Spread the love

MBUNGE Viti Maalum, Christine Mzava, ameishauri Serikali iwashughulikie watu wanaofanya ukatili wa kijinsia, kama inavyowashughulikia watuhumiwa wa uhujumu uchumi, kwa kuwanyima dhamana mahakamani, akidai wanahujumu uhai wa watu hasa watoto wadogo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kwa mwaka wa 2022/23, leo Jumatatu, bungeni jijini Dodoma, Mzava, ameshauri sheria zibadilishwe ili kuwezesha suala hilo.

“Ningeomba waziri kama inawezekana, sheria iletwe bungeni tuweze kuirekebisha sababu kama mtu anahujumu uchumi anakuwa hana dhamana, je anayehujumu uhai wa mtu inakuwaje? Hii haikubaliki tunajenga kizazi ambacho kinakuwa na maisha magumu,” amesema Mzava.

Mzava ametoa ushauri huo akisema, mwenendo wa kesi za ukatili wa kijinsia, hasa za ubakaji na ulawiti hauridhishi kwani asilimia kubwa huishia njiani kutokana na baadhi ya watuhumiwa wanaopewa dhamana kutokomea kusikojulikana.

Amesema, kuanzia Juni 2020 hadi Desemba 2021, kulikuwa na matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watu wazima 217, ambapo 149 yalifikishwa mahakamani huku kesi zilizotolewa hukumu kati yake zilikuwa ni 80 pekee.

Kwa upande wa ukatili wa watoto, Mzava amedai, matukio 661 yaliripotiwa kwenye kipindi hicho na kuwa yaliyopelekwa mahakamani ni 149, 80 pekee ndiyo yaliyotolewa uamuzi.

“Hii haikubaliki, tatizo ni nini?Hapa kuna tatizo. Kesi zinapelekwa mahakamani na ukizingatia sheria hii wanaofanya ukatili hasa suala zima wanaobaka na wanaolawiti, inawapa dhamana wahusika, wakishapewa dhamana wanatoroka, kesi zinapotelea hewani,” amesema Mzava.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *