Friday , 3 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Serikali yafafanua hatima ya viongozi NEC
Habari za SiasaTangulizi

Serikali yafafanua hatima ya viongozi NEC

Spread the love

WAKATI mjadala ukiibuka  juu ya hatma ya viongozi wa sasa katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), baada ya sheria yake kufanyiwa marekebisho na kuitwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Serikali imesema wataendelea kubaki hadi muda wao wa kukaa madarakani utakapoisha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Hayo yamebainishwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, akizungumza na MwanaHALISI kwa njia ya simu, kuhusu mabadiliko ya muundo wa tume hiyo baada ya kubadilishwa jina kufuatia utungwaji wa Sheria mpya ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya 2024.

Alipoulizwa iwapo mchakato wa mabadiliko ya watendaji wa tume umeshaanza, Matinyi alijibu “soma kifungu cha 27 cha sheria yenyewe, kisha ona kama bado kuna swali.”

Kwa mujibu wa kifungu cha 27 cha sheria hiyo iliyosainiwa hivi karibuni na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, baada ya muswada wake kupitishwa na Bunge Novemba 2023, kinasema mara baada ya sheria kuanza kutumika, viongozi wa tume wataendelea kushika madaraka hadi pale muda wao utakapokoma.

“Mara baada ya kuanza kutumika kwa sheria hii, mtu yeyote ambaye ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti au Mjumbe wa Tume ataendelea kushika madaraka hayo hadi pale ujumbe wake utakapokoma,” kinasema kifungu cha 27 cha sheria hiyo.

Kwa mujibu wa sheria ya zamani na sheria ya sasa, muda wa viongozi waandamizi wa tume kukaa madarakani akiwemo mwenyekiti wake ni miaka mitano, ambapo Jaji Jacob Mwambehele aliyeko madarakani sasa hivi, aliteuliwa na Rais Samia Disemba 2021, hivyo ataendelea kuwepo hadi muda wake utakapoisha.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa INEC watateuliwa na Rais kutoka katika majina yatakayopendekezwa na kamati ya usaili. Kisha wataapishwa na Rais.

Kifungu cha 25 cha sheria hiyo, kinasema tume kwa kushauriana na waziri mwenye dhamana na masuala ya utumishi, itaandaa muundo wa utumishi wa sekretarieti ya tume, huku cha 26 kikisema tume inaweza kutengeneza kanuni na miongozo na kutoa maelekezo kwa ajili ya utekelezaji bora wa majukumu yake.

Kifungu cha sita cha sheria hiyo kinasema tume itakuwa chombo huru na kinachojitegemea na uamuzi wake hautaingiliwa na chombo chochote au kulazimika kufuata maagizo ya mtu au idara yoyote ya Serikali au maoni ya chama chochote cha siasa.

Miongoni mwa watu waliohoji muundo wa tume baada ya kubadilishwa jina ni viongozi wa vyama vya siasa na asasi za kiraia. Ni baada ya Serikali kusema kuanzia tarehe 12 Aprili 2024, itaitwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Aliyekuwa Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema  viongozi wa tume ya sasa  (NEC) wajiuzulu ili kupisha mchakato wa kuwapata wajumbe wapya wa INEC “tume

ya sasa ikibakia ofisini baada ya tarehe 12 prili  itakuwapo kisheria lakini haitakuwa na uhalali wa kisiasa. mchakato wa uchaguzi ni mchakato wa kisiasa tena wenye misingi ya trust.”

“Endapo masharti ya Kifungu cha 5 cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 2024 hakitafuatwa basi, hatutakuwa na tume iliyo ofisini, kwa sababu tume ni makamishina na mwenyekiti wao. kujibanza kwenye kifungu cha 27 cha sheria mpya hakuna mantiki yeyote. Najua wengi, kwa bahati mbaya hata wana mageuzi wa muda mrefu, wamelalia kwenye hoja hii dhaifu kuhalalisha tume ya sasa kuendelea. Watu wanaowaza hivi wangekuwa afrika kusini wangemwacha mandela afie jela kwa sababu apartheid ilikuwa halali kisheria, lakini apartheid haikuwa haki wala halali kisiasa,” ameandika Zitto.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alitoa maoni yake kuhusu mabadiliko hayo kupitia akaunti yake ya mtandao wa X akisema “anayejua uhuru wa tume kwenye uchaguzi ulipatikana lini hadi sasa iitwe tume huru anisaidie.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!