Sunday , 28 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mbowe alinigomea kukutana na Magufuli – Job Ndugai
Habari za Siasa

Mbowe alinigomea kukutana na Magufuli – Job Ndugai

Spread the love

 

ALIYEKUWA Spika wa Bunge, Job Ndugai, amedai kuwa aliwahi kumshauri Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kukutana na Rais John Pombe Magufuli, ili kuzungumza mustakabali wa nchi. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza leo Alhamisi, wilayani Kongwa, mkoani Dodoma, wakati wa mazishi ya Chibiriti Chiuyo, kada maarufu wa Chadema mkoani humo, Ndugai alisema, “niliwahi kumshauri mheshimiwa Mbowe, wakati akiwa mbunge wa Hai (Kilimanjaro), nami nikiwa spika wake, kwamba akutane na aliyekuwa rais wa Tanzania. Lakini alinikatalia.”

Ndugai ni mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika jimbo la uchaguzi la Kongwa, ambako mwili wa marehemu Chiuyo unatarajiwa kuhifadhiwa.

Wakati wa uhai wake, Chiuyo alikuwa miongoni mwa waasisi wa Chadema mkoani Dodoma na wilyani kwake Kongwa; akitoa mchango mkubwa wa kueneza na kukilinda chama hicho katika maeneo hayo.

Alifariki dunia juzi na mazishi yake yanafanyika mchana wa leo.

Akimnukuu Mbowe, ambaye alikuwa pia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya upinzani bungeni, Ndugai alisema, “yule bwana aliniambia jambo hilo haliwezekani.”

Alisema, “nilipomuuliza Mbowe kwa nini haiwezekani?” Ndugai anasema, mwanasiasa huyo alijibu, “unawafahamu wale watu wangu. Hawatanielewa.”

Akiongea kwa kujiamini, Ndugai alisema, “siku moja, Mbowe akiwa mbunge, nilimuita ofisini kwangu. Nikamwambia, hivi kwa nini wewe usikae na rais aliyekuwapo (Magufuli). Wakazungumza baadhi ya haya mambo; si yatapungua.

“Kama kuna tatizo kubwa, mimi niko tayari kufanya mpango. Mkakutana na rais na mkazungumza. Akaniambia haiwezekani. Kwa nini haiwezekani?

Akasema, “wenzangu watanielewaje? Si unajua hawa jamaa zangu? Watanielewa vipi

Aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai

Ndugai anasema, “lakini nikamwambia ukiwa kama kiongozi, hupaswi kuwa ndani ya boki, wewe na wafuasi wako wote. Lazima wewe kama kiongozi, lazima utoe kichwa nje; uwe unaangalia huko. Ukirudi ndani ya boki, unawaambia wenzio.

“Mkikaa wote ndani ya boki, hamtajua yanayoendelea huko nje. Akaniambi wapi! Hilo unalonishauri siyo kabisa.”

Akaongeza, “nashukuru leo hii, katoa kichwa nje ya boki.”

Hata hivyo, Ndugai anayejitapa kuwa alimshauri Mbowe kukutana na Magufuli, ndiye aliyemvua ubunge aliyekuwa mbunge wa Chadema, katika jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu, katikati ya kuugulia majeraha ya risasi, aliyoshambuliwa akiwa bungeni mjini Dodoma.

Lissu alishambuliwa na wanaoitwa na serikali, “watu wasiojulikana,” nje ya nyumba yake, Area D, mjini Dodoma, tarehe   7   Septemba   2018.

Mara baada ya shambulio hilo, mwanasiasa huyo mashuhuri wa upinzani nchini, alikimbizwa nchini Kenya kwa matibabu na baadaye   nchini   Ubelgiji.

Ndugai alitangaza uamuzi wa kumvua Lissu ubunge wake, aliyoupata kwa jasho na damu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, tarehe 28 Juni 2019.

