MAHABUSU zaidi ya 2,240 waliokuwa wanashikiliwa katika vyombo vya kisheria kwa kesi za kubambikizwa, wameachwa huru tangu Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, aingie madarakani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 20 Julai 2023, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, katika kikao cha wajumbe wa Tume ya Haki Jinai na wahariri wa vyombo vya habari, kuhusu ripoti yake iliyowasilisha kwa Rais Samia, hivi karibuni.
Zuhura amesema kuachwa huru kwa mahabusu hao, ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Rais Samia, kuimarisha mifumo ya haki jinai nchini.
“Kwa mfano zaidi ya mahabusu 2,240 waliokuwa wanashikiliwa kwenye vyombo mbalimbali vya kisheria wakiweko viongozi wa dini, wanasiasa na wananchi wa kawaida waliachiwa na kurejea uraiani kuendelea na maisha yao. Hii ni baada ya Rais Samia kuagiza vyombo vya utoaji haki kushughulikia masuala hayo,” amesema Zuhura.
Miongoni mwa watu mashughuli walioachwa huru kutoka mahabusu za magereza mbalimbali wakikabiliwa na mashtaka mahakamani, ni pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na walinzi wake wanne, waliokuwa wanakabiliwa na mashataka ya uhujumu uchumi.
Wengine ni baadhi ya viongozi wa dini ya kiislamu waliokuwa wanakabiliwa na mashataka ya ugaidi katika mahakama mbalimbali nchini.
Mbali na kuwaacha huru mahabusu hao, Zuhura amesema Serikali ya Rais Samia imeendelea kuimarisha mfumo wa haki jinai kwa kutekeleza masuala mbalimbali, ikiwemo kuhakikisha wananchi wanapata tafsiri za mienendo ya kesi zao kwa kutumia Kiswahili.
Pamoja na kuanzisha kampeni ya kitaifa ya utoaji huduma ya msaada wa kisheria, inayofahamika kwa jina la “Samia Legal Aid Campaign”.
Katika hatua nyingine, Zuhura amesema baada ya tume hiyo kuwasilisha ripoti yake, ameagiza taasisi zinazosimamia mfumo wa haki jinai kuyafanyia kazi.
Leave a comment