Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Makunga: Tangulia Mzindakaya, shuhuda mwenza wa Kifo cha Sokoine
Makala & Uchambuzi

Makunga: Tangulia Mzindakaya, shuhuda mwenza wa Kifo cha Sokoine

Hayati Dk. Chrisant Mzindakaya
Spread the love

 

ILIKUWA siku ya Alhamisi tarehe 12 Aprili 1984, mimi nikiwa na Mwandishi mwanafunzi mwenzangu aitwaye Mosoeu Magalefa raia wa Afrika Kusini tuliyekuwa tunasoma naye Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania, tuliwasili ofisi ya mkuu wa mkoa wa Morogoro kwa mahojiano na Chrisant Majiyatanga Mzindakaya. Anaandika Mwandishi Maalum … (endelea).

Kwa mfumo wa mafunzo ya uandishi wa habari wa chuo hicho wakati huo, kumaliza mwaka wa kwanza wa mafunzo hayo lazima wanafunzi wakafanye mafunzo kwa vitendo katika vyombo vya habari. Mimi na mwenzangu Magalefa, tulipangiwa Kituo cha Morogoro cha Shirika la Habari Tanzania (Shihata).

Siku hiyo tulikuwa na mihadi ya mahojiano na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mzee Mzindakaya saa 3.30 asubuhi nasi tuliwasili hapo saa 3.00 asubuhi tayari kwa mahojiano hayo.

Tulipofika kwenye Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, kwa wale wanaoifahamu ofisi hiyo, ukitaka kuingia kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa, lazima upitie ngazi zilizo nje ya jengo hilo la ghorofa moja.

Wakati tunataka kuanza kupanda ngazi hizo, tukamwona mwenyeji wetu ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wakati huo, Mzee Mzindakaya akishuka kwa kasi kwenye ngazi hizo, na kwa sababu ya kasi ile tulimpisha naye akashuka hadi kwenye eneo la kuegeshea magari.

Sisi tulipigwa na mashangao sana kuona mwenyeji wetu anatupita pamoja ya kuwa alijua tuna mihadi naye kwa sababu mihadi hiyo tuliipanga kwenye gari lake, wakati tunarudi kutoka kwenye mahafali ya shule ya Sekondari ya Mzumbe wiki iliyotangulia.

Rais Samia Suluhu Hassan akiaga mwili wa mwanasiasa mkongwe, Chrisant Majiyatanga Mzindakaya

Mzee Mzindakaya alikwenda moja kwa moja hadi kwenye maegesho ya magari, bahati mbaya gari lake halikuwako hapo, akaliona gari la polisi aina ya Peugeot 404, ambayo wakati huo yalijulikana sana kama 999.

Mzee Mzindakaya akasikika akiita dereva wa gari lile kisha dereva akajitokeza na akamwamuru aingie kwenye gari kuna dharura. Yule dereva akawaita madereva wenzake walisukume lile gari kwani haliwezi kuwaka bila ya kusukumwa.

Yule dereva akaingia kwenye gari huku Mzee Mzindakaya akiwemo ndani, wale madereva wengine walilisukuma kisha likawaka na wakaondoka mahali hapo.

Sisi kuona hivyo, tukapanda ngazi kuelekea kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa kujua kumetokea nini kutoka kwa Katibu Muhtasi wake. Kufika hapo tukamwona naye akiduwaa kwa kilichotokea.

Tukamwuliza, vipi tulikuwa na mihadi na Mzee Mzindakaya, lakini badala yake tukamkuta akishuka kwenye ngazi kwa kasi bila hata ya kutusalimu wakati anajua tuna mihadi naye?.

Katibu Muthasi alitujibu kuwa hata yeye hajui nini kilichotokea ila alipokea simu ambayo mpigaji alitaka kuzungumza na Mkuu wa Mkoa naye alipomuunganisha naye na baada ya dakika chache akamwona Mzee Mzindakaya akitoka mkuku kutoka ofisini kwake na kuanza kushuka kwenye ngazi.

