MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Dk. Phillip Mpango, ameiagiza Wizara ya Kilimo, ichukue hatua za haraka kukabiliana na changamoto zinazorudisha nyuma sekta ya kilimo nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).
Dk. Mpango ametoa agizo hilo leo Alhamisi tarehe 27 Mei 2021, akifunga maadhimisho ya kumbukizi ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Hayati Edward Moringe Sokoine, yaliyofanyika Chuo Kilimo cha Sokoine (SUA), mkoani Morogoro.
Sokoine aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, katika vipindi viwili tofauti, 1977 hadi 1980 na 1983 hadi tarehe 12 Aprili 1984, alipofariki dunia.
Makamu huyo wa Rais Tanzania, ameiagiza wizara hiyo kuufanyia marekebisho mfumo wa ugani, ikiwemo kutanua wigo wa utoaji huduma za ugani maeneo ya vijijini.
“Eneo moja muhimu ambalo nafikiri Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, hazina budi kushughulikia kwa nguvu ni kufikisha huduma za ugani kwa wakulima vijijini.
Mfumo mzima wa ugani, vitendea kazi vya maafisa ugani na ufuatiliaji utendaji kazi wao. Huu mfumo unatakiwa ufanyiwe marekebisho makubwa,” amesema Dk. Mpango.
Wakati huo huo, Dk. Mpango ameagiza kampuni zinazojishughulisha na biashara ya uuzaji mbegu, kujikita katika kuzalisha mbegu hizo nchini, badala ya kuagiza nje ya nchi.

“Uzalishaji na usambazaji mbegu bora nchini hauridhishi, nachukua nafasi hii kuzitaka kampuni zote zinazoagiza mbegu kutoka nje, zizalishe mbegu hizi hapa nchini. Narudia tena, nazitaka kampuni zote zinazoagiza mbegu kutoka nje zizalishe hapa nchini,” amesema Dk. Mpango.
Dk. Mpango ameiagiza Wizara ya Kilimo kusimamia utekelezwaji wa agizo hilo.
“Na Wizara ya Kilimo ijipange kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo haya, wasisubiri nitakapowauliza. Kama hawakusikia, nasema wasisubiri niwaulize,” amesema Dk. Mpango.
Wakati huo huo, Dk. Mpango ameagiza taasisi za umma, nazo kuongeza juhudi katika uzalishaji mbegu nchini.
“Lakini taasisi zetu za Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa, lazima zijidhatiti zaidi katika uzalishaji mbegu bora. Nawataka wakuu wa taasisi hizi wajipime utendaji wao wa kazi katika hili, tumechelewa sana, hatuwezi kwenda kuwa uchumi wa kipato cha kati cha juu kwa mwenendo wa tija hii ya mazao,” amesema Dk. Mpango.
Leave a comment