MBUNGE wa Kalambo mkoani Rukwa (CCM), Josephat Kandege, amehoji sababu za jengo la Chama cha Mapinduzi (CCM), kutumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Kalambo, kuendesha shughuli zake, kitendo kinachokosesha chama hicho mapato. Anaripoti Jemima Samwel, DMC … (endelea).
Kandege amehoji hayo leo Jumatatu, tarehe 7 Juni 2021, katika kipindi cha maswali na majibu, bungeni jijini Dodoma.
“Mahakama ya Wilaya ya Kalambo sasa hivi wanatumia jengo la CCM na hivyo sisi kama CCM, tunaona wanatunyima mapato,” amesema Kandege.
Mbunge huyo wa Kalambo, ameihoji Serikali ina mpango gani kujenga jengo la mahakama ya wilaya hiyo.
“Je, Serikali iko tayari katika mpango wa kujenga mahakama ya wilaya, ili Wilaya ya Kalambo ikapewa kipaumbele kujenga mahakama ya kisasa, yenye kulingana na hadhi ya wilaya yetu?” amesema Kandege.
Wakati huo huo, Kandege ameiomba Serikali ipeleke watumishi wa mahakama hususan mahakimu, ili wananchi wapate huduma za kisheria.

Akimjibu Kandege, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda, amesema Serikali ina mkakati wa kujenga majengo ya mahakama za wilaya nchi nzima na kuwa hadi kufikia 2026, wilaya zote zitakuwa na majengo hayo.
“Tunao mkakati kufikia 2025/26, nchi nzima katika makao makuu ya wilaya zote, zitakuwa na majengo ya mahakama. Na makao makuu ya tarafa zote nchini yatakuwa yamepata majengo, nimuombe mheshimiwa awe mvumilivu,” amesema Pinda.
Kuhusu uhaba wa watumishi wa mahakama, Pinda amesema Serikali inaifahamu changamoto hiyo, na kwamba itaongeza watumishi kadri itakavyowezekana.
“Kuhusu swali la kwanza linalohusu suala la watumishi na mahakimu, ni mpango wa mahakama kuongeza idadi ya mahakimu ili iweze kutosheleza, ingawa kwa kweli bado tatizo ni kubwa la watumishi katika sekta mbalimbali nchini,” amesema Pinda.
Leave a comment