Tuesday , 26 September 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Mabula, Masanja ‘out’, Makamba apelekwa mambo ya nje
Habari za SiasaTangulizi

Mabula, Masanja ‘out’, Makamba apelekwa mambo ya nje

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula
Spread the love

 

MABADILIKO madogo ya Baraza la Mawaziri, yaliyofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, yamegusa kwa namna tofauti baadhi ya mawaziri, ambapo wapo waliotemwa, waliohamishwa na kubakishwa katika wizara zao. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa mujibu wa mabadiliko hayo yaliyotangazwa mapema leo na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka, waziri aliyeachwa ni Dk. Angelina Mabula, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, baada ya nafasi yake kuchukuliwa na Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa.

Mwingine aliyeachwa kwenye mabadiliko hayo, ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Marry Masanja, ambaye nafasi yake imechukuliwa na Mbunge wa Mkinga, Dustan Kitandula.

Mbali na mawaziri hao kuachwa, katika mabadiliko hayo Rais Samia amewahamisha kwenye wizara baadhi ya mawaziri na manaibu waziri.

Miongoni mwa mawaziri waliohamishwa ni aliyekuwa Waziri wa Madini, Dotto Biteko, ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu, pamoja na kuhamishwa kuwa Waziri wa Nishati, akichukua nafasi ya January Makamba, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Nafasi ya Biteko katika Wizara ya Madini, imechukuliwa na Anthony Mavunde, aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo. Rais Samia amemteua Mbunge wa Misungwi, Alexander Mnyeti, kujaza nafasi ya Mavunde katika wizara ya kilimo.

Waziri wa Madini, Dotto Biteko

Waziri mwingine aliyehamishwa ni aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa, aliyeteuliwa kuwa Waziri katika wizara mpya ya uchukuzi. Kwenye mabadiliko hayo, Rais Samia amemrudisha Dk. Stergomena Tax, kuchukua nafasi ya Bashungwa.

Kabla ya mabadiliko hayo, Dk. Tax alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Wengine waliohamishwa ni, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, aliyehamishiwa katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, akichukua nafasi ya Dk. Pindi Chana, aliyepelekwa kumrithi katika Wizara ya Katiba na Sheria.

Angellah Kairuki, aliyekuwa Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, amehamishwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, akichukua nafasi ya Mohamed Mchengerwa, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Mawaziri waliobakishwa katika wizara zao baada ya mabadiliko hayo, ni pamoja na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia avunja bodi ya REA

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua Balozi Jacob Kingu, kuwa...

Habari za SiasaTangulizi

Chande aliyeng’olewa TANESCO kwenda TTCL apelekwa Posta

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua aliyekuwa, Mkurugenzi Mkuu wa...

Habari za Siasa

Kamugisha aanika utekelezaji mpango kazi 2022/23

Spread the loveMWENYEKITI wa Ngome ya Vijana ya Chama Cha ACT-Wazalendo Mkoa...

Habari za Siasa

Vijana ACT-Wazalendo wakabidhiwa kivumbi kulinda kura uchaguzi 2024,2025

Spread the loveNGOME ya Vijana ya Chama cha  ACT-Wazalendo, imetakiwa kuwanoa wafuasi...

error: Content is protected !!