Wednesday , 8 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Nyuki wadhibiti tembo waharibifu kwa asilimia 99
Habari Mchanganyiko

Nyuki wadhibiti tembo waharibifu kwa asilimia 99

Spread the love

 

IMEELEZWA kuwa matumizi ya uzio wa mizinga ya nyuki umewezesha kudhibiti tembo waharibifu ambao wamekuwa wakitoka Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa na Nyerere wilayani Kilombero mkoani Morogoro kwa asilimia 99.5. Anaripoti Selemani Msuya, Morogoro … (endelea). 

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kikundi cha Mizinga ya Nyuki cha Njokamoni, kilichopo kijiji cha Mang’ula A, wilayani Kilombero mkoani Morogoro, Ahmed Churi wakati akizungumza na waandishi wa habari waliokuwa katika ziara ya kuangalia Ushorba wa Tembo Kilombero.

Ziara hiyo ya waandishi iliratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), kupitia ufadhili wa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.

Churi amesema wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakiteswa na tembo kwa miaka mingi, hali ambayo ilichangia wananchi kushindwa kujihusisha na kilimo, ila ubunifu huo wa kutumia uzio wenye mizinga ya nyuki umefanikiwa kwa asilimia 99.5.

Makamu Mwenyekiti huyo amesema awali Shirika lisilo la Kiserikali la Mpango wa Kuhifadhi Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP), liliwawezesha kutumia uzio wa pilipili iliyochanganywa na oili ambapo walipaka kwenye vitambaa na kuwafanya tembo wakimbie kwa kuwa walikuwa wanapiga chafya, ila baadae walibadilisha mbinu.

“Mwaka 2012 tulikuwa tunatumia mbinu ya kuweka pilipili iliochanganywa na oili, ila tembo waligundua wakaanza kuingia kinyumenyume, hivyo ndio tukaja na uzio wa mizinga ya nyuki ambayo imeweza kufanya kazi nzuri,” amesema.

Churi amesema ubunifu huo wa kutumia uzio wenye mizinga ya nyuki umekuwa na faida mara mbili, mosi wanakikundi wa Njokamoni wanapata asali na pili tembo wamedhibitiwa kwani wakitikisa uzio nyuki wanatoka kuwang’ata.

Amesema kupitia ubunifu huo wakulima na makazi ya wananchi katika vijiji husika wamekuwa salama na mavuno yameongezeka.

“Mradi wetu una mizinga 76, upo kati ya hifadhi ya Taifa ya Udzungwa na mashamba ya wananchi Kijiji cha Sole, kupitia mradi huu umezuia tembo kwa asilimia 99.5. Ila asali ambayo tunapata ni ndogo kwa kuwa eneo hili lina majimaji, hivyo nyuki wanashindwa kuchavusha,” amesema.

Churi alisema kutokana na changamoto ya upatikanaji wa maua uzalishaji wa asali umekuwa mdogo, hivyo kupelekea mapato kuwa madogo.

Mwekahazina wa kikundi hicho, Glory Nyachi amesema mikakati yao ni kuhakikisha wanapata wataalam ambao watawasaidia kupata fedha za kununua mizinga zaidi.

Nyachi amesema dhamira yao ni kuitangaza asali ya Njokamoni katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku akiomba wataalam wa ufugaji nyuki kuwatembelea ili waweze kuongeza uzalishaji.

“Kikundi chetu kina wanachama 17 ambapo tumeanza kupata manufaa na kila mwisho wa mwaka tunagawana shilingi 50,000 kila mmoja na pia tunarajia kununua viti kwa ajili ya ofisi ya kijiji,” anasema.

Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Mahusiano kati ya Tembo na Binadamu (HEC), kutoka STEP, Kim Lim amesema lengo la ujio wao lilikuwa ni kurejesha Ushoroba wa Tembo Kilombero, ila baadae waliona ni vema kuwezesha vikundi kikiwemo Njokamoni.

Lim amesema mbinu hiyo ya kutumia mizinga imewezesha kuzuia uharibifu wa mazao unaosababishwa na tembo.

Amesema shirika lao linafanyakazi na vikundi saba kwa upande wa mradi wa uzio wa mizinga ya nyuki ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia tembo kuingia katika mashamba ya watu na kuharibu mazao.

“Kupitia uzio au fensi ya mzinga ya nyuki wanakikundi wanapata asali na kujipatia fedha ambazo hutumia kuanzisha miradi mingine au kugawana kila mwaka kutokana na makubaliano ya kikundi husika,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Matumizi ya nishati safi sio anasa, ladha ipo

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi kwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC, SILABU waungana kufikisha elimu ya fedha majumbani

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano...

AfyaHabari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kisukari cha mimba ni nini?

Spread the loveKisukari cha mimba ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi...

Habari Mchanganyiko

Mafunzo kwa bodaboda 395 yamkuna Meya Dodoma

Spread the loveNAIBU Meya wa Jiji la Dodoma, Asma Karama amepongeza mafunzo...

error: Content is protected !!