October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mdee, Bulaya, Msigwa, Heche waponea chupuchupu

Spread the love

HALIMA James Mdee, John Heche, Peter Msigwa na Ester Bulaya, wametokea kwenye tundu la sindano kufutiwa dhamana. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Hakimu Mkuu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, Thomas Simba, ameeleza kuwa mahakama yake, imejiridhisha kuwa utetezi uliowasilishwa na washitakiwa mahakamani hapo kupinga kufutiwa dhamana zao, “ulikuwa dhaifu.”

Hakimu Simba ameeleza katika uamuzi wake aliyosoma leo Jumatano, tarehe 20 Novemba, utetezi wa washitakiwa hao, haujitoshelezi na hivyo mahakama yake, ina kila sababu ya kufuta dhamana hizo.

Hata hivyo, Hakimu Simba amesema, ameamua kuwachia huru washitakiwa hao, kwa kuwa “uamuzi wa kuwafutia dhamana, ni mkali sana.”

Washitakiwa wote wanne, ni wabunge wa Bunge la Jamhuri. Mdee, ni mbunge wa Kawe (Chadema), Msigwa (Iringa Mjini), Heche (Tarime Vijijini) na Bulaya (Bunda Mjini.

Katika kesi ya msingi Na. 112/2018, washitakiwa hao wanne na wengine watano, wanakabiliwa na mashitaka 13, likiwamo la uchochezi. Washtakiwa wengine katika kesi hiyo, ni mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe; Katibu Mkuu wake, Dk. Vicent Mashinji na manaibu makatibi wakuu, Jonh Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Mshitakiwa mwingine kwenye kesi hiyo, ni Ester Matiko, ambaye ni mbunge wa Tarime Mjini na mweka hazina wa baraza la wanawake la Chadema.

Mahakama ilitoa amri ya kukamatwa kwa wabunge hao, tarehe 15 Novemba 2019.

“Pamoja na kujitetea kwao, bado bado utetezi wao hauna mashiko,” ameeleza Hakimu Simba na kuongeza, “lakini mahakama yangu imeamua kutowafutia dhamana zao. Badala yake, nimetoa onyo kali kwa washitakiwa hawa wote.”

Akichambua hoja moja baada ya nyingine, Hakimu Simba amesema, hatua yao ya kujisalimisha kwenye vituo vya polisi, ilionesha wazi kuhofia kile ambacho kingewakuta hapo mbele.

“Nimepitia hoja za pande zote mbili, na kuona kuwa mahakama isiwafutie dhamana washtakiwa hawa. Nimeona kuwafutia dhamana ni uamuzi hatari… natoa onyo kali tukiruhusu huu mchezo, kesi itakuwa haiishi,” ameeleza.

Hakimu Simba amemtaka Msigwa kupeleka mdhamini mwengine mahakamani kwa mdhamini wake wa awali amekihama chama chake. Amesema, akishindwa kufanya hivyo, atamfutia dhamana yake.

Naye Heche ametakiwa kupeleka wadhamini wake mahakamani hapo, kesi ikitajwa tena. Kesi hiyo itatajwa tena 26 Novemba mwaka huu.

Washtakiwa hao wanne – Heche, Msigwa, Mdee na Bulaya – waliokuwa mikononi mwa jeshi la magereza na polisi kuanzia tarehe 16 Novemba 2019, walifikishwa mahakamani hapo wakiwa chini ya ulinzi mkali na askari wenye silaha za moto na mabomu ya machozi.

Mahakama ilipowachia, wafuasi waliohudhuria kwenye ukumbi namba moja wa mahakama hiyo, walisikika wakisema ‘People’s Power.’

Walipotoka nje kwa furaha, Mdee alikumbatiana na mama yake mzazi na wafuasi wengine. Wenzake wengine, waliondoka kimyakimya.

error: Content is protected !!