MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeamua kusikiliza mapingamizi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na Mawakili wa Mbunge wa viti Maalum (Chadema), Halima Mdee na wenzake 18 kabla ya kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo. Anaripoti Faki Ubwa… (endelea)
Jaji Cyprian Mkeha alitoa uamuzi huo jana tarehe 2 Septamba 2022, kutokana na majibizano ya hoja za mawakili wa upande waombaji kina mdee na zile za wajibu maombi namba moja (Chadema).
Kwenye shauri hilo namba 36 la mwaka 2022 Mdee na wenzake wanawashtaki Chadema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (A. G).
Upande huo unawakilishwa na Ipilinga Panya, Edson Kilatu, Emmanuele Uhashu, na Aliko Mwananenge. Huku Stanley Kaloka akiongoza jopo la Mawakili wa Serikali kwa ajili ya mjibu maomba namba mbili NEC na namba tatu AG.
Upande wa wajibu maombi namba moja (Chadema) uliongozwa na Wakili Peter Kibatala, Jeremiah Mtobesya, Omary Msemo, Dickson Matata, Suleiman Makauka, Deogratius Mahenyela.
Awali tarehe 26 Agosti shauri hilo lilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji ambapo Mahakama ilitoa amri ya kufika kwa Mdee na wenzake saba kwa ajili ya kuhojiwa na upande wa mawakili wa Chadema.
Mdee na wenzake walifika lakini mawakili wao waliibuka na hoja ya kupinga kuhojiwa na kuendelea na usikilizwaji kwa kupinga kiapo kinzani cha upande wa wajibu maombi namba moja (Chadema) kwa kudai kuwa kinakasoro zitakazoathiri mwenendo wa shauri hilo.
Jana Jaji Mkeha alipokuwa anatoa uamuzi wake alisema atasikiliza pingamizi hilo kwa kuwa utaratibu unaolekeza kuwa huwezi kuendelea kusikiliza shauri kukiwa kuna mapingamizi.
Alisema kuwa wakati shauri hilo linaanza, mawakili wa pande zote walikuwa wanakiu ya shauri hilo lisikilizwe mapema na kuahidi kutokuweka mapingamizi yatakayokwamisha usikilizwaji wake.
Jaji Mkeha aliendelea kuwakumbusha mawakili ahadi yao hiyo huku akisema kuwa tarehe 26 Agosti, 2022 upande wa waombaji ulikwenda kinyume na ahadi yao kwa kuweka pingamizi la kutoendelea kusikilizwa kwa shauri hilo mpaka lisikilizwe pingamizi hilo.
Leave a comment