Saturday , 30 September 2023
Home Kitengo Biashara NMB yawa benki ya tatu kwa faida Afrika Mashariki
Biashara

NMB yawa benki ya tatu kwa faida Afrika Mashariki

Spread the love

Benki ya NMB imeshika nafasi ya tatu kwa ukubwa wa faida katika ukanda wa Afrika Mashariki ikiwa ni kutokana na mafanikio yake kiutendaji hasa ufanisi katika uendeshaji na utoaji wa huduma bora za kibenki nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu benki hiyo imetengeneza faida baada ya kodi ya Sh  262 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 27 ukilinganisha na nusu ya kwanza ya mwaka 2022.

Kutokana na kutengeneza kiasi hicho cha faida, NMB imeshika nafasi ya tatu kwa ukubwa wa faida kati ya mabenki yote ndani ya ukanda huu wa Afrika Mashariki, ikitanguliwa na Benki ya Equity pamoja na Benki ya KCB zote kutoka nchini Kenya ambazo zimepata faida ya Sh 430 bilioni na Sh  264 bilioni mtawalia. NMB imepanda kutoka nafasi ya 10 mwaka 2018 hadi kufikia nafasi ya tatu sasa.

Takwimu na uchambuzi wa hivi karibuni wa masoko ya hisa katika ukanda huu unaonyesha kuwa taasisi hiyo kubwa ya fedha nchini yenye mali zenye thamani ya zaidi ya Sh 11 trilioni imekua kiushindani na kuimarika sokoni katika miaka ya hivi karibuni, huku bei ya hisa zake sokoni ikiongezeka kwa takribani asilimia 28 tangu kutangazwa kwa matokeo yake ya kifedha ya nusu mwaka 2023 hadi kufikia sh 4,440 kwa kila hisa Septemba 8 2023.

Kutokana na kufanya vizuri kifedha, mtaji wa Benki ya NMB katika soko la hisa umekua kutoka Sh 1.38 trilioni mwaka 2018 hadi kufikia mtaji wa kiasi cha Sh 2.22 trillioni tarehe 8 Septemba 2023, hivyo kuifanya NMB kuwa kampuni ya pili kwa ukubwa katika soko la Tanzania ikitanguliwa na kampuni ya TBL.

Pia NMB imekuwa kampuni ya sita kwa ukubwa ndani ya kanda ya Afrika Mashariki, Shelisheli na Mauritus, ikitokea nafasi ya 14 mwaka 2019. Kampuni ya Safaricom Kenya ndiyo inayoongoza katika ukanda huu ikiwa na mtaji wa zaidi ya Sh  nne trilioni.

Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, mafanikio haya makubwa yanatokana na mazingira wezeshi ya kibiashara yanayowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na uimara wa uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Ruth aliongeza kuwa ufanisi wa taasisi hiyo pia umechangiwa na miaka mingi ya ukuaji endelevu pamoja na utekelezaji makini wa mpango mkakati wa uendeshaji wa benki hiyo.

Mwaka 2022, NMB ilipata faida kabla ya kodi ya Sh 617 bilioni na kuweka historia ya faida kubwa kuwahi kutengenezwa na taasisi yoyote ya fedha nchini.

Jarida la Euromoney limeitangaza benki ya NMB kama benki bora zaidi Tanzania 2023, hii ikiwa ni mara ya 10 ndani ya miaka 11 kwa benki hiyo kubwa kupata tuzo hiyo inayo heshimika duniani kote.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Dk. Edwin Mhede, alisema wamejipanga kuendelea kuchangia kikamilifu ukuaji wa uchumi wa nchi na ujenzi wa taifa kwa ujumla.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Biashara

Mwezi wa kutoboa ni huu, cheza Keno Bonanza utusue Maisha

Spread the love MWEZI wa Oktoba wengi hupenda kuuita mwezi wakutoboa wakiwa...

Biashara

Wataalam Uganda wapewa darasa teknolojia mpya uchimbaji madini katika maonesho Geita

Spread the loveMAONESHO ya Teknolojia ya Madini yamezidi kuwa darasa kwa wadau...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Stamico yafungua fursa za kiuchumi kwa makundi maalumu

Spread the loveSHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limemwaga neema kwa watu...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Maabara ya bilioni 5 upimaji madini yazinduliwa Geita, inapima kwa mionzi

Spread the loveZaidi ya Sh bilioni tano zimewekezwa katika kampuni ya MSALABS...

error: Content is protected !!