Tuesday , 26 September 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Bunge laridhia marekebisho ushirikiano anga Afrika
Habari za Siasa

Bunge laridhia marekebisho ushirikiano anga Afrika

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa
Spread the love

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limepitisha azimio la kuridhia mapendekezo ya Katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga ya Afrika ya 2009, yanayolenga kupanua wigo wa ushirikiano katika tasnia hiyo kwenye nchi wanachama. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Azimio hilo limepitishwa leo tarehe 30 Agosti 2023, bungeni jijini Dodoma, baada ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, kuwasilisha hoja ya kuomba wabunge kuridhia mapendekezo ya katiba hiyo, ili Tanzania ianze kuungana na mataifa mengine yaliyoiridhia na kuanza kutekeleza matakwa yake.

Prof. Mbarawa ametaja manufaa ambayo Tanzania itapata baada ya kuridhia katiba hiyo, ikiwemo kuendelea kunufaika na fursa za uongozi na ajira zitakazojitokeza ndani ya tume, kunufaika na tafiti zitakazofanyika kupitia miongozo ya tume, pamoja na nchi kukidhi viwango vya taasisi za kimataifa zinazosimamia usafiri wa anga, ikiwemo mipango ya kuongoza ndege.
“Kazi ya katiba hiyo itakuwa ni kukuza na kuratibu miundombinu, utoaji mafunzo na kuendeleza rasilimali watu katika tasnia ya usafiri wa anga, kusaidia katika uanzishaji mamlaka ya usafiri wa anga zinazojitegemea, kuunda mikakati ya pamoja kupata rasilimali za kuwezesha usafiri wa anga kimataifa na kuwezesha nchi wanachama kushirikiana, pamoja na kulinda maslahi ya nchi wanachama katika majukwa ya kimataifa,” amesema Prof. Mbarawa.

Waziri Mbarawa aliwataka wabunge kuridhia katiba hiyo, akitaja mafanikio mbalimbali ambayo Tanzania iliyapata baada ya kuridhia katiba ya awali ya 1969, ikiwemo nchi kupata uwakilishi katika mabaraza ya kimataifa, ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuteuliwa kuwa mkaguzi wake na watalaamu wake kupata mafunzo na uzoefu juu ya usafiri wa anga.

Waziri huyo amesema, tume hiyo iliamua kuandaa katiba mpya, baada ya katiba yake ya awali ya 1969 kukabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kukosekana ushindani wa haki katika mikataba ya usafiri wa anga nchini, ikiwemo kutoruhusu makampuni mengine ya usafiri wa anga hususan binafsi yenye umikili wa asilimia 100 wa wawekezaji wa nje, kupewa leseni za utoaji huduma.

Amesema mapungufu mengine ni gharama kubwa za nauli za ndege, kwa safari za ndani na nje ya nchi kutokana na masharti ya utoaji leseni za huduma za usafiri wa anga, uwepo wa vikwazo katika udhibiti katika idadi ya miruko ya ndege na idadi ya abiria katika safari hizo kwa wiki inayotokana na kutofungua soko huru la ndege nchini.

Kabla ya azimio hilo kupitishwa, baadhi ya wabunge akiwemo, Leonard Chamuriho na Mbunge Viti Maalum, Sophia Mwakagenda, waliitahadharisha Serikali juu ya athari itakazoipata Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), katika ushindani wa soko la usafiri huo, kutokana na kukosa mtaji wa kutosha.

“Kukubali mkataba huu maana yake ni kuingia kwenye ushirikiano na ushindani wa kibiashara, je shirika letu lina uwezo wa kukabiliana na ushindani? Kwa kuwa tunakwenda kuingia kwenye ushindani wa kibiashara, lazima Serikali ikubali kufanya mabadiliko kwenye ushindani wa kibiashara ili tuweze kufaulu,” alisema Mwakagenda.

Aidha, Mwakagenda aliitaka Serikali ipitie upya kesi za madai za kitaifa ili kuepusha ndegeza ATCL kukamatwa zirukapo katika anga za kimataifa.

Kufuatia tahadhari hizo, wizara hiyo iliwahakikishia wabunge kwamba, Serikali imejipanga kukabiliana na ushindani utakaojitokeza kwenye biashara ya usafiri wa anga, huku ikisema mpango huo utawezesha ATCL kufanya safari za anga katika mataifa mengine.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia avunja bodi ya REA

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua Balozi Jacob Kingu, kuwa...

Habari za SiasaTangulizi

Chande aliyeng’olewa TANESCO kwenda TTCL apelekwa Posta

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua aliyekuwa, Mkurugenzi Mkuu wa...

Habari za Siasa

Kamugisha aanika utekelezaji mpango kazi 2022/23

Spread the loveMWENYEKITI wa Ngome ya Vijana ya Chama Cha ACT-Wazalendo Mkoa...

Habari za Siasa

Vijana ACT-Wazalendo wakabidhiwa kivumbi kulinda kura uchaguzi 2024,2025

Spread the loveNGOME ya Vijana ya Chama cha  ACT-Wazalendo, imetakiwa kuwanoa wafuasi...

error: Content is protected !!