Sunday , 19 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Kamati ya bunge yapigia chapuo kilimo ikolojia
Habari Mchanganyiko

Kamati ya bunge yapigia chapuo kilimo ikolojia

Spread the love

SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo imeshauriwa kushirikiana na wadau wa kilimo ikolojia kutoa elimu kuhusu kilimo hicho ambacho kina tija kwenye soko na ni salama kwa afya za watumiaji. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea).             

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Biashara, Viwanda na Kilimo, Deo Mwanyika wakati akizungumza na waandishi wa habari bungeni Dodoma baada ya kukutana na Kikosi  Kazi cha Mbegu za Wakulima kilichokutana na kamati hiyo.

Mwanyika amesema kikosi kazi hicho kimeonesha kuna changamoto ya utekelezaji wa mkakati wa kilimo ikoloji ambao ulizinduliwa Novemba 9, 2023, hivyo ni wakati muafaka wa kuweka nguvu kwenye eneo hilo, hasa kwa kutoa elimu kwa wakulima na jamii juu ya faida ya kilimo hicho.

Amesema ni vema utekelezaji wa mkakati ukanza ili kilimo kinachotumia mbegu za wakulima kupewa kipaumbele.

“Mikoa mingi ya Nyanda za Juu Kusuni inazalisha mazao kwa wingi, ila inaonekana kukabiliana na changamoto ya lishe duni na udumavu, hivyo ni wakati muafaka wa kuelekeza nguvu kwenye kilimo hai, hasa kwenye kutoa elimu ambayo itazingatia mkakati wa kilimo ikolojia,” amesema.

Mwenyekiti huyo amesema historia inaonesha babu na bibi zetu waliweka mkazo kwenye matumizi ya mbolea za asili, hivyo kuna haja ya kurejea katika kilimo hicho pamoja na ukweli kwamba hawawezi kuacha kilimo cha kisasa moja kwa moja kutoka na mahitaji ya chakula duniani.

Amesema iwapo kutakuwa na mkazo wa kuwekeza nguvu kwenye mbegu za wakulima ni wazi kuwa jamii ya Kitanzania itakuwa salama kiafya kwa asilimia kubwa pamoja na uhakika wa soko.

“Kazi ya Bunge na kamati zake ni kushauri, kushawishi na kuweka msukumo kwenye mambo ambayo yanahusu jamii na sisi kama kamati tutafanya hivyo ili serikali iweze kuchukua hatua kwenye kilimo ikolojia ambacho kina tija kwa nchi na wananchi, ” amesema.

Mjumbe wa Kamati, Dk Christine Ishengoma amesema watatumia nafasi zao kuhakikisha serikali kupitia wizara ya kilimo wanaweka kipaumbele kwenye matumizi ya mbegu za wakulima.

“Sisi tumezaliwa na kukuzwa kwa vyakula vya asili, hivyo tunakiri kuwa mbegu za asili ni nzuri kiafya, ila pia mnatakiwa kufanya utafiti ambao utaonesha mbegu za asili ni nzuri kuliko za kisasa, sisi tutaendelea kutoa elimu na kuishawishi serikali,” amesema.

Mbunge wa Viti Maalum, Kuntu Majala amesema katika kuunga mkono juhudi za Kikosi Kazi cha Mbegu za Wakulima yupo tayari kushirikiana nao kusambaza mbegu za wakulima katika shule 197 zilizopo wilayani Chemba mkoani Dodoma  kwa kuwa mbegu hizo zina faida kwa afya ya binadamu.

Naye Mbunge anayewakilisha Vijana, Ng’wasi Kamani amesema kamati yao itahakikisha inashauri serikali ifanyie marekebisho ya sheria ya mbegu ili iweze kulinda wakulima wa mbegu asili, huku akishauri Kikosi Kazi cha Mbegu za Wakulima kuongeza juhudi katika kutoa elimu zaidi.

Mratibu wa Mtandao wa Baionuai Tanzania (TABIO), Abdallah Mkindi amesema wamefurahishwa na ushirikiano ambao wamepewa na kamati hiyo na kwamba wanapata nguvu ya kupigania mbegu za wakulima kwa moyo mmoja.

Mkindi amesema wadau wa kikosi kazi cha mbegu za wakulima wanatamani kuwepo kwa sheria ambayo itaweza kusaidia mbegu za mkulima ili zipewe nguvu ya kisheria na kuendelezwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Islands  of Peace (IDP) Tanzania, Ayesiga Buberwa amesema ombi lao la kukutana na kamati hiyo ni kuhakikisha mbegu za mkulima zinalindwa na kuendelezaa hali ambayo itaiondoa nchi kwenye utegemezi wa mbegu na chakula.

“Sisi juhudi zetu ni kuona kuna mizani inayofanana hasa kwenye kulinda na kutunza mbegu zetu za asili ambazo zina lishe bora, tunaamini kamati itashauri serikali kufanikisha mipango yote ambayo inaenda kuleta tija kwenye mbegu za wakulima,” amesema.

Joanita Kahangwa, Mwanachama wa Shirikisho la Wakulima Tanzania (CHIWAKUTA), kutoka mkoani Kagera, ameishauri Serikali iweke nguvu kwenye mbegu asili kwa kuwa zinaweza kukabiliana na wadudu, mabadiliko ya tabianchi na niendelevu.

“Tunaomba Serikali ilinde mbegu za asili kwa kuwa hazina madhara kama mbegu za kisasa, naamini kinachohitajika ni mafunzo zaidi ya kuzilinda na kuzitunza,”amesema.

Naye Elibaraka Joseph Mwanachama wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Mkoa wa Arusha (MVIWAARUSHA) amesema wabunge wanawajibu wa kulinda wakulima na Watanzania kwa nguvu zote, ili kuwa na taifa la watu wasio na changamoto za kiafya.

Baadhi ya zinazosishiki katika kikosi kazi cha mbegu za wakulima TABIO, IDP, PELUM, TOAM), SAT, ECHO EA, ESAFF, AFRONET, ENVIROCARE, MVIWAARUSHA, MVIWAMA, MVIWAKI, (MVIWAMORO), TUSHIRIKI, ActionAid Tanzania na SwissAid Tanzania, ACB, ANSAF, VOCHAWOTA, SHIWAKUTA, FLORESTA na wengine.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

CCM yamteua Pele kuwa mgombea ubunge Kwahani

Spread the loveKamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Canada yatenga bilioni 38 kutekeleza mradi ya kuinua vijana TZ

Spread the loveSERIKALI ya Canada kupitia ‘CARE International Canada’ imetenga takribani Sh...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Ujenzi kituo cha kupoza umeme Chalinze wafikia asilimia 93.7

Spread the loveKamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza...

Habari Mchanganyiko

Balile ateuliwa rais wa wahariri Afrika Mashariki

Spread the loveJumuiya ya Wahariri wa Afrika Mashariki (EAES), imemchagua Mwenyekiti wa...

error: Content is protected !!