May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge aomba Serikali iimarishe mawasiliano Igalula

Spread the love

 

MBUNGE wa Igalula mkoani Tabora (CCM), Venant Daudi, ameiomba Serikali ipeleke mawasiliano ya simu kwenye vijiji vya jimbo hilo. Anaripoti Jemima Samwel DMC … (endelea).

Daudi alitoa ombi hilo jana tarehe 12 Mei 2021, katika kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma.

Mbunge huyo amesema, Serikali inapaswa imalize changamoto ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini, kwa kuwa ni muhimu katika kuharakisha maendeleo.

“Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mawasiliano ya simu kwenye vijiji vya Igalula, ambavyo havina mawasiliano ya simu?” amehoji Daudi.

Akijibu swali hilo, Naibu waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, David Silinde amesema, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), itavifanyia tathmini vijiji hivyo, kwa ajili ya kuchukua hatua za kuboresha huduma za mawasiliano.

David Silinde, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)

“Serikali kupitia UCSAF itavifanyia tathmini vijiji vyote, vitakavyobainika kuwa na changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano, vitaingizwa katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika zabuni, zitakazotangazwa katika siku za usoni kadri ya upatikanaji wa fedha,” alisema Silinde.

Hata hivyo, Silinde alisema Serikali imeshaanza kutatua changamoto ya mawasiliano katika jimbo hilo, ambapo hadi sasa imetekeleza miradi sita ya mawasiliano kwenye kata tano kati ya 11 za Igalula.

“Jimbo la Igalula lina Kata 11 ambapo Serikali kupitia UCSAF imetekeleza miradi 6 ya mawasiliano, katika Jimbo la Igalula ambapo imejengwa minara 6 inayotoa huduma za mawasiliano katika Kata 5, ambazo ni Kizengi, Loya (Miradi 2), Lutende, Miswaki na Tura” alisema Silinde.

Pia, Silinde alisema kata 10 kati ya 11 za Igalula zina watoa huduma za mawasiliano.

“Kata zenye watoa huduma za mawasiliano katika Jimbo la Igalula ni 10 ambazo ni Igalula, Kigwa, Loya, Lutende, Miswaki, Kizengi, Miyenze, Tura, Goweko na Nsololo,” alisema Silinde.

error: Content is protected !!