WANAWAKE wawili na watoto wao wa familia ya Marehemu Amiri Mrisho wa Dar es Salaam wamemuomba Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuingilia ili kurejeshewa miili ya eneo la ardhi waliloachiwa na mume wao aliyefariki mwaka 2006. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Eneo hilo la kiwanja namba 108 Port Access kilichopo eneo la Mapambano wilayani Temeke, Dar es Salaam limekuwa na mgogoro kwa takribani miaka 15 sasa baada ya mmoja wa mtoto wa Marehemu Mrisho, Sophia Mrisho kudaiwa kuliuza kinyemela kwa Kamapuni ya Nahla Development ya jijini humo.
Eneo hilo lenye zaidi ya ukutwa wa ekari mbili lina wafanyabiashara zaidi ya 2000 ambao wamekuwapo hapo wakiendesha shughuli za ujasiliamali kama mafundi milango, vitanda na kadhalika. Ambao nao wameobwa wasitimliwe eneo hilo.
Kwa mujibu wa Anseline Mrisho, Mjane wa Mrisho, alisema mtoto wao huyo mmoja ambaye wanamchukulia kama msaliti alifungua kesi ya kudai mirathi namba 167 ya mwaka 2006 katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo.
Anseline alisema mchakato wa kuuzwa kwa kiwanja hicho namba 108 ni wa kitapeli kwa kuwa baada ya kufariki mumewe hakuna kikao cha familia ambacho kilikaa na kujadili kuuza eneo hilo au kugawana mirathi.
Alisema wakati wakiwa wamefungua kesi ya madai namba 94 katika Mahakama Kuu ya Tanzania ghafla wanakutana na notisi kutoka Ofisi ya Ardhi Mteule Temeke ambaye anajulikana kwa jina la P.0 Masoy akiwataarifu kuwa ofisi yake inakusudia kuhamisha milki ya kiwanja tajwa kwenda kwa ndugu NAHLA Development Limited S.L.P 10507 Dar es Salaam.
“Sisi tunamlilia Rais Samia kuwa sisi wajane tumeporwa eneo letu na Kampuni ya NAHLA Development, eneo hilo tunamiliki kwa zaidi ya miaka 40 sasa mtu anakuja na kulazimisha kununua kwa bei anayotaka hili halikubaliki, kwani hakuna siku tumekaa tukakaa kikao cha familia na kuteua mtu wa kufungua mirathi,” amesema.
Mjane huyo alisema hadi sasa hati ya eneo hilo wanayo hivyo wanashangaa kwanini mahakama na wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuwa ikiwapuuza pamoja na ushahidi uliopo.
Anseline alisema marehemu Mrisho ameacha watoto 22 lakini kuna mazingira ambayo yalitumika kumrubuni mwanao Sophia kupitia madalali wa Kampuni ya Tambaza kuuuza eneo hilo kinyemela.
“Mbaya zaidi tumeenda kuonana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi lakini hajatusikiliza bali alituambia hawezi kufanya lolote kwa sababu tumekuwa tukifungua kesi na kushindwa,” amesema.
Naye Mjane Amina Mrisho alimuomba Rais Samia kuunda tume ya uchunguzi katika sakata hilo kwa kuwa hata maamuzi ya mahakama yamekuwa yakipuuzwa kwani wakati kesi inaendelea inakuja notisi jambo ambalo sio sahihi.

“Rais wetu tunakukimbilia wewe baada ya kukosa msaada katika mamlaka husika ambazo zimeziba masikio na macho ili kutimiza azma yao ya dhuluma kwa makusudi.
Kwa upande wake mtoto wa marehemu, Rachel Mrisho alisema wanaungana na mama zao katika kudai eneo lao kwa sababu taratibu za manunuzi hazikufanyika kihalali.
Alisema siku ambayo inatajwa kuwa kulifanyika mnada hakuna mnada ambao ulifanyika kwa kuwa huyo mteja alikuwa ndani ya gari na Kampuni ya Udalali ya Tambaza ikashiriki kuwahujumu.
Rachel alisema iwapo familia ingekuwa na lengo la kuuza ingeuza kwa bei ambayo ilitolewa na mthamini ambayo ni Sh.5.4 bilioni lakini katika mazingira ya kutatanisha eneo hilo linadaiwa kuuzwa kinyemela Sh.2.5 bilioni bei ambayo hatuko tayari kuuza.
“Eneo hili lina thamani kubwa kwani mwaka 2006 lilikuwa na thamani ya Sh.5.4 bilioni kwa nini liuzwe Sh.2.5 bilioni, mbaya zaidi baada ya hicho kinachodaiwa kuuzwa mgawaji wa fedha alikuwa Kampuni ya Udalali ya Tambaza ndiye aligawa fedha kwa wanafamilia aliowarubuni wakiongozwa na mchonga dili Sophia,” alisema.
Rachel alisema kibaya zaidi dalali alichukua Sh.637 milioni kati ya Sh.2.5 bilioni ambapo wanafamilia waliorubuniwa kila mmoja akipewa Sh.98 milioni kiasi ambacho sio cha haki.
Alisema familia inakosa imani na Waziri Lukuvi kutokana na kutotaka kuwasikiliza lakini mbaya zaidi hata sanduku la posta ambalo limetumiwa kuwafikishia notisi iliyotoka tarehe 5 Julai 2021 ofisi ya ardhi Temeke ni ya uongo lengo ni wazi kuwa wizara yake inahusika,” alisema.
Akizungumzia sakata hilo, Kamishina wa Ardhi Dar es Salaam, Idrisa Kayera alisema suala hilo analijua ila kinachotakiwa ni mahakama kuhojiwa kwanini inatoa uamuzi huo wa kusema kuwa uuzaji ni halali.
Kamishina huyo alisema wao wametoa notisi kulingana na sheria kutaka hivyo na sio kwamba wanaegemea upande wowote na kuitaka familia kuchukua hatua za kisheria kupinga notisi
Kwa upande wake, Waziri Lukuvi alivyotafutwa ili kuelezea shutuma hizo alisema yeye kama waziri anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyopo na sio kubeba upande wowote.
Alisema mgogoro huo anaujua na amekuwa akiushughulikia kila anavyohitajika na kwamba mara ya mwisho aliwaunganisha wana familia hao na Jaji Kiongozi Eliaza Feleshi ili aweze kuwasikiliza.
“Hawa watu nimekutana nao hapa Dar es Salaam, nikawaunganisha na Jaji Feleshi ili aweze kumaliza hilo jambo kwa kuwa sina mamlaka ya kulimaliza mimi ni jambo la kimahakama siwezi kuingilia au kubadilisha hukumu ya mahakama,” amesema.
Leave a comment