October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mutharika atavuka? Malawi wapiga kura leo

Spread the love

SWALI kubwa linalogubika Malawi na sehemu ya Afrika, ni kwamba Rais Peter Mutharika atashinda kwenye uchaguzi unaofanyika leo Jumanne tarehe 23 Juni 2020 nchini Malawi?

Mutharika anapambana ili kupata ridhaa ya raia wa Malawi kuongoza taifa hilo kwa muhula wa pili.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya miezi mitano Mahakama ya Katiba nchini humo, kufuta matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana kutokana na kuwa na dosari.

Kwenye uchaguzi huo wa Mei 2019, Tume ya Uchaguzi nchini humo ilimtangaza Peter Mutharika kushinda kwa asilimia 38.5. Mutharika na timu yake walishtakiwa kwa kuiba kura.

Lazarus Chakwera, mpinzani mkuu anayeongoza muungao wa upinzani, ndiye anayemtoa jasho Mutharika.

Mgombea anayeonekana kuwafuatia wawili hao kwa kukubalika ni Peter Kuwani.

Kwa mujibu wa sheria mpya ya uchaguzi nchini humo, mshindi sasa atahitaji kupata asilimia 51 ya kura.

Uchaguzi huo unaweza kupunguza sintofahamu iliyochagizwa na maandamano pia vurugu zilizotokana na kupinga matokeo ya uchaguzi wa awali.

Takwimu za kiuchumi zinaonesha, kwamba Malawi imeanguka huku umasikini ukionekana kuota mizizi miongoni mwa raia wake, ukosefu wa ajira umerekodiwa kuwa kiwango cha juu kutokana na taifa hilo kushindwa kukabiliana na ufisadi uliokithiri.

Vyama vyote vya upinzani nchini humo, vimeungana kumuunga mkono Chakwera anayepambana na Mutharika. Mutharika anagombea kuongoza taifa hilo katika awamu ya pili.

Baada ya Mutharika kutangazwa kushinda kiti cha urais, viongozi wa upinzani walipinga matokeo hayo mahakamani, wakidai uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu. Februari mwaka huu, Majaji waliamuru kufutwa kwa matokeo hayo na kurudiwa kwa uchaguzi.

Malawi inakuwa nchi ya pili Afrika matokeo yake ya urais kufutwa na mahakama na kuagizwa uchaguzi urudiwe upya.

Matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2017 nchini Kenya, yalifutwa na mahakama na kuagiza uchaguzi huo kurudiwa. Hata uliporudiwa, Uhuru Kenyatta alishinda tena kuongoza Taifa hilo la ukanda wa Afrika Mashariki.

error: Content is protected !!