November 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwongozo wafungwa Zanzibar kutoa malalamiko waja

Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa

Spread the love


CHUO cha Mafunzo Zanzibar, pamoja na wadau mbalimbali ikiwemo na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kimekamilisha mchakato wa kupokea maoni ya uboreshaji rasimu ya mwongozo wa mawasiliano na utoaji malalamiko ya haki za binadamu kwa wanafunzi (wafungwa). Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Mchakato huo umekamilishwa leo Jumatatu, tarehe 26 Septemba 2022, baada ya mwakilishi wa Kamishna wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar, SSP Seif Makungu na Mratibu wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, kufanya ziara katika baadhi ya vyuo vya mafunzo (magereza), kwa ajili ya kukusanya maoni ya wanafunzi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari ya THRDC, SSP Makungu pamoja na Olengurumwa, walitembelea vyuo kadhaa kikiwemo cha Hanyegwa Mchana na Kiinua Miguu, kilichopo Unguja, pamoja vyuo vya  Tungamaa na Wete, wilivyopo wilayani Wete, Pemba.

“Katika ziara hiyo wadau wamefanikiwa kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wanafunzi wanawake, wanaume pamoja na watoto waliopo katika vyuo hivyo kulingana na uhitaji wao katika kulinda haki za binadamu,” imesema taarifa ya THRDC.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kupitia mchakato huo wa ukusanyaji maoni, uliofanyika tarehe 13 na 14 Septemba mwaka huu, wanafunzi 200 walifikiwa, ambapo watoto wanaokinzana na sheria 25, watu wazima 155 na wanawake 20.

Mbali na wanafunzi hao, timu iliyoundwa kwa ajili ya kukusanya maoni hayo, ilikusanya maoini katika taasisi za kiraia takribani 50, ambazo ni mwanachama wa THRDC visiwani Zanzibar.

Rasimu ya mwongozo huo ina lengo la kuboresha mchakato wa utoaji maoni kwa njia rahisi, itakayowezesha malalamiko na mapendekezo ya wanafunzi kufanyiwa kazi kwa wakati.

“Mwongozo huu umelenga kuboresha hali ya mawasiliano na utoaji taarifa za malalamiko katika njia ambazo sasa zitakuwa rasmi na zitakuwa zinasimimamiwa na magereza yenyewe kwa kushirikiana na wadau wa haki hapa Zanzibar. Miongozo hii imetumika katika magereza duniani kote kama njia ya kulinda haki za walioko kuzuini hasa pale wanapokuwa na malalamiko lakini wanakosa njia sahihi za kuziwasilisha,” imesema taarifa ya THRDC.

error: Content is protected !!