JESHI la Polisi nchini Tanzania limesema, linamshikiliwa kiongozi wa chama cha kikuu cha upinzani nchini humo cha Chadema, Freeman Mbowe kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo za ugaidi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Mbowe na wenzake 14, walikamatwa na Polisi mkoa wa Mwanza, saa 8 usiku wa kuamkia Jumatano tarehe 21 Julai 2021, katika Hotel ya Kingdom, walipokuwa wamefikia.
Siku hiyo, Mbowe alikuwa aongoze kongamano la kudai katiba mpya jijini Mwanza na kujikuta akiishia mikononi mwa polisi. Alisafirishwa jana Jumatano kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam.
Leo Alhamisi, tarehe 22 Julai 2021, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime ametoa taarifa juu ya kushikiliwa kwa Mbowe akisema, alikuwa akichunguzwa juu ya tuhuma mbalimbali.
“…Mbowe anashikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na tuhuma zinazomkabili za kula njama ya kufanya vitendo vya kigaidi ikiwemo kuua viongozi wa serikali ambapo wenzake sita walishafikishwa mahakamani,” amesema Misime
Amesema, uchunguzi unaoendelea Mwanza kutokana na kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, ukibaini kuna sheria aliyovunja, “hatutasita pia kumfikisha mahakamani pamoja na viongozi wenzake wanaoshikiliwa kule.”
Leave a comment