WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameuagiza Wakala wa Majengo (TBA) kuhakikisha unakusanya deni la Sh 81.5 bilioni wanazodai kwa wapangaji wao sambamba na kuwaondoa wadaiwa sugu katika nyumba hizo ili upatikanaji wa fedha hizo usaidie utekelezaji wa miradi mingine nchini. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma… (endelea).
Bashungwa ameyasema hayo jana tarehe 7 Septemba 2023 jijini Dodoma alipofanya ziara kwa mara ya kwanza kwa Wakala huo na kuzungumza na menejimenti ya TBA na kueisitiza uwekezaji wenye tija kwa watumishi na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Bashungwa ameagiza TBA kuhakikisha wanakuja na mikakati itakayosaidia kujenga nyumba za bei nafuu hasa kwa vijana wanaoajiriwa katika utumishi wa umma hususan Dodoma ili kumudu gharama za maisha.
“Kuna vijana ambao wanaingia kwenye kada ya utumishi wa umma na bado hawajawa na uwezo wa kujijengea nyumba, kupitia TBA mnaweza kujenga nyumba za bei rahisi kwa ajili ya vijana hao ili kuwarahisishia gharama za maisha”, amesema Bashungwa.
Pia ameutaka uongozi wa TBA kuwa na utaratibu wa kuwajengea uwezo wataalamu walionao ili kuenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya teknolojia hasa katika suala la ujenzi na uendelezaji wa majengo mbalimbali.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, amesema TBA itatafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo na kumuahidi Waziri Bashungwa kuandaa mikakati mizuri itakayosaidia Wakala huo kutoa huduma bora kwa wananchi.
Awali, Arch. Kondoro ameeleza kuwa hadi sasa TBA inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 3500 za watumishi wa umma eneo la Nzuguni Dodoma ambapo awamu ya kwanza ya nyumba 150 utekelezaji umefikia asilimia 95 na awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 150 utekelezaji wake umefikia asilimia 10.
Miradi mingine ni ujenzi wa nyumba 20 za Viongozi jijini Dodoma ambazo zililenga kukabiliana na uhaba wa nyumba za Viongozi baada ya Serikali kuhamia Dodoma ambapo mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na nyumba zimeanza kutumiwa na viongozi.
Leave a comment