HASHIM Salum Hashim, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), amejitosa katika kinyang’anyiro cha Urais wa Zanzibar, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Leo Jumanne tarehe 23 Juni 2020 katika Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar iliyoko Kisiwandui, Hashim amekabidhiwa fomu ya kuwania nafasi ya kugombea urais Zanzibar na Cassian Gallo’s, Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Oganaizesheni Zanzibar.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, amesema kama atafanikiwa kuwa Rais wa Zanzibar, ataiboresha sekta ya michezo visiwani humo pamoja na kurejesha hashima ya Zanzibar kimataifa.
Hashim amesema, endapo atafanikiwa kuwa Rais wa Zanzibar, atahakikisha taifa hilo linapata uanachama kamili katika Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

“Kutokana na uzoefu niliokuwa nao nitahakikisha heshima ya Zanzibar inarudi, tunapata uanachama kamiliwa FIFA na CAF,” amesema Hashim.
Wakati huo huo, Hashim amesema kutokana na uzoefu aliokuwa nao kwenye masuala ya michezo, “Nitahakikisha michezo itapata udhamini wa Asilimia 100 kutoka serikalini sababu mpaka sasa Ligi Kuu Zanzibar inacheza haina mdhamini. Ni wajibu wangu kama mwanamichezo nitahakikisha udhamini unapatikana na michezo inatoa ajira.”
“Kwa hiyo nitahakikisha udhamini unarudi na michezo yote inapata wadhamini sababu vipaji vipo shida ni umasikini tu, uwezo wa kupata CAF tunao na wa kupata FIFA tunao,” amesema
Hashim ambaye amekuwa mwanachama wa 24 wa CCM kuchukua fomu ya kugombea urais wa Zanzibar, ameahidi kwamba, kama chama chake kitamteua kugombea urais na kushinda, ataendelea mazuri aliyoyafanya Dk. Ali Shein, Rais anayemaliza muda wake.
Amesema ataendeleza pale alipoacha Rais Shein, kwenye siasa, afya, elimu na miundombinu.
“Kama chama kikinipa ridhaa ya kupeperusha bendera, nitaanza pale alipoachia Rais Shein katika siasa uchumi, elimu na mambo mengine, na masuala mazima ya michezo,” amesema Hashim.
Wengine 23 waliokwisha kuchukua fumo ni;
- Mbwana Bakari Juma
- Ali Abeid Karume
- Mbwana Yahya Mwinyi :
- Omar Sheha Mussa
- Hussein Ali Mwinyi
- Shamsi Vuai Nahodha
- Mohammed Jaffar Jumanne
- Mohammed Hijja Mohammed
- Issa Suleiman Nassor
- Makame Mnyaa Mabarawa
- Mwatum Mussa Sultan
- Haji Rashid Pandu
- Abdulhalim Mohammed Ali
- Jecha Salum Jecha
- Dk Khalid Salum Mohammed
- Rashid Ali Juma
- Khamis Mussa Omar
- Mmanga Mjengo Mjawiri
- Hamad Yussuf Masauni
- Mohammed Aboud Mohammed
- Bakari Rashid Bakari
- Hussein Ibrahim Makungu
- Ayoub Mohammed Mahmoud
Endelea kufuatilia MwanaHALISI ONLINE & MwanaHALISI TV kwa habari zaidi
Leave a comment