July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Baregu afariki dunia

Marehemu Profesa Mwesiga Baregu

Spread the love

 

MWANAZUONI na mwanasiasa mahiri nchini Tanzania, Prof. Mwesiga Baregu, amefariki dunia, usiku wa kuamkia leo Jumapili, tarehe 13 Juni, 2021, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikokuwa akipatiwa matibabu. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa zilizothibitishwa na mmoja wa wanafamilia yake zinasema, Prof. Baregu amekutwa na mauti, alfajiri ya leo. Mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwake, Kunduchi, mkoani Dar es Salaam.

Katika kipindi cha uhai wake, Prof. Baregu, alikuwa mhadhiri katika chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Idara ya Sayansi ya Siasa.

Aidha, Prof. Baregu aliwahi kuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mwaka 1995 hadi 1997, Prof. Baregu alikuwa mwanachama na mshauri wa Augustino Lyatonga Mrema, wakati mwanasiasa huyo alipokuwa mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano.

Prof. Baregu alijiondoa kwenye kazi ya kumshauri Mrema, baada ya kujiridhisha kuwa aliyepewa kazi ya kumshauri, “ana washauri wengine, wanaofanya kazi ileile.”

Kwa takribani miaka miwili sasa, Prof. Baregu amekuwa mgonjwa. Alipata maradhi ya kiharusi mara mbili na kutibiwa katika hospitali hiyo na maeneo mengine mbalimbali. Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi – Amin.

error: Content is protected !!