WAFANYABIASHARA wanaotarajia kukopa ili kuendesha biashara wameshauriwa kuchukua mikopo kwenye taasisi za kifedha ambazo zimesajiliwa na Benki Kuu (BoT). Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma (endelea).
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mabanda ya maonesho ya kilimo, mifugo na uvuvi yanayofanyika kikanda katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.
Amesema taasisi zote zinazotoa mikopo zinatakiwa kuwa zimesajiliwa na Benki kuu ya Tanzania na lazima leseni za taasisi hizo ziwe sehemu ya wazi kwa nia ya mteja kujiridhisha na usajili wa taasisi husika.
Mkuu huyo wa mkoa amesema taasisi ambazo zinatoa fedha bila kuwa na usajili wa BoT zinavunja sheria ya nchi na kwa kufanya hivyo ni sawa na kuwatapeli wale ambao wamekuwa wakikopa pesa hizo kwani hawastahili kutoa mikopo hiyo.
Kwa upande wake Mwalimu wa shule ya Msingi Nzuguni, ambaye hakutaja jina lake litajwe amesema kuwa walimu wamekuwa wahanga zaidi katika mikopo umiza na wakati mwingine hulazimika kuwapatia wale wanaowakopesha kadi za benki na kila mshahara unapoingia hulazimika kukatwa pesa hizo.
Aidha, amesema kutokana na kupata elimu ya kutosha juu ya ukopaji sasa watakuwa makini katika kutambua taasisi sahihi ambazo zipo kisheria katika kukopesha badala ya kujitumbukiza katika mikopo umiza.
Leave a comment