RAIS mteule wa Kenya, William Ruto anatarajiwa kuapishwa Jumanne, tarehe 13 Septemba, 2022. Hii ni baada ya Mahakama ya Juu Milimani kutupilia mbali ombi la mpinzani wake Raila Odinga, kutaka ushindi wa Ruto ubatilishwe. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Mpangilio wa shughuli utafanyika katika muda wa wiki moja ijayo kabla ya hafla ya kuapishwa kwa Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua.
Kwa mujibu wa kifungu cha 141 cha Katiba ya Kenya rais mteule anatakiwa kuapishwa Jumanne ya kwanza baada ya siku saba za mahakama kutoa uamuzi hivyo, kuapishwa kwa rais mteule William Ruto kutafanyika Jumanne ijayo.
Rais mteule huyo atachukua madaraka kwa kula kiapo cha utii na kuapa kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake.
Wakati wa hafla hiyo Rais Mteule ataapishwa hadharani mbele ya Jaji Mkuu au Naibu Jaji Mkuu ikiwa Jaji mkuu hayupo.
Baada ya kuapishwa, Rais atatia saini cheti cha kuapishwa na Rais anayemaliza muda wake atamkabidhi Rais zana za mamlaka, upanga na Katiba.
Hayo yanajiri baada ya Mahakama hiyo jana Jumatatu kuthibitisha kuchaguliwa kwa Ruto kama Rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya.
Akisoma uamuzi huo, Jaji Mkuu Martha Koome alisema Ruto alipata asilimia 50 pamoja na kura moja kama inavyohitajika kisheria.
Leave a comment