SERIKALI imepata hasara ya kiasi cha Sh. 111.76 milioni, baada ya baadhi ya hospitali za rufaa za mikoa kutoa msamaha wa matibabu kwa watu wasiokuwa na sifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Hayo yamebanishwa katika ripoti ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, kwa mwaka wa fedha wa 2022/23, iliyowasilishwa jana Jumatatu, bungeni jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa ukaguzi huo, imebanika hospitali tatu za rufaa zilitoa misamaha kwa wagonjwa wasiostahili, Mount Meru ilitoa msamaha wa Sh. 25.36 milioni, Sekou Toure (Sh. 7.29 milioni) na Songwe (Sh. 79.09 milioni).
“Ukaguzi ulibaini hospitali tatu za rufaa za mikoa hazikukusanya jumla ya Sh. milioni 111.76, baada ya kutoa misamaha ya gharama za matibabu kwa wagonjwa wasio na sifa ikijumuisha misahama ya matibabu ya wafungwa na watu wengine bila kuwepo kwa nyaraka za kuthibitisha vigezo vilivyotumika,” imesema ripoti hiyo na kuongeza:
“Badala yake, hospitali hizi zilipaswa kuwasilisha hati za madai ya gharama za matibabu ya wafungwa katika idara husika ya Magereza (Fungu 29). Upotevu huu wa mapato unasababishwa na kutofanyika kwa tathmini ya vigezo vya utoaji wa misamaha ya gharama za matibabu.”
Leave a comment