Thursday , 2 May 2024
Home Kitengo Maisha Elimu NBC yaunga mkono ufaulu somo la hesabu Ubungo
ElimuHabari za Siasa

NBC yaunga mkono ufaulu somo la hesabu Ubungo

Spread the love

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imeendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini, kwa kufadhili mpango wa kuchochea kiu ya kufundisha na kujifunza somo la Hisabati katika Jimbo la Ubungo, jijini Dar es Salaam unaofahamika kama KiuHisabati. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Mpango huo ulioasisiwa na Mbunge wa Ubungo, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, unalenga kuongeza ufaulu kwenye somo hilo kupitia motisha mbalimbali ikiwemo tuzo na zawadi hususani fedha taslimu kwa walimu wanaofaulisha wanafunzi zaidi kwenye somo hilo.

Aidha, kupitia mpango huo pia wanafunzi waliofanya vizuri somo hilo wananufaika na ufadhili wa mahitaji ya kimasomo wanapofaulu kwenda kidato cha tano kwa shule za serikali.

Hafla ya utoaji wa tuzo hizo kwa walimu hao imefanyika mwishoni mwa wiki jimboni humo ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara ambae pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Anamringi Macha, viongozi waandamizi wa chama na serikali Mkoa wa Dar es Salaam, walimu, wananchi pamoja na maofisa wa benki ya NBC wakiongozwa na Meneja wa Benki hiyo tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Anne Mwaisaka.

Akizungumzia hatua hiyo, Macha alimpongeza mbunge huyo kwa kubuni mpango huo huku akiishukuru na kuiomba benki ya NBC iangalie namna inavyoweza kuutanua mpango huo uweze kufika maeneo mbalimbali nchini ili uwanufaishe walimu na wanafunzi wengi zaidi hatua ambayo alisema itasaidia kuchochea kasi ya ufaulu wa somo hilo.

‘’Hesabu ndio nguzo mama ya masomo yote kwenye mfumo wa elimu yetu. Jitihada zozote zinazofanywa na wadau mbalimbali kuongeza ufaulu kwenye somo hili zinaungwa mkono na chama pamoja na serikali kwa ujumla.

“Hii ndio sababu tunampongeza Mbunge wa jimbo la Ubungo kwa ubunifu huu mzuri na zaidi pia tuishukuru benki ya NBC kwa ufadhili wake kwenye mpango huu…tunaomba sana NBC muangalie namna ya kuutanua zaidi mpango huu’’ alisema Macha.

Akifafanua zaidi kuhusu mpango huo Prof Kitila pamoja na kuishukuru benki ya NBC kuwa mfadhili mkuu wa mpango huo alisema unahusisha walimu na wanafunzi watakaopata daraja la A katika somo la Hisabati na wanafunzi watakaofaulu somo la Hisabati kwa kiwango cha daraja A na B.

“Kila mwalimu wa Somo la Hisabati atapata shilingi 100,000/= kwa kila mwanafunzi atakayepata daraja la A katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne katika somo hilo.

“Mwanafunzi atakayepata daraja A katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne katika somo la Hisabati atanunuliwa vifaa vyote muhimu vya shule, ikiwemo sare, madaftari na vitabu kama atajiunga na shule ya serikali kidato cha tano,’’ alifafanua.

Kwa mujibu wa Prof Kitila, tangu kuanza kwa mpango huo mwaka 2020 tathmini inaonesha kuwa kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaopata alama A na B katika jimbo hilo lakini sio katika kupunguza idadi ya wanafunzi wanaofeli somo la Hisabati.

“Hii inaonesha kuwa programu ya motisha kwa walimu imekuwa na tija katika kuwahamasisha wanafunzi kujifunza zaidi hisabati. Hata hivyo, changamoto bado ni kubwa kwa kuzingatia takwimu kwamba wastani wa ufaulu kwenye somo hili kwa jimbo hili la Ubungo ni asilimia 11 tu huku wastani wa ufaulu kitaifa kwa somo hili ukiwa ni asilimia 19 hadi 20,’’ aliongeza.

Kwa upande wake Mwaisaka alisema hatua ya benki hiyo kufadhili mpango huo ni  muendelezo wa jitihada za taasisi hiyo kuunga mkono mipango ya serikali pamoja na wadau mbalimbali yenye nia ya kuboresha sekta ya elimu nchini.

“Kimsingi ufadhili wetu kwenye mpango huu unalenga kuchochea utoaji wa motisha kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri kwenye somo la Hesabu katika mtihani wa kidato cha nne.

“Tukiwa kama taasisi ya fedha, moja kwa moja tunakuwa wadau wa elimu likiwemo somo la hisabati kwa kuwa shughuli zetu kwa kiasi kikubwa zinazongozwa na hesabu…hivyo tuna wajibu pia wa kuhakikisha ustawi wake,’’ alibainisha.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya walimu na wanafunzi walionufaika na mpango huo, Mwalimu Michael Msembwe kutoka Shule ya Sekondari Kimara ambae aliongoza kwa kufaulisha wanafunzi 20 kwa ufaulu wa Daraja A kwenye somo la Hisabati jimbo la Ubungo alisema ujio wa mpango huo umeongeza chachu na motisha kwa walimu wa somo hilo na wanafunzi kwenye jimbo hilo hatua ambayo alisema inaahidi mustakabali mzuri zaidi katika kuongeza kiwango cha ufaulu wa somo hilo kwa miaka ijayo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!