December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

SANKARA: Rais aliyetendwa vibaya na swahiba, alipinduliwa na kuuawa

Thomas Sankara

Spread the love

 

NI takribani miaka 34 imepita tangu kuuawa kwa aliyekuwa Rais wa Burkina Faso, Thomas Sankara. Lakini kesi juu ya mauaji yake imeanza kutonesha kidonda kwa wafuasi wake hasa ikizingatiwa moja ya watuhumiwa ni aliyekuwa rafiki yake wa karibu Blaise Compaore.

Compaore ambaye alikuwa Rais wa taifa hilo kuanzia tarehe 15 Oktoba, 1987 hadi tarehe 31 Oktoba, 2014 ni miongoni mwa washtakiwa 14 wa mauaji hayo.

Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa tarehe 11 Oktoba, 2021 lakini ikaahirishwa mpaka tarehe 25, Oktoba ya mwaka huu baada ya upande wa utetezi kuomba muda wa kujiandaa zaidi.

Mjane wa Rais Sankara pia alikuwepo siku ambayo kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa na kunukuliwa akisema “Ni siku ya ukweli kwangu, kwa familia yangu na raia wote wa Burkina Faso”.

Tuhuma za Rais Compaore

Rais Compaore ndiye mshukiwa muhimu wa mauaji hayo na ndiye alirithi nafasi ya urais baada ya mapinduzi yaliyosababisha kifo cha swahiba wake Rais Sankara.

Kwa mujibu wa nyaraka za jeshi zilizogunduliwa na Shirika la Habari la Ufaransa AFP, Compaore anatuhumiwa kwa makosa ya kushiriki mauaji, kuhujumu usalama wa taifa na kuficha maiti ya Sankara.

Compaore ambaye anaishi uhamishoni nchini Ivory Coast tangu alipoondolewa madarakani mwaka 2014, ndiye mtuhumiwa namba moja licha ya kwamba hayupo mahakamani.

Ivory Coast imekua ikikataa kumrejesha Compaore nchini mwake licha ya Burkina Faso kutoa waranti ya kukamatwa kwake miaka sita iliyopita.

Blaise Compaore

Tarehe 8 Novemba mwaka huu, mshtakiwa Jean-Pierre Palm ambaye ni mkurugenzi wa zamani wa usalama wa kitaifa, naye ni mmoja wa watuhumiwa kwani aliteuliwa kuwa mkuu wa vikosi vya ulinzi mwezi mmoja baada ya mapinduzi.

Jean-Pierre Palm anatuhumiwa kushiriki katika kuhatarisha usalama wa nchi. Muda mfupi kabla ya mapinduzi, alikuwa mkuu wa idara ya upelelezi.

Akizungumzia tukio hilo la mapinduzi, Jean-Pierre Palm amesema hakujua chochote kwani alikuwa kwa daktari wa meno wakati serikali iliposhambuliwa.

Amesema katika msukosuko huo, alikimbilia kwa mtu anayemjua, ilikuwa usiku na siku iliyofuata alienda makao makuu ya serikali na kupata habari juu ya kifo cha Thomas Sankara.

“Wewe ni mwanajeshi, ulisimamia ulinzi, unasikia milio ya risasi na unakimbilia kwa rafiki yako kwa sababu huelewi kinachoendelea? “, Ferdinand Nzepa, wakili wa familia ya Sankara alimhoji.

“Ulitaka nifanye nini?” Nilikuwa peke yangu, nimevaa kiraia na bila silaha, ” alijibu Jean-Pierre Palm.

Jean-Pierre Palm anashukiwa kuharibu, siku moja baada ya Oktoba 15, 1987, mitambo ya kurekodi sauti ya vikosi vya ulinzi akishirikiana na maofisa wa Ufaransa. Inadaiwa kwamba wakati huo, washirika wa Thomas Sankara walikuwa wakirekodi sauti za viongozi kadhaa ikiwa ni pamoja na Blaise Compaoré, na rekodi hizi zingeweza kumtia hatiani rais huyo wa zamani.

