Friday , 3 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rai ya Majaliwa kwa Watanzania
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rai ya Majaliwa kwa Watanzania

Spread the love

TAREHE 2 Aprili 2024, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizindua mbio za Mwenge wa Uhuru mjini Moshi mkoani Kilimanjaro. Kutokana na umuhimu wa historia ya Mwenge wa Uhuru pamoja na malengo ya mbio hizo, ifuatayo ni sehemu ya hotuba ya Waziri Mkuu aliyoitoa katika uzinduzi huo.

NDUGU wananchi, historia ya mwenge wa uhuru inaanza kabla ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 ambapo mwaka 1958 Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati akizungumza na wajumbe wa Baraza la Kikoloni la kutunga sheria aliwaeleza azma yake ya kuwasha mwenge mara Tanganyika itakapokuwa huru.

Ndugu Wananchi, Tanganyika ilipopata uhuru, Mwalimu Nyerere alitimiza azma hiyo kwa kuwasha mwenge na kukabidhi kikosi cha vijana kikiongozwa na Luteni Alexander Ngweba Nyirenda ili waupandishe juu ya Mlima Kilimanjaro.

Wakati akihutubia Taifa, aliwatangazia Watanganyika, Afrika na Dunia nzima, kwa kusema, yafuatayo… ninanukuu: “Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, ulete upendo mahali penye chuki na heshima mahali palipojaa dharau,” mwisho wa kunukuu.

Falsafa hiyo kuhusu mwenge wa uhuru imeendelea kufikishwa kwa wananchi wa Tanzania kupitia mbio za mwenge wa uhuru tangu zilipoanza rasmi mwaka 1964. Wakati wote mbio hizi zimekuwa kichocheo kikubwa katika kuhamasisha amani, uzalendo, umoja na mshikamano ndani na nje ya Taifa letu. Mbio hizi zinafanyika pia kwa lengo la kuchochea shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii sambamba na mapambano dhidi ya adui ujinga, maradhi na umasikini.

Ndugu Wananchi, falsafa hii ya mwenge wa uhuru imekuwa chimbuko la masuala mengi muhimu ya Taifa. Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 yaliyoondoa utawala wa Kisultani ni matokeo ya falsafa hii. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964, nao ni matokeo ya falsafa hii. Kadhalika, mbio za mwenge wa uhuru zimeendelea kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa Kitaifa.

Maeneo yote ambapo mwenge umekuwa ukipita wananchi wamekuwa wakibaki na furaha na matumaini mapya.

Ndugu Wananchi, vilevile, mwenge wa uhuru umekuwa chombo muhimu cha kuhamasisha uzalendo, kujitolea pamoja na kuchochea shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Hii ni kutokana na ukweli kuwa wakati wote mbio za mwenge zimekuwa zikihimiza kasi ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika jamii za Watanzania.

Ndugu Wananchi, mbio za mwenge wa uhuru zimekuwa zikitatua changamoto za wananchi wa maeneo ya pembezoni, zikikemea vitendo vya ubaguzi, dhuluma, rushwa, wizi, ufisadi na kuhamasisha mapambano dhidi ya maradhi, umaskini na ujinga.

Ndugu Wananchi, licha ya hayo, maono ya ushiriki wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa bara la Afrika yamechagizwa na falsafa hii ya mwenge wa uhuru.

Ndugu Wananchi, kati ya mambo yaliyonifurahisha katika sherehe za leo ni kaulimbiu ya mbio za Mwenge za mwaka huu isemayo: “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”.

Kaulimbiu hii ni halisi na imebeba vipaumbele muhimu sana vya kitaifa vya mwaka 2024. Kaulimbiu hii ni wito kwa Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao mchakato wake umeshaanza. Kaulimbiu hii, vilevile, inatukumbusha Watanzania wote wenye sifa ya kuchagua na kuchaguliwa kushiriki uchaguzi huo ifikapo Oktoba 2024.

Aidha, inatukumbusha wananchi wote kutumia fursa ya kuwachagua wenyeviti wa vitongoji, vijiji na mitaa, zoezi litakalokwenda sambamba na upatikanaji wajumbe wa halmashauri kuu za vijiji. Viongozi hao ni muhimu sana kutokana na ukweli kwamba wako karibu zaidi na wananchi na wanahusika moja kwa moja na utekelezaji wa mipango na mikakati ya kuwaletea wananchi maendeleo katika maeneo yao utawala.