Aliuambiwa mkutano wa Bunge wa jioni ya siku hiyo, kwamba amechukua uamuzi huo, kufuatia Lissu kutoonekana bungeni kwa   muda   mrefu   bila   yeye   kuwa   na   taarifa   ya maandishi;   na   kutojaza   fomu   ya   tamko   la   mali   na madeni.

Akiongea   kwa   hisia   kali,  Spika   Ndugai   alisema,“Septemba   2017,   kwa   sababu   ambazo   zinafahamika kwa kila mtu, mbunge wa Singida Mashariki, aliondoka hapa nchini kwa ajili ya matibabu nchini Kenya.

“Kufanya hadithi iwe fupi, mtakumbuka zaidi ya mwaka mmoja   amekuwa   akionekana   kwenye   vyombo   vya habari   vya   kitaifa   na   kimataifa   akifanya   mihadhara mbalimbali.

“Lakini   kwa   muda   wote   huo,  hajafika   bungeni   na hajawahi   kuleta   taarifa   yeyote   ile   kwa   Spika   kuhusu mahali   alipo   na   anaendeleaje;   wala   hajawahi   kuleta taarifa kupitia kwa uongozi wake wa kambi au uongozi wa Bunge.” 

Kufuatia hali hiyo, Ndugai alisema, Katiba ya nchi ipo wazi katika mambo ya aina hiyo, na pkwamba baadhi ya wabunge   wameshapata   matatizo   kutokana   na   utoro kama huo wa Lissu.

 

Aliongeza,   “…wa   (utoro)   kushindwa   hata   kuwambia Spika niko mahala fulani naendelea na jambo fulani hivi hakuna   chochote,   yaani   kama   kumdis-regard   Spika kama hakuna chochote.

“Jambo   la   pili, wabunge   wanatakiwa   kujaza   taarifa zenye   maelezo   ya   mali   na   madeni   kama   Katiba inavyotaka.   Tunatakiwa   tujaze   fomu   mbili,  na   nakala inabaki kwa Spika.”

Alisema, “baada ya kuona kwenye kumbukumbu zangu hakuna   fomu   za   Lissu,  nilichukua   jukumu   la   kupata uhakika   wa   jambo   hili   kwa   Kamishena   wa   Tume   ya Maadili   na   nilijibiwa   kwa   barua   kwamba   Lissu hajawasilisha na hawana taarifa zozote.”

Spika Ndugai alisema, kwa maana hiyo, Lissu hakuwa amejaa   fomu   na   kwamba   katika   mazingira   hayo, kifungu   cha   37   kifungu   kidogo   cha   3   cha   Sheria   ya Uchaguzi   kinamtaka   kumtaarifu   mwenyekiti   wa   NEC kuhusu suala hilo.

“Napenda   kuwafahamisha   kuwa   nimemwandikia mwenyekiti   wa   Tume   ya   Taifa   ya   Uchaguzi   kwamba jimbo la Singida Mashariki lipo wazi, alijaze kwa mujibu wa sheria zetu.

Nimefanya hivyo kwa sababu hizo mbili– kushindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge kwa muda mrefu bila kutoa taarifa kwa Spika na kutotoa taarifa za mahali alipo na kugoma kutoa tamko la mali na madeni kama ibara ya 71 (1g) inavyotaka,” alieleza Ndugai.

Ni Job Ndugai huyo huyo, anayedai kumshawishi Mbowe kukutana na Magufuli, aliyewasakama wabunge kadhaa wa upinzani wakati wa uongozi wake, ikiwamo kuridhia uamuzi wa Prof. Ibrahim Lipumba wa kuwavua ubunge wabunge 8 kutoka Chama cha Wananchi (CUF), kinyume na taratibu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Sauti ya Watanzania waeleza sababu za kuiunga mkono Chadema

Spread the love  KIKUNDI kinachojipambanua katika kupigania rasilimali na uhuru wa nchi,...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Tanzania, Somalia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Somalia...

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

error: Content is protected !!