Uswahiba wa Sankara na Compaore?

Historia inamtambua Thomas Sankara kama ‘Che guevara ama Fidel Castro’ wa Afrika. Hii ni kutokana na maono yake katika uongozi na fikra zake kudumu mpaka sasa hasa miongoni mwa wafuasi wake.

Lakini pia alikuwa ni kiongozi mashuhuri wa siasa Barani Afrika katika karne ya 20 akifananishwa na Nelson Mandela (Afrika Kusini) na Patrice Lumumba (Congo DRC).

Agosti mwaka 1983, vijana wawili, makapteni wa jeshi na wanamapinduzi, Kapteni Thomas Sankara na Kapteni Blaise Compaore, waliipindua Serikali ya Rais wa wakati huo katika nchi iliyokuwa ikijulikana kama Upper volta. Rais huyu aliitwa Baptiste Ouedraogo.

Vijana hawa wakiwa katika fikra za Karl Max, wakiwa na ndoto nyingi za kuijenga Upper volta, walibadili kabisa historia ya taifa hilo, walibadili jina la nchi na kuitwa Burkina faso, maana yake nchi ya watu waaminifu.

Compaore na Sankara

Mara nyingi Sankara alikuwa anatumia baiskeli kutembelea vijiji kuhimiza maendeleo, wakati pacha wake yaani Compaore wakiwa kama pete na kidole.

Urafiki wa makapteni hawa wa jeshi, ulikuwa mkubwa kiasi kwamba wakati wanausalama walipomwambia Sankara kuwa Compaore ana mpango wa kumpindua na kumuua, aliwajibu kuwa Compaore asingeweza kufanya hivyo, labda mtu mwingine.

Compaore alikutana na Sankara mwaka 1976 katika mafunzo ya kijeshi nchini Morocco na hapo walianza urafiki wao uliokuwa wazi kwa karibu watu wote waliokuwa wakiwafahamu nchini Burkina Fasso na nchi jirani.

Sankara alikuwa akiwaeleza wanausalama wake kuwa, hata kama Compaore angetaka kufanya hayo, hakuna wa kumzuia.

Ni wazi kuwa Kapteni Sankara alikuwa karibu sana na Compaore, kwa kiasi ambacho Compaore alikuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya Sankara.

Kama ilivyotabiriwa na watu wengi wa karibu wa  Sankara, Compaore aliongoza mapinduzi yaliyosababisha kifo cha Sankara mwaka 1987, na yeye mwenyewe (Compaore), huku akishuhudia rafiki yake kipenzi Sankara akiuawa, akawa ndiye mrithi wa kiti cha Urais wa iliyokuwa Upper Volta baadaye Burkina Fasso.

Thomas Sankara ni nani?

Sankara alizaliwa tarehe 12 Desemba, 1949 mjini Yoko katika nchi iliyokuwa ikiitwa Upper Volta (Volta ya juu) na kuuawa tarehe 15 Oktoba, 1987 na wanajeshi wenzake wakiongozwa na anayedaiwa kuwa rafiki yake Compaore katika mapigano ya usaliti yaliyotokea Mjini Ouagadougou akiwa katika kikao cha utendaji wa kazi.

Kuna nyakati ambazo Compaore aliwahi kunena kwa kinywa chake katika shirika la kutetea haki za Binadamu duniani kwamba ‘kifo cha Thomas Sankara kilikuwa ni ajali tu’.

Mwaka 1981, Sankara alikuwa waziri wa mambo ya ndani katika serikali ya kijeshi ya Rais wa wakati huo wa Burkinabe ya zamani (Upper Volta), Dk. Jean Baptiste Major.

Baadaye aliteuliwa kuwa waziri mkuu kwa kipindi cha kuanzia Januari 1983 mpaka Mei alipokamatwa na kutiwa mbaroni na serikali ya Rais Major Jean Baptiste kutokana na msimamo wake juu ya ukombozi kwa watu wote wa Volta ya Juu na kupendelea mapinduzi ya kijamaa.

