KIPYENGA cha uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kimepulizwa rasmi. Anaandika Mwandishi Maalum … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa ya tarehe 6 Juni 2021, iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi ya shirikisho hilo, Kiomoni Kibamba, ni kwamba uchaguzi wa chama hicho, utafanyika jijini Tanga, 8 Agosti 2021.
Mkutano huo mkuu wa TFF, pamoja na mambo mengine, utachagua viongozi wakuu wa chombo hicho akiwepo rais wake na wajumbe sita wa Kamati ya Utendaji.
Kwa mujibu wa katiba ya sasa, wajumbe wa kuchanguliwa wa Kamati ya Utendaji, wamepunguzwa kutoka 13 hadi sita. Viongozi watakaochaguliwa katika mkutano huo, wataruhusiwa kuongoza TFF kwa muda wa miaka minne ijayo.
Baada ya uchaguzi wa wajumbe hao sita wa Kamati Tendaji, rais atakayechaguliwa atateua wajumbe wengine wanne, akiwamo mwanamke mmoja.
Huu ndio uchaguzi pekee utakaokuwa rahisi kwa Rais wa sasa, Wallace John Karia, kuibuka mshindi. Hii ni kwa sababu, una sura ya demokrasia kwamba ni huru, lakini ndani yake, umefinyanga haki.

Na kwa kutazama mazingira halisi, uchaguzi huo tayari umeshafanyika. Kilichobaki ni kutumia mbinu zile zile chafu, kumthibitisha Karia kuwa rais kwa kipindi kingine.
Mazingira ya kumfanya Karia kuendelea na wadhifa wake wa urais, yalianza kuonekana mapema, kufuatia hatua yake ya kuwashughulikia kila aliyeonyesha dhamira ya kumpinga. Amewatafutia sababu za kuwafungia kushiriki soka.
Ukitazama mikoani asilimia kubwa ambao walikuwa hawao na Karia amewashughulikia. Mifano halisi ni Songwe, ambako mwenyekiti wake amefungiwa miaka mitatu na Mbeya, Elias Mwanjala, naye amefungiwa miaka mitatu.
Akatumia kamati ya maadili, akamfungia David Mwakalebela kwa muda wa miaka mitano.
Haitoshi kwa sasa, Karia yupo mikoani. Anakutana na viongozi mbalimbali ambao ni wajumbe kwenye uchaguzi huo. Kinachofanyika huko, hakuna anayekijua.
Wakati haya yakiendelea, tumeona taarifa ya TFF inayotaja sifa za mtu mwenye uwezo wa kuwania nafasi ya urais. Ni sharti mgombea awe na shahada.
Kama hiyo ni kweli, basi ni uoga ule ule wa kuendelea kutengeneza mazingira ya uchaguzi huru, lakini usio na haki. Unasemaje mgombea awe shahada?
Katika nchi na mabara mengine ambako mpira wa miguu umepiga hatua kubwa, ikiwamo UEFA, hawana ukiritimba wa elimu.
Viongozi wanaoongoza vyama vya soka wamekuwa hasa wachezaji wa zamani wa soka ambao hawakupata muda wa kutafuta shahada za taaluma nyingine, lakini wamekuwa wakiongoza vizuri sana.
Mazingira mengine ambayo Karia amejitengenezea, kupunguza idadi ya Kanda na wapiga kura katika mkutano mkuu. Katika uongozi wake, kumefutwa kanda kutoka 13 hadi sita. Hii maana yake, ni kwamba kanda saba zimeondolewa.
Hayo aliyafanya mwaka 2019 ambako katiba ya TFF ilifanyiwa mabadiliko mara mbili ndani ya mwaka mmoja.
Kwa mfano, kanda namba 13, ilikuwa inaundwa na mkoa wa Dar es Salaam pekee yake. Lakini sasa, imeunganishwa na mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi na Mtwara.
Kabla ya mabadiliko haya, Lindi na Mtwara, walikuwa wanaunda kanda namba tisa, huku Pwani na Morogoro, wakiwa namba 11.
Kanda namba mbili, sasa inaundwa na mikoa mitano, ambayo ni Ruvuma, Njombe, Mbeya, Songwe na Iringa. Kabla ya mabadiliko hayo, Njombe na Ruvuma, zilikuwa zinaunda kanda moja, iliyopewa jina la kanda namba nane.
Nayo Iringa, Mbeya, wakati huo Songwe, ilikuwa sehemu ya mkoa wa Mbeya, iliunda kanda namba sana.
Karia ameichukua mikoa minne ya Manyara, Arusha, Tanga na Kilimanjaro, kuifanya kanda moja ambayo ni kanda namba tatu.
Kabla ya mabadiliko hayo, Manyara na Arusha, zilikuwa zinaunda kanda namba nne, huku Tanga na Kilimanjaro, walikuwa wanaunda kanda namba 12.
Kanda nyingine alizounda Karia, ni Dodoma, Singida, Simiyu na Shinyanga, ameifanya kanda moja kuwa kanda namba nne. Kabla ya hapo, Dodoma na Singida, ziliunda kanda namba 10 na Simiyu na Shinyanga, zilikuwa kanda namba tatu.
Aidha, kuna kanda ya Kagera, ambayo ina mikoa ya Geita, Mwanza na Mara. Kabla ya hapo, Kagera na Geita, huku Mwanza na Mara, wakiwa wanaunda kanda namba mbili.
