Sunday , 28 April 2024
Home Kitengo Habari Kimataifa Ruto asema mchungaji Mackenzie ni gaidi, waliokufa wafikia 58, mwenyewe agoma kula
Kimataifa

Ruto asema mchungaji Mackenzie ni gaidi, waliokufa wafikia 58, mwenyewe agoma kula

Spread the love

RAIS wa Kenya, Dk. William Ruto amemtaja mchungaji Paul Mackenzie kama mhalifu na gaidi kufuatia kufukuliwa kwa maiti 58 kutoka kwenye  ardhi yake huko Kilifi nchini humo. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa …(endelea).

Mchungaji huyo amejikuta katika kona mbaya kisheria baada ya wapelelezi kufichua kuwa makumi ya watu wamefariki kwa njaa kwa ahadi kwamba watakutana na Yesu.

Akihutubia Wakenya mjini Kiambu mapema leo Jumatatu tarehe 24 Aprili 2023, Ruto ambaye ameonekana mwenye hasira aliwasuta wachungaji ambao wamekuwa wakitumia imani potofu za kidini kuwapotosha Wakenya.

 

Amemfananisha Mackenzie na gaidi na kusema anapaswa kufunguliwa mashitaka.

“Kinachoshuhudiwa huko Shakahola ni sawa na ugaidi. Mackenzie ambaye anafanya kazi ya uchungaji kwa kweli ni mhalifu wa kutisha. Magaidi wanatumia dini kuendeleza vitendo vyao viovu. Watu kama Paul Mackenzie wanatumia dini kufanya vitu kama hivi.

“Watu kama hawa ni sawa na magaidi wengine wowote si wa dini yoyote. Wanatakiwa kuwa gerezani,” Ruto amesema.

WALIOFARIKI WAFIKIA 58

Rais Ruto pia amegusia suala hilo wakati shughuli ya ufukuaji wa miili ikiingia siku ya nne leo.

Wapelelezi wa Kaunti ya Kilifi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai bado wamekita kambi katika msitu wa Shakahola huko Malindi kutafuta miili ya wafuasi wa mchungaji Paul Mackenzie waliozikwa kwenye makaburi ya halaiki.

Hadi leo Jumatatu miili 58 imegundulika kutoka kwenye makaburi ya halaiki katika msitu wa Shakahola, mashariki mwa Kenya, inayodhaniwa kuwa wafuasi wa madhehebu ya Kikristo wanaoamini kwamba wangeenda mbinguni ikiwa wamefunga.

Idadi ya waliofariki, ambayo imekuwa ikiongezeka kwa kasi katika muda wa siku mbili zilizopita huku uchimbaji ukifanywa, inaweza kuongezeka zaidi kwani Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limesema watu 112 wameripotiwa kupotea kwenye dawati la ufuatiliaji wanaloendesha.

Ibada hiyo iliitwa Good News International Church na kiongozi wake, Paul Mackenzie, alikamatwa kufuatia taarifa iliyodokeza kuwapo kwa makaburi yenye kina kirefu yenye miili ya wafuasi wake 31.

Miili ya watoto ilikuwa miongoni mwa waliofariki. Polisi walisema wanaendelea uchimbaji wa makaburi mengine ili kutafuta miili zaidi unaendelea.

Moja ya makaburi hayo inaaminika kuwa na miili ya watu watano wa familia moja – watoto watatu na wazazi wao.

Kiongozi wa kanisa hilo, Paul Makenzie Nthenge yuko rumande, akisubiri kufikishwa mahakamani.

Nthenge amekana kutenda makosa, lakini amenyimwa dhamana. Anasisitiza kwamba alifunga kanisa lake mnamo 2019.

Inadaiwa aliwaambia wafuasi wajinyime kwa njaa ili “kukutana na Yesu”.

Waziri wa mambo ya ndani wa Kenya, Kithure Kindiki, alisema ekari zote 800 za msitu huo zimefungiwa na kutangazwa kuwa eneo la uhalifu.

Nthenge alidaiwa kuvipa majina vijiji vitatu vya Nazareti, Bethlehemu na Yudea na kuwabatiza wafuasi kwenye madimbwi kabla ya kuwaambia wafunge.

AKATAA KULA

Wakati hayo yakiendelea, Mchungaji huyo Paul Mackenzie amekataa kula chakula gerezani.

Ripoti ya polisi inasema Mackenzie amekuwa akikataa kula wala kunywa chochote tangu alipokamatwa kuhusiana na vifo vya washirika wake.

Makachero walisema kuna wakati walitaka kumpa kikombe cha maji lakini alikataa akisema ni wakati wa kufunga na kuomba.

Kisa chake kimewaacha Wakenya vinywa wazi kuhusu alivyofanikiwa kuwashawishi washirika kushiriki zoezi hilo hatari.

Kwa mujibu wa baadhi ya jamaa wa familia za walioathirika, kanisa hilo huwataka watoto kuanza kufunga hadi kufariki, kisha wanafuatwa na kina mama na mwisho wanaume.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Tanzania, Somalia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Somalia...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Kimataifa

Majaji kuamua hatima ya Zuma leo

Spread the loveMajaji nchini Afrika Kusini leo Jumanne wataamua ikiwa rais wa...

Habari za SiasaKimataifa

Spika Afrika Kusini ajiuzulu kwa tuhuma za rushwa

Spread the loveSpika wa Bunge la Afrika Kusini, Nosiviwe Mapisa-Nqakula ametangaza kujiuzulu...

error: Content is protected !!