Kuona hivyo tukatoka nje ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kushuka kwenye ngazi, kufika tu karibu na eneo la maegesho ya magari, mara tukaliona gari la Mkuu wa Mkoa likifika maeneo ya maegesho ya magari.

Tukamwona dereva naye kwa kuwa wiki iliyotangulia tulikuwa naye kwenye safari ile ya kwenye mahafali Sekondari ya Mzumbe, anatufahamu nasi tunamfahamu, nikamwambia bosi wako (Mzee Mzindakaya) amepanda gari la polisi anakoelekea hatupajui.

Hayati Chrisant Mzindakaya

Dereva akatujibu ndiyo, ameliona gari hilo alipokuwa akitoka kujaza mafuta, mimi nikamweleza gari lenye bovu, limetoka hapo kwa kusukumwa kwa hiyo likizima huko linakokwenda itakuwa kasheshe kwa bosi wake.

Nikamshauri tumfuate kwa kuwa ni rahisi kuliulizia limeelekea wapi kwa jinsi ilivyo gari lenye ambalo lina kimulimuli. Dereva akakubali nasi tukaingia kwenye gari hilo na hao tunaanza safari ya kumsaka Mzee Mzindakaya alikoelekea.

Dereva akapiga mguu, kwa wale wanaoifahamu ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ilipo, iko kwenye mteremko kama unaelekea mjini, tulipokaribia round about ya iliyokuwa stendi ya mabasi toka mikoani ambayo sasa ni stendi ya daladala, inapoishia barabara ya Boma, tukaliona lile gari alilopanda Mzee Mzindakaya linapinda kona kuelekea hospitali ya mkoa wa Morogoro.

Dereva akasikika akisema lile pale, baada ya muda tukawa nyuma ya gari lile alilopanda Mzee Mzindakaya na tulipofika karibu na hospitali ya Mkoa wa Morogoro tukaliona linapinda kuingia eneo la hospitali nasi tukapinda kulifuata gari lile.

Magari yote yalisimama Mzee Mzindakaya akashuka nasi tukashuka akatuona akatabasamu kisha akamwambia yule dereva wa gari la polisi kurudi ofisini kwani gari lake limefika.

Pembeni mwa sehemu yaliposimama magari, kulikuwa na Daktari wa Mkoa wa Morogoro wakati huo akiwa na daktari mwingine ambao walionekana walikuwa wanamsubiri Mkuu wa Mkoa.

Mganga Mkuu akamsogelea Mzee Mzindakaya nasi, mimi pamoja na mwandishi mwanafunzi mwenzangu kutoka Afrika Kusini, tukiwa nyuma ya mkuu wa mkoa, na kisha akamwambaia kuwa, Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine, alipata ajali eneo la Wami Dakawa akitokea Dodoma na amekufa.

Mzee Mzindakaya huku akipigwa na butwaa, aliuliza yuko wapi, Mganga Mkuu wa Mkoa akamjibu yuko chumba cha maiti. Mzee Mzindakaya akaamuru twende tukamwone.

Kufika kwenye chumba cha maiti, tulikuwa watu sita, madaktari wawili muhudumu wa chumba cha maiti, mzee Mzindakaya, mimi na yule mwandishi mwanafunzi mwenzangu kutoka Afrika Kusini. Kwa maanahiyo mbali na madaktari na muhudumu wa chumba cha maiti, sisi tulikuwa watu watatu wa kwanza kuona mwili ya marehemu Sokoine.

Yule mhudumu wa chumba cha Maiti akafungua mlango tukaingia ndani, akafungua kabati mojawapo akalivuta tukamwona marehemu akiwa amefungwa bandeji mithili ya msalaba.

Bandeji moja ilitoka shingoni nyuma ya kichwa, ikapita kichwani na kushuka kufunika pua na mdomo kisha kushuka kifuani. Nyingine ikatoka upande mmoja wa sikio na kufunika mdomo na kwenda hadi kwenye sikio jingine na kuzunguka nyuma ya kichwa hadi kwenye sikio jingine.