Ndugu Wananchi, Kaulimbiu hii kwa upande mwingine, inaweka msisitizo kwa jamii nzima kushiriki kikamilifu katika suala la uhifadhi na utunzaji wa mazingira. Hii ni kutokana na ukweli kwamba suala la utunzaji wa mazingira linamhusu kila mmoja wetu. Kaulimbiu hii kwa maneno mengine, inatukumbusha wajibu wetu wa kuhakikisha dunia inaendelea kuwa mahali salama kwa viumbe vyote kutokana na ukweli kwamba shughuli za binadamu ndizo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikisababisha uharibifu wa mazingira.

Ndugu Wananchi, katika kuiishi kaulimbiu hiyo, mbio za mwenge wa uhuru za mwaka huu zitaendelea kusisitiza kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa. Msisitizo mkubwa utaelekezwa katika kupanda miti, uhifadhi miti, misitu, mapori na uoto wa asili, usafi wa miji na makazi yetu, udhibiti wa taka ngumu na taka hatarishi, uhifadhi wa vyanzo vya maji na ardhi oevu.

Ndugu Wananchi, sambamba na kaulimbiu hii, mbio za mwenge wa uhuru zitaendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii ya Watanzania kuhusu umuhimu wa lishe bora, mapambano dhidi ya rushwa, VVU/ukimwi, matumizi ya dawa za kulevya na ugonjwa wa malaria.

Ndugu Wananchi, dhamira ya Serikali zetu zote mbili ni kuboresha huduma za jamii na kuinua ustawi wa maisha ya Watanzania. Jitihada kubwa za Serikali zinaelekezwa katika kuboresha miundombinu ya

barabara, nishati ya umeme, upatikanaji wa huduma za uhakika za maji safi na salama mijini na vijijini. Vilevile, Serikali zote zinatekeleza dhamira ya kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya na elimu.

Pia, kuongeza tija katika kilimo, utalii na kuimarisha sekta ya viwanda na mazingira bora ya uwekezaji. Kipekee nitumie nafasi hii kuipongeza sana Kamati ya Maandalizi ya mbio za mwenge kwa kuona umuhimu wa kujumuisha masuala muhimu ya kuweka kipaumbele katika mbio za mwenge kwa mwaka 2024.

Ndugu Wananchi, Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira kutokana na shughuli za binadamu zisizo endelevu. Athari za uharibifu wa mazingira ni pamoja na ukame uliokithiri, kuongezeka kwa kina cha bahari, mafuriko, magonjwa ya mlipuko, kuongezeka kwa joto na kuenea kwa wadudu waharibifu, magonjwa ya binadamu, mimea na wanyama pamoja na kuharibika kwa mifumo ikolojia ya viumbe vyote.

Kutokana na athari hizo na nyingine nyingi, ili ufanisi uweze kupatikana ni wazi kuwa kila Mtanzania anawajibika kuwa sehemu ya utekelezaji wa mikakati yote ya Kitaifa ya utunzaji wa mazingira.

Ndugu Wananchi, Serikali tayari imeshaweka mifumo imara kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 ambayo imeweka masharti yanayozuia uharibifu na uchafuzi wa mazingira kutokana na shughuli za kiuchumi na kijamii. Pia, imeweka Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali Maji ya mwaka 2009 inayozuia shughuli za kibinadamu zaidi ya ukomo wa mita 60 kutoka kwenye chanzo cha maji. Vilevile,

inatekeleza Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021, Mkakati wa Taifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2021. Mifumo hiyo imewekwa kwa lengo la kuhakikisha suala la utunzaji wa mazingira linasimamiwa ipasavyo na kila mhusika anafahamu wajibu wake kisheria.

Ndugu Wananchi, kama nilivyogusia hapo awali, Viongozi wa Serikali za mitaa ni muhimu sana katika kusimamia shughuli za maendeleo ya wananchi. Licha ya hayo, majukumu yao mengine ni pamoja na kusimamia ulinzi na usalama na kuhakikisha wananchi wanaishi kwa utulivu na amani. Kutokana na umuhimu wa majukumu yao katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii suala na uchaguzi wa

viongozi wenye sifa za kusimamia shughuli zote hizo ni muhimu sana.

Hivyo basi, nitoe rai kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu wa 2024 ili Taifa letu liweze kufikia matarajio na malengo yanayokusudiwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!