RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amefuta tozo ya asilimia sita, inayotozwa kila mwaka na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kwa wanufaika wa mikopo hiyo, kwa ajili ya kutunza thamani ya fedha. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Rais Samia amefuta tozo hiyo, leo Jumamosi tarehe 1 Mei 2021, akihutubia katika maadhimisho ya sherehe za wafanyakazi duniani ‘Mei Mosi’, zilizofanyika Uwanja wa CCM, jijini Mwanza.
Mbali na kufutwa kwa tozo hiyo, amesema makato ya asilimia 15 yanayokatwa kila mwezi kwenye mshahara wa mnufaika wa mikopo hiyo kila mwezi, itabaki kama ilivyo.
“Changamoto nyingine ni makato ya HELSB, kwenye changamoto hii tumeamua kubakia na asilimia 15 inayokatwa na Serikali imeamua kufuta asilimia sita tuliyokuwa tukikata zaidi,” amesema Rais Samia.
Kiongozi huyo wa Tanzania amefuta tozo hiyo, baada ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), kuiomba Serikali ipunguze mzigo wa makato kwa wanufaika wa mikopo hiyo.
Aidha, Rais Samia amewaagiza wanufaika wa mikopo ya HELSB, waendelee kulipa mikopo hiyo.
“Tusisitize kwamba, deni hili wale waliokopa waendelee kulipa na nichukue fursa hii kuwaagiza HELSB kuondoa asilimia 6,” ameagiza Rais Samia.
Leave a comment