Tuesday , 30 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Makonda aungana na wanaomgwaya Lissu
Habari za SiasaTangulizi

Makonda aungana na wanaomgwaya Lissu

Spread the love

MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amedai kuwa mwanasiasa mashuhuri nchini kwa sasa, Tundu Lissu, asijadiliwe kwa kuwa hajaweza kupona majeraha ya risasi aliyonayo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumza na chombo kimoja cha habari hapa nchini Makonda amesema, Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki, hajapona kwa hivyo hana kumbukumbu nzuri.

Amesema, “nawasihi wanasiasa, vyama vya siasa, hasa chama changu CCM (Chama Cha Mapinduzi) na Watanzania wazalendo, kuacha kumjadili na kumlaumu Lissu kwa sababu yoyote ile kwa kuwa ameshathibitisha bado hajapona vizuri.” 

Ameongeza, “kama mgonjwa hajapona, ni wazi kuwa hawezi kukumbuka chochote, hawezi kurudi nchini kuwashukuru Watanzania na wananchi wake waliokuwa wakimwombea na kumtolea mchango.”

Lissu ambaye kwa sasa yuko nchini Marekani alikokwenda kwa mwaliko maalum uliolenga kutaka kufahamu kwa undani kilichompata, jinsi alivyotibiwa na hali iliyo nchini, amekuwa akiituhumu serikali ya Rais John Magufuli, kuhusika na shambulio dhidi yake.

Miongoni mwa maofisa wa serikali anaotaja kuwa walikuwa nyuma ya shambulio dhidi yake, amemtaja kuwa ni pamoja na Makonda.

Mwanasiasa huyo ambaye pia amepata kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alishambuliwa kwa risasi nje ya nyumba yake, eneo la Area D, mjini Dodoma na wanaoitwa na serikali “watu wasiofahamika.”

Mara baada ya shambulio hilo, Lissu alipata matibabu katika hospitali ya mkoa wa Dodoma na kabla ya kufikishwa kwenye hospitali ya Chuo Kikuu cha Luvein, mchini Ubelgiji, alipatiwa matibabu Nairobi nchini Kenya.

Lissu alikwenda Ubelgiji, tarehe 6 Januari mwaka jana kwa msaada kutoka kwa marafiki zake wa karibu wa ndani nan je ya nchi.

Shambulio dhidi ya Lissu lilitokea tarehe 7 Septemba 2017, muda mfupi baada ya kushiriki mkutano wa Bunge wa asubuhi na kulihutubia Bunge.

Lakini Makonda anasema, “siridhishwi na mjadala unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini kuhusu Lissu,” ameeleza Makonda na kuongeza, “…Lissu hakumbuki chochote kama alichangiwa na akapatiwa matibabu mjini Dodoma. Hawezi kukumbuka hata maombi aliyofanyiwa na viongozi wa dini.”

Makonda ametoa wito wa kuacha kumjadili Lissu na kwamba hawapaswi kufanya hivyo kwa kuwa hana anachokumbuka kuhusu kilichomkuta na badala yake waendelee kumwombea arudi katika hali yake ya kawaida.

“Wanasiasa na jamii wahoji utekelezaji wa miradi kama hii ya maendeleo badala ya kuendelea kupigia kelele suala Lissu ambaye bado yupo nje ya nchi kwa matibabu,” ameeleza.

Kauli ya Makonda imekuja wakati viongozi wa Bunge, Serikali na CCM wamekuwa wakimjadili na kumtuhumu Mnadhimu huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kufuatia uamuzi wake wa kuzunguuka Ulaya na Marekani, kuzungumza na vyombo vya habari na kuituhumu serikali.

Hivi karibuni akiwa Kilosa, mkoani Morogoro, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiri Ally, alidai kuwa “Lissu hafahamu shida za wananchi ndio maana anaichafua serikali kimataifa.”

Alisema, “yupo msomi mmoja anaitwa Tundu Lissu ameugua ugonjwa wa deko, anadeka hajui jembe kwa maisha yake, hajui mpunga unalimwaje wala samaki wanavuliwaje.

“Hajapanda bodaboda muda mrefu na watoto wake hawasomi shule hizi. Anazunguka dunia nzima kutuchafua. Tunao Tundu Lissu wengi serikalini. Tumewaamini. Tumewapa dhamana ila ukiwatembelea ofisini wanadeka.”

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alinukuliwa akiwaambia waandishi wa habari jijini Arusha, kuwa anaerwa na ziara za Lissu ughaibuni.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

Habari za SiasaTangulizi

Samia ataja miradi ambayo Tanzania inashirikiana na IDA

Spread the loveRais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu amehutubia...

error: Content is protected !!