Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Pato la kila Mtz dola 1,200, TRA yavunja rekodi
Habari za SiasaTangulizi

Pato la kila Mtz dola 1,200, TRA yavunja rekodi

Spread the love

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema Tanzania imeendelea kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa pato la kati, ikimaanisha pato la wastani la kila mwananchi kwa mwaka (GNI per capital) sasa limeongezeka kutoka dola za Marekani 1,080 mwaka 2019 hadi kufikia dola 1,200 mwaka 2022. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Pia amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kukua licha ya athari kubwa za mlipuko wa UVIKO-19 duniani pamoja na vita za Urusi na Ukraine na pia huko Mashariki ya Kati.

Amesema matatizo haya yaliutikisa uchumi wa Tanzania uliokuwa umefikia wastani wa ukuaji wa zaidi ya 7% na kuushusha hadi 4.2% mwaka 2020.  Hata hivyo, hivi sasa ukuaji umefikia 5.2% kutokana na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Matinyi ametoa kauli hiyo leo Jumapili wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam kuhusu miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani.

Amesema Serikali pia imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambapo kwa sasa ni chini ya 4% – kiwango ambacho ni miongoni mwa viwango bora katika nchi za jumuiya za kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama, kama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Vile vile, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa toshelezi ambapo katika kipindi chote cha miaka mitatu hadi Desemba 2023, nchi ilikuwa na akiba inayotosha kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi kwa miezi 4.5, ikiwa ni kiwango cha juu ya lengo la miezi 4. Akiba hiyo ni sawa na dola za Marekani bilioni 5.4,” amesema.

Kuhusu kusanyaji mapato amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kufanya vizuri katika kipindi cha miaka mitatu kwa kufuata mwongozo wa Rais wa kujenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara na kujali changamoto wakati wa kukusanya kodi.

Amesema makusanyo yamefikia Sh 24.14 trilioni kwa mwaka 2022/23 kutoka Sh 18.15 trilioni mwaka 2020/21 ikiwa ni ongezeko la Sh 5.99 trilioni.

Aidha, amesema kwa mwezi Desemba 2023, TRA ilivunja rekodi ya ukusanyaji ya kila mwezi baada ya kufanikiwa kukusanya Sh  3.05 trilioni licha ya kuwa wastani kwa mwaka huu hadi sasa ni Sh 2.13 trilioni.

“Ni vema kufahamu kwamba hadi kufikia tarehe 20 Machi, 2024, TRA ilikuwa imeshakusanya kiasi cha Sh  19.21 trilioni, ikiwa ni dalili mkwamba itavuka kiasi cha mwaka uliopita,” amesema.

Kuhusu uwekezaji, Matinyi amesema katika kipindi mwaka Machi 2021 hadi Machi 2024 Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimefanikiwa kusajili jumla ya miradi 1,188 ambayo ilikadiriwa kuwekeza kiasi cha mtaji wa dola za Marekani milioni 15,041 na kutoa jumla ya ajira 345,464.

Amesema kati ya miradi hiyo asilimia 35 inamilikiwa na Watanzania, asilimia 41 ni ya Wageni na asilimia 24 ni ya ubia kati ya Watanzania na wageni.

Aidha, amesema Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Uwekezaji (National Investment Steering Committee – NISC) ilitoa idhini ya kusainiwa mikataba ya utekelezaji kwa miradi 16.

“Miradi hiyo yenye hadhi ya mirahi mahiri ni pamoja na Mradi wa Bagamoyo Sugar Limited; Mradi wa Kagera Sugar Limited; na Mradi wa Mtibwa Sugar Estate Limited,” amesema.

Aidha, amesema kwa mujibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, thamani ya uwekezaji katika taasisi zinazosimamiwa na Ofisi hiyo imeongezeka kutoka Sh 70 trilioni mwaka 2021 hadi kufikia Sh 76 trilioni mwaka 2023 – sawa na ongezeko la 8.6%.

“Sababu ya ongezeko hili ni Serikali ya Awamu ya Sita kuongeza mitaji kwa kiasi cha Sh 5.5 trilioni katika mashirika ya kimkakati kwa maslahi ya taifa,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!