October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ndoto ya Odinga kuwa rais wa Kenya ‘imezima’

Spread the love

NDOTO ya Raila Odinga, mtoto wa makamu wa rais wa Kwanza wa Kenya, Jaramogi Odinga, kuwa rais wa Jamhuri ya Kenya imeonekana kuzima kabisa baada ya leo tarehe 5 Septemba, 2022 mahakama ya juu kuidhinisha ushindi wa Dk. William Ruto.

Hii imekuwa mara ya tano kwa Raila Odinga, mwenye umri wa miaka 77, kugombea urais.

Odinga aligombea urais mara ya kwanza mwaka 1997 ambapo alimaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Daniel Arap Moi na Mwai Kibaki.

Alijiondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2002 na kumuunga mkono Mwai Kibaki dhidi ya Uhuru Kenyatta.

Mwaka 2007, Raila Odinga aligombea urais dhidi ya Mwai Kibaki na akapata kura milioni 4.35 dhidi ya milioni 4.58 za Mwai Kibaki. Maandamano yalitokea, ghasia na mauaji ya maelfu ya watu. Kesi ilifunguliwa katika mahakama ya uhalifu wa kivita ICC. Aliunda serikali ya umoja wa taifa na Kibaki, na kuwa waziri mkuu. Serikali hiyo ilijulikani kama ‘nusu mkate’.

Mara ya tatu, Raila aligombea urais mwaka 2013 ambapo alishindwa na Uhuru Kenyatta. Alipata kura milioni 5.34. Kenyatta alipata kura milioni 6.17. Alipinga matokeo hayo mahakamani lakini ikatupiliwa mbali.

Mara ya nne alishindwa na Uhuru Kenyatta mwaka 2017. Kenyatta alipata kura milioni 7.7 huku Raila akipata kura milioni 6.3. Odinga alikataa matokeo hayo na kuelekea mahakamani ambapo matokeo yalitupiliwa mbali na kuagiza uchaguzi kurudiwa.

Hata hivyo, alisusia uchaguzi wa marudio uliofanyika na uhuru kupata kura milioni 7.48 huku Raila akipata kura 73,200.

Alijiapisha kama rais. Uhuru Kenyatta alifanya mazungumzo na Raila na kukubaliana kushirikiana katika kuliunganisha taifa la Kenya.

Mara ya tano Raila Odinga kugombea urais ni mwaka huu 2022 ambapo ameshindwa na Dk. William Ruto. Aliwasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa Ruto wa kura milioni 7.1 dhidi ya kura zake alizopata milioni 6.9.

Hata hivyo,  Mahakama imetupilia mbali kesi hiyo kwa kukosekana ushahidi na kusema tume ya uchaguzi IEBC iliandaa uchaguzi huo kwa njia ya wazi.

Wachambuzi wanasema itakuwa vigumu kwa Raila Odinga (77) kugombea urais miaka mitano ijayo kwa sababu ya umri. Wakati huo, atakuwa na umri wa miaka 82.

Viongozi walio karibu na Raila wamesema hawakubaliani na maamuzi ya mahakama

Mawakili wa Raila Odinga hata hivyo, wamesema kwamba wanaheshimu lakini hawakubaliani na maamuzi ya mahakama kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa Dk. William Ruto.

Kiongozi wa mawakili wa Odinga, James Orengo, amesema kwamba “mahakama ilikosea katika uamuzi wake.”

Mgombea mwenza wa Odinga, Martha Karua naye ameandika ujumbe wa twitter akisema kwamba “mahakama ya juu imefanya uamuzi. Naheshimu uamuzi huo lakini sikubaliani nao.”

Katibu mkuu wa wafanyakazi COTU, ambaye pia ni mfuasi mkubwa wa Raila Odinga, Francis Atwoli amesema kwamba anakubali maamuzi ya mahakama. Makala haya imeandaliwa na Mwandishi wetu kwa msaada wa mitandao ya kimataifa.

error: Content is protected !!