Baada ya kimya kirefu huku tukipigwa na bumbuwazi, Mzee Mzindakaya akasema inatosha na tukaondoka hapo kwenye chumba cha maiti na kurejea kwenye ofisi ya Mganga mkuu wa mkoa.

Hayati Chrisant Mzindakaya

Kwa waandishi wa habari, fikiria jinsi mimi nilivyokuwa, mwandishi mwanafunzi unakumbana na stori ya aina hiyo, unaiandikaje sasa. Tangu pale nilianza kufikiri nianzie wapi.

Unaweza kusema si ukaripoti kwa mwandishi mkuu wa Shihata wa mkoa akusaidie kuandika intro, aliyekuwa Mwandishi wa Shihata Mkoa wa Morogoro wakati ule Richard Semwaiko, alinikabidhi ofisi kupata nafasi ya kuwa na mkewe ambaye alikuwa anapata operesheni siku hiyo ya Alhamisi Aprili 12.

Taharuki haikuwa kwa upande wangu pekee, hata Mzee Mzindakaya naye alikuwa na taharuki. Hakutaka kutuachia sisi tuwe mbali naye na kila alichokuwa anataka kukifanya alituomba ushauri.

Mimi nikamwambia nataka kwenda ofisini nikaandike stori je naweza kukutumia wewe kuwa chanzo cha habari. Mzee Mzindakaya akaruka na kuniambia yeye hawezi kuwa chanzo cha habari ile. Nikaduwaa.

Kisha akatuomba tuondoke pale hospitali twende naye hadi ofisini kwake, tukaondoka, kabla ya kufika ofisini kwake akaamua twende nyumbani kwake akatoe taarifa kwa Rais Mwalimu Julius Nyerere.

Huku tukiwa nyumbani kwake, Mzee Mzindakaya akawa anapiga simu, ikumbukwe kuwa wakati huo simu zilikuwa za kunyonga. Akapiga simu ile ikawa inaita upande wa pili, kwa sababu ya ukimya uliotanda katika chumba kile, hata sisi tulikuwa tunamsikia yule wa upande wa pili.

Mzee Mzindakaya akajitambulisha kwa huyo wa upande wa pili nasi tukasikia sauti ikijibu amsaidie nini. Mzee Mzindakaya alijibu anataka kuzungumza na Mwalimu Nyerere.

Akaunganishwa na kisha tukamsikia mzee Mzindakaya akijitambulisha kwa Mwalimu, mimi ni Chrisant Mzindakaya.

Mwalimu alisikika akisema vipi Chrisant…Mzee Mzindakaya akajibu nina taarifa ambayo siyo nzuri nakata kukueleza.

Mwalimu akajibu ipi hiyo Chrisant…Mzee Mzindakaya akamwambia, Waziri Mkuu Sokoine alikuwa anasafiri kutoka Dodoma asubuhi hii kufika Wami Dakawa alipata ajali…amekufa.

Mwalimu akasikika kwenye simu akihoji nini…kisha simu ikawa kimya Mzee Mzindakaya alipotaka kuendelea kuelezea simu ilikuwa imekatika.

Mzee Mzindakaya akaanza tena kuikorogo simu ili amalizie maelezo yake, na baada ya jitihada ya kukorogo simu yake akaipata tena na aliyepokea ambaye ndiye aliyemuunganisha na Mwalimu mwanzo, akamweleza kuwa Mwalimu ametoka mara baada ya kuzungumza naye amekwenda nyumbani Msasani.

Kisha baada ya mazungumzo na Mzee Mzindakaya, kwa shingo upande alituruhusu sisi twende ofisifi Shihata kutoa taarifa ya Kifo cha Waziri Mkuu Sokoine. Alitupa sharti la kurudi pale nyumbani kwake mara baada ya kutoa taarifa Shihata Makao Makuu.

