Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mabadiliko tabia ya nchi tishio EAC
Habari za Siasa

Mabadiliko tabia ya nchi tishio EAC

Baadhi ya makazi ya watu katika Kijiji cha Kipwa mkoani Rukwa, yaliyozungukwa na maji ya mafuriko kutoka Ziwa Rukwa
Spread the love

 

WATAALAM wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wamekutana jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa athari za mabadiliko ya tabia ya nchi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wataalamu hao kutoka katika sekta ya majanga na mabadiliko ya tabia ya nchi ya EAC, wamekutana jijini hapa katika mkutano wao wa siku tatu, ulioanza leo Alhamisi tarehe 27 Mei 2021, hadi Jumamosi tarehe 29 Mei mwaka huu.

Akizungumza na wanahabari kuhusu mkutano huo, Mkuu wa Idara ya Mazingira na Maliasili EAC, Mhandisi Ladslaus Kyaruzi, amesema lengo lake ni kuweka mikakati ya kuwasaidia wananchi, juu ya kukabiliana na changamoto hizo.

“Tunakuja hapa kama EAC na nchi wanachama kuweka misingi sahihi, itakayosaidia mwananchi wa kawaida katika jamii kupunguza athari hizi. Tuko hapa siku tatu tukishirikiana pamoja na kuja na muongozo, utakaotupeleka mbele kukupunguza athari kwa ukanda huu,” amesema Kyaruzi.

Mkuu huyo wa mazingira EAC, amesema mkutano huo umeitishwa baada ya uwepo wa matishio ya athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, hasa mafuriko katika bonde la Ziwa Victoria na Rukwa, ukame na maporomoko ya ardhi.

Baadhi ya makazi ya watu katika Kijiji cha Kipwa mkoani Rukwa, yaliyozungukwa na maji ya mafuriko kutoka Ziwa Rukwa

“Kumekuwa na majanga mbalimbali kama mafuriko, ukame, nyumba zinaangukiwa na udongo na magonjwa mbalimbali. Ambayo yanasababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi, kwa mfano suala la mafuriko,” amesema Kyaruzi.

Kyaruzi amesema mabadiliko ya tabia ya nchi yanasababisha ukame, kuongezeka kwa maji katika Ziwa Victoria, hali inayoathiri uwekezaji wa hoteli zilizojengwa pembezeno mwa ziwa hilo, kwa ajili ya utalii.

“Majanga ni mengi, mfano ukame ambapo mkulima analima halafu mazao yake yanakauka, kitendo kinachosababisha kipato cha mkulima kupungua. Pamoja na majanga ya wadudu, tatizo lililokumba Tanzania inayopunguza uzalishaji wa mazao ya vyakula,” amesema Kyaruzi.

Kyaruzi amesema “hilo tatizo ni kubwa, mfano Ziwa Victoria maji yanaongezeka na sasa liko zaidi ya mita mbili, linasababisha hoteli za maeneo ya ukanda wa ziwa hazifanyi biashara.”

Amesema, athari nyingine ya mabadiliko ya tabia ya nchi ni kuongezeka maji katika Bahari ya Hindi, na kuathiri uzalishaji wa zao la mwani, katika nchi ya Tanzania na Kenya.

Mkuu wa Idara ya Mazingira na Maliasili EAC, Mhandisi Ladslaus Kyaruzi

“Kuna jamii zilikuwa zinaishi na kuzalisha mazao, katika nchi mbili Tanzania na Kenya, wana suala la uzalishaji wa mwani kwenye eneo la bahari, lakini sasa ni tatizo kubwa. Athari nyingine ni kujaa maji katika Bahari ya Hindi, inayosababisha watu kwenda kwa shida ufukweni na wanyama wanapungua katika hifadhi zetu,” amesema Kyaruzi.

Kuhusu jitihada zinazofanyika kukabiliana na athari hizo, Kyaruzi amesema nchi za EAC zinatekeleza Mkataba wa Mabadiliko ya Tabia ya Nchi wa Parisi, ulioasisiwa 2015 na kutarajiwa kumalizika muda wake 2030.

“Nchi zote zimefanya juhudi mbalimbali kukabiliana na tatizo hilo, 2015 tumekuja na kitu kinaitwa Mkataba wa Mabaidliko ya Tabia ya Nchi wa Parisi. Ambapo nchi zote zimeweka malengo hadi kufikia 2030, kusaidia juhudi za dunia za upunguzaji athari hizo,” amesema Kyaruzi.

Naye Jean Baptitse Havugimana, Mkurugenzi wa Sekta ya Uzalishaji EAC, amesema maazimio ya mkutano huo wa siku tatu, yatasaidia kukabiliana na changamoto hizo.

“Kwenye huu mkutano tunaweza kuongea na kuzungumza, kwa ajili ya kuweka mikakati ya kusaidia wananchi wa nchi zote za EAC. Na mikakati hii haitabaki ofisini, bali tutakwenda kuitekeleza kwa wananchi moja kwa moja,” amesema Havugimana.

Hali kadhalika, Havugimana amesema EAC itaboresha utoaji taarifa za mabadiliko ya hali ya hewa kwa wananchi, ili wapate taarifa sahihi juu ya mabaidliko, kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi katika masuala ya kilimo na mafuriko.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

error: Content is protected !!