Kanda nyingine, ni Kigoma na Tabora, ambayo sasa ameunganisha na mikoa ya Katavi na Rukwa, ambayo ni kanda namba sita.
Kuhusu wajumbe wanne, watakaoteuliwa na Karia, nini maana yake? Ni kwamba anataka kutawala TFF bila upinzani.
Kwamba atakuwa na wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanne ambao kwa vyovyote vile, watakuwa ‘royal’ kwake, na hivyo kuweza kuwatawala atakavyo.
Vilevile, katika mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2019, Karia na timu yake walifyeka idadi ya wapiga kura kutoka 129 hadi 83 ambao kwa sasa, ana uwezo wa ‘kuwakontro.’
Kwamba, kila mgombea urais, anapaswa kuwa kudhaminiwa na viongozi watano wanaotoka kanda tofauti. Kila kiongozi anaruhusiwa kudhamini mgombea mmoja. Akishafanya hivyo, anapaswa kuwataarifa wenzake, kwamba tayari amedhamini.
Ikitokea mgombea mwingine anakwenda katika mkoa mwingine ambao kanda yake kuna kiongozi alidhamini, hilo haliwezekani.
Hivyo utaona kwamba Karia akinasa kanda tano, kati ya sita, basi atakuwa ameacha kanda moja.
Tayari wanaogombea nafasi ya urais mpaka juzi wmefikia watano akiwamo Karia. Bila kupepesa macho, wagombea wengine wote, waweza kuwa wasindikizaji.
Ibara ya 26 ya Katiba hiyo, inataja wapiga kura wawili kutoka kila mkoa, yaani mwenyekiti na mjumbe wa mkutano mkuu. Kwa mikoa 26 ya Tanzania Bara, kutakuwa na wapigakura 52. Hapo katibu mkuu wa chama cha soka mkoa, ameshapigwa panga.
Kwa upande wa vilabu vya Ligi Kuu Tanzania Bara, ni mwenyekiti pekee anayeruhisiwa kupiga kura. Maana yake, kutakuwa na kura 16. Msimu ujao wa Ligi Kuu utakuwa na timu 16 tu za Ligi Kuu.
Vyama shiriki vya TFF ni kama vifuatavyo: Chama cha Soka Wanawake (TWFA); Chama cha wachezaji wa mpira wa miguu (Sputanza); Chama cha Waamuzi (Frat); Chama cha Makocha (Tafca) na Chama cha Madaktari wa Tiba za Wanamichezo Tanzania (Tasma).
Kila chama kitatoa wajumbe watatu ambao ni mwenyekiti, katibu na mjumbe wa mkutano mkuu hivyo, ukichukua 3 ukazidisha kwa vyama vitano unapata wajumbe 15 kutoka vyama shiriki vya TFF.
Ukichukua 52+16+15 unapata jumla ya wapiga kura 83. Swali, kama vyama shiriki umeacha wapigakura watatu, iweje mikoa ufute mpiga kura mmoja?
Mazingira haya yote yanaashiria vielelezo vya Karia kuendelea kuifinyanga demokrasia na kujihalalishia utawala wa kudumu.
Ni kweli Karia kwa kipindi chake tumeona mapinduzi makubwa ya soka, ijapokuwa pia kwa kipindi chake, kumeibuka tuhuma kubwa za rushwa kwenye uendeshaji wa soka.
Sasa kwa kuwa alishajua ameharibu, ndiyo maana alianza kutengeneza mazingira ya kushinda.
Ili walau kwa asilimia 50 uchaguzi ukaribu kuwa huru na haki, basi inahitajika kuwe na Tume huru ya Uchaguzi ambayo haibebwi na Karia.
Lakini nje na hapo ni kuendelea kuibeba demokrasia kwenye fuko lililotobokatoboka huku tukiamini tupo salama. Hakuna usalama kwenye demokrasia inayoamuliwa na mtu anayewania nafasi hiyo hiyo.
Serikali ambayo ndiyo walezi wa vyombo hivi wanaweza kuliangalia hili. Mapendekezo yangu ni kuwa ili Karia asiwe Rais labda jina lake liondolewe kwa nguvu na serikali kutoka kwenye orodha ya wagombea. Kinyume cha hapo, ni kuichezea kwata demokrasia.
Yapo manung’uniko mengi juu ya uongozi wa Karia kama ulivyokuwa wa Jamal Malinzi. Wachambuzi wengi wanasema, Karia na Malinzi wote viatu vya Leodegar Tenga vimewapwaya ijapo vipindi vyao vimekuwa na fedha nyingi.
Lakini lingine ni kwamba TFF ni shirikisho la mpira wa miguu la Tanzania Bara, ingawa kinajiita – Shirikisho la Soka Tanzania (Tanzania Football Federation -TFF).
Kwamba, TFF siyo chombo cha Muungano, lakini chenyewe kinajipa mamlaka ya kusimamia masuala ya Zanzibar kwenye shirikisho la mpira wa miguu ulimwenguni (FIFA).
Pamoja na TFF kuwa si chombo cha Muungano, lakini hakuna chombo kinachosimamia michezo ndani ya Jamhuri ya Muungano.
Kwamba pamoja na kutokuwapo kwa chombo hizo, Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), si mwanachama wa TFF.
Hii yaweza kumsabishia mgombea urais wa TFF anayetokea Zanzibar – kama atajitokeza kuwania nafasi hiyo, kutopata fursa ya kugombea; na au kupigiwa kura na watu ambao hawamhusu.
Leave a comment