Kwanini alipendwa na wananchi wake?

Sankara alikuwa Rais wa Upper Volta (Volta ya Juu) kuanzia tarehe 4 Agosti, 1983 hadi mwezi tarehe 15 Oktoba, 1987 baada ya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Jean Baptiste yaliyoongozwa na rafiki yake mkuu Kapteni Compaore na kuwa Rais wa tano wa nchi hiyo.

Sankara alianzisha Program mbalimbali za kijamii na kiuchumi kuleta mabadiliko katika nchi za Afrika.

Alibadilisha Upper Volta na kuwa Burkina Faso (land of Upright Men). Alianzisha kampeni ya kuboresha elimu na kutanua huduma za afya kwa watu wa Burkina Faso maeneo ya vijijini hasa kwa watoto walioathirika na magonjwa ya uti wa mgongo, homa ya manjano na surua. Watoto karibu milioni tatu walipata matibabu.

Pia alianzisha kampeni ya upandaji wa miti kitaifa na takribani miti milioni 10 ilipandwa nchi nzima. Alianzisha kampeni ya usafi nchini kote, kila mwananchi alipaswa kufanya usafi eneo alipo na Sankara mwenyewe alikuwa anashika fagio na kuingia barabarani kufanya usafi.

Aliongeza idadi ya wanawake katika serikali yake, ikiwa ni kampeni yake nchi nzima kupinga ukeketaji kwa wanawake, pia alianzisha utaratibu wa kisheria wa kuwataka wasichana waliopata mimba wakiwa mashuleni kuendelea na masomo.

Aliajiri wanawake jeshini, akawapa ajira katika sekta za umma ili kupunguza unyanyasaji wa kijinsia na kuleta uwiano na usawa nchini Burkina Fasso.

Pia ndoa za utotoni na za kulazimishwa hasa za kimila katika maeneo yote ya Burkina Fasso zikapigwa marufuku.

Sankara ambaye hakutaka makuu kabisa kwa wananchi wa Burkina Fasso. Akiwa kama Rais wa nchi, alivaa nguo zilizotengenezwa Burkina Faso badala ya suti kutoka Paris na London. Mara nyingi alionekana akiwa kwenye gwanda la jeshi.

Alifuta matumizi ya magari ya kifahari kwa viongozi na watumishi wote wa umma, yeye kama Rais bila kutumia walinzi, alitumia baiskeli au miguu kwenda kwa wananchi vijijini kuhimiza na kusimamia shughuli za kimaendeleo.

Kwa muda mfupi akiwa kama Rais wa Burkina Fasso, aliifanya nchi kujitosheleza kwa chakula na kuanza kuunza nje.

Sankara aliwahimiza watawala wa Afrika waache kuwaibia wananchi, waache kutegemea misaada kutoka nje.

Alitaka Afrika iache kulipa madeni yasiyolipika. Mwalimu Nyerere naye wakati huo alisema mtu hawezi kulipa madeni wakati watoto wanakufa njaa.

Sankara alisema ukitaka kujua maana ya ubeberu angalia sahani yako ya chakula, utaona kila aina ya chakula unachokula kinatoka nje. Ndipo akahimiza Afrika ijitegemee kwa chakula, akisema: “Anayekulisha anakutawala”

Katika kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinahudumia wanachi wa kawaida, Sankara alipambana na rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma, huku akimtaka kila mwananchi kujituma kulijenga taifa.

Alikuwa mtu anayechukia rushwa na ufisadi, uvivu, uzembe, dhuluma na unyonyaji wa wananchi na rasilimali zao. Alitaka kuona watu wake wakifaidika kwa rasilimali za nchi yake.

Huyu ndiye Thomas Sankara ambaye alipunguza mshahara wake hadi dola 450 sawa na Sh milioni moja kwa mwezi.

Makala hii imeandaliwa na Victoria Mwakisimba, TUDARCo.

error: Content is protected !!