BAADA ya kupachika mabao mawili kwenye mchezo wa jana Jumapili tarehe 30 Agosti 2020 dhidi ya Aigle Noir ya Burundi kwenye kilele cha ‘Wiki ya Mwananchi’ mshambuliaji Michael Sarpong na winga Tuisila Kisinda wa Yanga, wameanza vizuri kwenye mchezo wao wa kwanza toka walipojiunga na timu hiyo kwenye dirisha kubwa la usajili. Anaripoti Kelvin Mwaipungu… (endelea)
Mchezo huo ambao ulikuwa wa kirafiki na kama sehemu ya tamasha hilo, viwango vya nyota hao wawili vilionekana kuwavutia mashabiki wengi wa klabu hiyo ambao walionekana kutegemea makubwa kutoka kwao katika kurudisha heshima yao ya ubingwa kwa msimu huu ambao wameukosa kwa miaka mitatu mfululizo.
Bao la kwanza la Yanga katika mchezo huo, lilifungwa na Tuisila Kisinda dakika ya 38 na baadae katika kipindi cha pili, Michael Sarpong alipachika bao la pili 51 kwa kichwa baada ya kupokea pasi kutoka kwa Ditram Nchimbi.
Katika mchezo huo, Kisinda alionekana kuvutia mashabiki wengi wa Yanga kutokana na kasi yake uwanjani na uwezo mkubwa wa kufunga pale anapopata nafasi.
Kwa upande wa Sarpong alionekana kuwa msumbufu kwa walinzi wa timu pinzani kutokana na umbile lake la mwili na uwezo mkubwa wa kukaa na mpira miguuni pamoja na kufunga.
Wote wawili wamejiunga na Yanga katika dirisha hili kubwa la usajili linaloenda kufungwa muda mchache kutoka sasa.
Kisinda alijiunga na Yanga akitokea klabu ya AS Vita ya Congo, huku Sarpong amesajiliwa na klabu hiyo akitokea Rayon Sport ya nchini Rwanda
PICHA YAKE