November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mdhamini: Nimewasiliana na Lissu, kanijibu hivi 

Spread the love

MDHAMINI wa Tundu Lissu, Ibrahim Ahmed ametoa msimamo wa mdhaminiwa wake, kwamba amepona na hayuko tayari kurejea nchini. Anaripoti Faki Sosi…(endelea).

Ibrahim ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kwamba amewasiliana na mdhaminiwa wake (Lissu), na kutoa msimamo huo akieleza kuhofia usalama wake.

Ibrahim ameeleza, aliwasialiana na Lissu, Mwansheria Mkuu wa Chadema, baada ya Hakimu Mkuu Mkazi wa mahakama hiyo Thomas Simba, kuwataka wadhamini wa hao kupeleka ushahidi kwamba mdhaminiwa wao ni mgonjwa.

Hakimu Simba tarehe 23 Oktoba 2019, aliwataka wadhamini hao kupeleka uthibitisho wa afya ya Lissu ambaye yupo nchini Ubelgiji, baada ya kumaliza matibabu yake.

“Lissu amesema kwa sasa amepona, ila hawezi kuja Tanzania kuhofia usalama wake,” Ibrahim ameieleza mahakama hiyo leo tarehe 21 Novemba 2019.

Lissu na wenzake watatu – Simon Mkina, mhariri wa gazeti la MAWIO,  Jabir Idrissa, mwandishi wa gazeti hilo na Ismail Mehbob, mfanyakazi wa kampuni ya uchapishaji magazeti Jamana – wanakabiliwa  na mashitaka matano mahakamani, likiwamo uchochezi.

Wote wanne, wanatuhumiwa kuandika, kuchapisha na kusambaza taarifa hizo kwenye gazeti la MAWIO la tarehe 14 Januari 2016, kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Kwa mujibu wa upande wa mashitaka, watuhumiwa walitenda kosa hilo jijini Dar es Salaam. Habari ambayo inadaiwa kuwa ya uchochezi, ilibeba kichwa cha maneno kisemacho: “Machafuko yaja Zanzibar.”

Katika shitaka la pili, washatakiwa wote wanne, wanadaiwa kuwa 14 Januari 2016, walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Shitaka la tatu linamkabili mshtakiwa wa tatu, Mehboob ambaye anadaiwa kuwa 13 Januari 2016, katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam, alichapisha gazeti la MAWIO lililokua na taarifa za uchochezi.

Mshitakiwa huyo alidaiwa pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Shitaka la tano linawakabili washtakiwa wote kwa pamoja ambao wanadaiwa kuwa  tarehe 14 Januari 2016,  bila ya kuwa na mamlaka yoyote,  waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya uchaguzi mkuu.

Lissu alishambiliwa kwa risasi tarehe 7 Septemba 2019, akiwa nyumbani kwake eneo la ‘Area D’ jijini Dodoma na kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa mkoa huo.

Baadaye alihamishiwa Nairobi nchini Kenya ambapo tarehe 6 Januari 2018 alipelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi ambapo yupo mpaka sasa.

Shambulizi dhidi ya Lissu, lilitokea muda mfupi baada ya kutoka kwenye mkutano wa Bunge wa asubuhi.

error: Content is protected !!