SHURA ya Maimamu Tanzania, imewasilisha pongezi zake kwa Serikali ya Afrika Kusini, kufuatia uamuzi wake wa kuishtaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ikiituhumu kwa mauaji ya halaiki katika vita inayoendelea ukanda wa Gaza dhidi yake na kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Pongezi hizo ziliwasilishwa na viongozi hao wa kiislamu katika Ubalozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, tarehe 24 Januari mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, amesema “Tumepeleka salamu kwa Balozi wa Afrika Kusini, sehemu ya waraka wetu inasema ingawa hukumu ya mahakama ya kimataifa haijatoka lakini tayari mmeshinda katika mahakama ya ubinadamu na mahakama ya maoni ya watu. Kitendo chenu kimegusa nyoyo na akili za mamilioni ya watu duniani.”
Kupitia waraka huo wa Shura ya Maimamu kwenda kwa Afrika Kusini, wamesema uamuzi wao huo umerejesha imani kuwa ubinadamu haujafa na kuchochea ari ya kupigania haki za Wapalestina.
Mapigano kati ya Hamas na Israel yaliibuka Oktoba 2023 baada ya wanamgambo wa kundi hilo kufanya mashambulizi ya kushtukiza yaliyosababisha mauaji ya maelfu ya watu wengi wao wakiwa waisrael.
Baada ya shambulizi hilo, Israel ilijibu mapigo kitendo kilichoibua muendelezo wa vita iliyopoteza maisha ya maelfu ya watu.
Leave a comment