Hata hivyo, alituonya kuwa taarifa ya tukio hilo itatolewa na Ikulu na kwamba yeye kwa namna yoyote ile asitajwe kuwa chanzo cha habari ile. Ili kuhakikisha kuwa tunarudi pale alitupa gari lake litupeleke Ofisini Shihata na kuturudisha tena pale.

Tulipofika Ofisini, mimi ambaye wakati huo ndiye nilikuwa kaimu Mwandiishi Mkuu wa Shihata wa Mkoa, nikapiga simu Shihata Makao makuu Dar es Salaam. Simu Ikapokewa na Mhariri wa Habari wa Shihata.

Nikajitambulisha, Mimi naitwa Theophil Makunga, Mwandishi Mwanafunzi, niko hapa Morogoro kwenye mafunzo naomba kuzungumza na Mkurugenzi wa Shihata. Yule Mhariri wa Habari alinijibu,…wewe mwanafunzi tu unataka kumweleza nini mkurugenzi.

Nikamsihi na kumwomba aniunganishe na Mkurugenzi nina jambo la kuzungumza naye. Baadaye alikubali akaniunganisha na Mkurugenzi wa Shihata wakati huo alikuwa marehemu Nkwabi Ngwanakilala.

Mkurugenzi alinipokea nami nikajitambulisha kuwa ni Mwandishi Mwanafunzi ninayesoma Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania (TSJ) jana nilikabidhiwa ofisi na Mzee Semwaiko ambaye yuko huko Dar es Salaam.

Mkurugenzi akaniambia kuwa anafahamu kuwa Semwaiko yuko Dar kwa matibabu ya mke wake, je kuna nini? Nikamwambia kuwa nina taarifa ya msiba wa waziri mkuu Sokoine lakini mkuu wa mkoa wa Morogoro hayuko tayari kuwa chanzo cha habari hiyo.

Mkurugenzi Ngwanakilala akaniuliza maswali ya kiuhariri kuthibitisha kama hicho nilichosema nina uhakika nacho.

Aliniuliza nina uhakika gani kama Waziri Mkuu amekufa. Nikamwambia nilikuwa pamoja na mkuu wa Mkoa alipokwenda kuthibitisha kifo cha Sokoine katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Morogoro.

Nikazidi kumweleza kuwa nia yangu ya kumpa taarifa ni kuwaweka tayari waandishi kwani wakati wowote wanaweza kuitwa Ikulu kwa ajili ya Rais kutoa tamko la kifo cha Waziri Mkuu. Mzee Ngwanakilala alinishukuru.

Kisha nilielezwa kuwa alikwenda chumba cha habari na kuitisha mkutano wa waandishi na wapiga picha wote waliokuwapo ofisini hapo kuwapa taarifa hiyo na kujiandaa.

Mmojawapo kati ya walioitwa ni yule Mhariri wa Habari wa Shihata ambaye alinikejeli nilipomweleza nataka kuzungumza na Mkurugenzi.

Theophil Makunga

Baada ya muda mfupi nikiwa bado ofisini Shihata Morogoro, nikasikia simu ikiita na baada ya kuipokea yule Mhariri wa habari akaniuliza kama mimi ni Makunga, nikamwambia ndiye, akaniomna radhi kwa maneno ya kejeli na kweli ile taarifa ilikuwa apewe Mkurugenzi pekee.

Baadaye alasiri siku hiyo Mwalimu alitoa tamko la kifo cha Edward Moringe Sokoine. Tangulia Mzee Mzindakaya, shuhuda mwenza wa kifo cha Sokoine, tangulia baba.

Mwandishi wa Makala hii ni; Theophil Makunga, Mwandishi mkongwe nchini Tanzania aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

1 Comment

  • Asante kwa kutupa ushuhuda wako licha ya kwamba ni kumbukumbu mbaya lakini wewe ni sehemu ya historia hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!