) kwa awamu ya kwanza na ya pili, na kinachotajwa ni ushirikiano sio miradi. Ukienda 5 (1) ndio inaeleza miradi itakayoanza ni ipi, ambayo ni Bandari ya Dar maeneo 7. Lakini mtu anakuja kukuambia yako maeneo 54, mpaka unapata tabu kwa sababu hayapo.
Aidha, amesema hakuna ibara inayoonesha kuwa bandari hiyo imeiuzwa.
“Wanaosema bandari inauzwa, waonyeshe watu mahali panaposema mauziano, kwa sababu hata ibara ya 12 (1) inaongelea mambo ya ulinzi katika mkataba huu wa uwekezaji wa bandari na wala sio kuuziana kama watu wanavyojaribu kusema” amesema na kuongeza kuwa;
“Watanzania wote wana haki ya kuzungumzia mkataba huu, lakini lazima tuuweke kisheria. Bahati mbaya katika wapotoshaji hawa wakati mwingine hawatumii hoja za msingi jambo linalopoteza maana ya majadiliano mitaani.”
Leave a comment